Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
ACT
Constituent
Ukonga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BAKARI B. SHINGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii tena ya kuchangia Wizara yetu ya Nishati. Kwanza kabla sijaenda mbele ninaomba nimwambie ndugu yangu Waziri kwamba, shida ya ukatikaji wa umeme pia, katika jimbo langu imekuwa ni jambo la kawaida, hasa Kata ya Gongo la Mboto, Kata ya Pugu Station na Buyuni, imekuwa inajitokeza mara kwa mara.
Mheshimiwa Naibu Spika, jana peke yake imejitokeza mara mbili kwa hiyo, ninaomba kwa umuhimu wake, Mheshimiwa Waziri, aone namna ya kumalizia hili tatizo ambalo ukiliunganisha linaweza likachukua zaidi ya miezi miwili sasa. Kwa hiyo, imekuwa ni karaha na hasa ukizingatia kwamba, jimbo langu lina wafanyabiashara wengi, machinga na kadhalika na umeme ndiyo sehemu pekee sasa hivi ya ukombozi wa uchumi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama unavyojua, ili tuweze kuvuka ni lazima tutumie umeme. Katika Jimbo langu la Ukonga yapo maeneo ambayo kwa sura ya kawaida ya kimipaka yanaonekana kwamba, ni maeneo ya Jiji la Dar es Salaam, lakini kiuhalisia ni kama tupo kijijini; Kata kama ya Zingiziwa, Chanika, Buyuni na Pugu Station. Hizi ni kata ambazo, kama unapita kwenye barabara ya lami kila siku unaweza ukahisi huko nyuma ndiyo maisha yalivyo, lakini huko nyuma kuna misitu, Msitu wetu maarufu wa Zingiziwa, ukitembelea maeneo yale utakuta zaidi ya mita na 100 hakuna miti mikubwa, hii maana yake ni nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake ni kuwa wananchi wa pale wanajikimu kwa kutumia miti ile kufanya kuni. Katika mazingira hayo ninaamini inatokana na hali ya uchumi wa wananchi wa jimbo lile, katika hayo maeneo, wanashindwa kubeba gharama za malipo ya umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitatolea mfano kwa bei za TANESCO, kuanzia mita sifuri hadi mita 30 ni shilingi 321,000 na kwa mita sifuri hadi mita 70 ni shilingi 515,000 na mita sifuri hadi mita 120 ni shilingi 796,000 na kidogo. Pia, ukienda vijijini huko ambako kuna huduma ya REA utakuta nako mita sifuri hadi 30 ni shilingi 27,000, lakini ikizidi hapo gharama zinafanana, kama hizi ambazo nimetaja hapo juu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa katika hali ya kawaida ya wananchi wetu pesa hizi ni nyingi sana, kwa hiyo, ninaomba Mheshimiwa Waziri na cabinet yake na Serikali waangalie mpango wa makusudi. Huko nyuma tulikuwa na utaratibu wa mwananchi asiyekuwa na cash anaruhusiwa kulipia kidogo kidogo, bahati mbaya ule utaratibu sijui ulifutwaje, ambapo sasa haupo, lakini yapo maneno ambayo yamekuwa siyo rasmi.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba, mimi ni mtaalam wa umeme kwa hiyo, haya mambo nayajua. Kumekuwa na taarifa zisizo rasmi kwamba, kumekuwa na baadhi ya wananchi waliodhaminiwa kulipa kidogokidogo wakawa hawalipi, lakini ninaamini kwamba, inawezekana pia, kwenye shirika letu kulikuwa kuna uzembe wa kiutendaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii tunaona kodi za majengo zinalipwa kwa ufanisi kupitia bili za umeme tunapowenda kununua units. Sasa kwa kuwa, sasa hivi tupo kwenye hali ya tahadhari na mazingira na kata hizo nilizozitaja, kama zinavyojulikana kijiografia zipo kandokando ya misitu yetu, ninaomba sasa kwa umuhimu wa pekee kwa jimbo langu na majimbo mengine kwamba, Serikali irudi kwa utaratibu ule wa wananchi kuchangia 25% angalau ya gharama halisi ya kuvuta service line, halafu gharama inayofuata wachangie asilimia mbili kila wanapoenda kununua zile units. Hakika ndio njia sahihi, ambayo itakwenda sambamba na kunusurisha misitu hasa kwetu Kazimzumbwi na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kwa umakini, tukiondoa uvivu wa baadhi ya watendaji wa shirika, tunaweza kujikuta tunafanya vizuri. Hivi tunavyozungumza habari ya Mradi wa REA ninashukuru na baadhi ya Wabunge wenzangu hapa wanazungumzia umuhimu wa Miradi ya REA na umuhimu wa bei, wanazungumzia jinsi bei za TANESCO zilivyo juu. Ili tutoke ni lazima tuweke utaratibu ambao utawawezesha wananchi wetu kulipa kidogokidogo, kama ambavyo tunalipa kodi za majengo, tulipe hivyohivyo na ninaamini inawezekana kwa sababu, umeme ndiyo kila kitu.
Mheshimiwa Naibu Spika, huko nyuma, ili uweze kupika, uwe na jiko na uweze kutumia umeme; ilikuwa inahitajika uwe na matumizi ya wastani wa current inayoanzia 15 kwenda hadi 45, wakati wa majiko yale ya plate, enzi za coil, lakini kwa sasa tumepata teknolojia mpya, tuna majiko madogo yanayotumia current ndogo kati ya tano hadi 12. Kitendo hiki maana yake ni kinakuja kutupunguzia gharama za uendeshaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni gharama sana kutumia gesi kwa sasa kuliko kutumia umeme kwa kupikia. Ni gharama sana kutumia mkaa na kuni kuliko kutumia majiko ya kisasa. Kwa hiyo, ninamwomba Mheshimiwa Waziri ni ndugu yangu, jamaa yangu wa karibu, aangalie hili jambo kwa umuhimu wa namna hiyo. Siyo mara zote tufanye uwekezaji wa kulipa leo, tumeona uwekezaji mzuri na mkubwa tunaoufanya kule kwenye Viwanja vya AFCON, uwekezaji mkubwa sana Arusha na viwanja vingine vidogovidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunawekeza kule tukiwa na maana tutapata baada ya kuwa viwanja vimekamilika kwa hiyo, style hiyo hiyo tuitumie pia, kuwekeza kwa wananchi wetu kuhusu suala la umeme. Kwa hiyo, tusione ubaya kuweka mabilioni kuwawezesha wananchi wetu kupata huduma ya umeme kwa lengo la kuondokana na uchafuzi wa mazingira na pia afya zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninajua ndugu zangu, watani zangu Wasukuma, wakati wanatumia yale mabaki ya maji ya chakula cha ng’ombe, akinamama wengi wamekuwa wanapata shida ya macho mekundu, lakini pia, hata kwangu kwenye jimbo langu, matumizi ya kuni yanaleta sababu ya macho kuwa mekundu. Ile ni athari kiafya kwa hiyo, tuondokane na hiyo hali hasa ukizingatia kwamba, tunatakiwa tubadilike kwa sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, twende kwenye suala ambalo ndiyo linaonekana lipo kimjini sasa hivi. Tuna ombwe kubwa la bei ya mafuta, bei ya mafuta inasababishwa na wababe duniani na Waswahili wanasema wapambanapo fahari wawili, ziumiazo ni nyika. Sisi tunakubali tunakwenda kuumia, lakini ninaiomba Serikali, kwa makusudi kabisa kwamba, sasa ifike wakati ipunguze tozo, angalau kwa shilingi 300, wakati huo iweze kuongeza ruzuku kwa shilingi 300, utakuta tunakuwa tumeokoa karibu shilingi 600. Kwa mwananchi wa kawaida huko tunakotoka utakuwa ni msaada mkubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama unavyojua siku zote, baba kwenye mji ndiyo anabeba gharama za uendeshaji wa maisha ya familia yake nyumbani, ama kama mama ni mwenye mji ndiyo anabeba gharama zote za uendeshaji wa familia nyumbani. Kwa hiyo, ninaiomba Wizara na Serikali kwa ujumla, kwa jambo hili, ikubali tu kulivaa kama bomu tuweze kuvuka.
Mheshimiwa Naibu Spika, inawezekana wababe wakaendelea kupigana ikasababisha ongezeko la bei zaidi, lakini siyo maana yake tuogope, tupambane kadri ya hali itakavyokuwa, lakini Serikali iangalie katika hayo mazingira. Katika mtazamo wetu huu na kwa kuwa tupo hapa kwa malengo yanayofanana, pamoja na majukumu ya Wabunge ya kuisimamia na kuishauri Serikali na kadhalika; Serikali pia, yenyewe ina majukumu ya kuangalia watu wake. Ukifanya tathmini ya Wabunge tulio wengi humu ndani tumechangia tukizungumzia habari ya hizi bei na upatikanaji wa huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, tafsiri yake ni kwamba, wawakilishi wa wananchi walio wengi tunawakilisha shida ambayo ndiyo maisha tunayoishi nayo kule kwetu. Kwa hiyo, ninaomba kabisa Wizara kwa makusudi kabisa ichukulie hata uchangiaji wa Wabunge tulio wengi juu ya hoja ya kurahisisha masharti ya wananchi kupata umeme iwe ndio dira na uelekeo wa Wizara.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niishie hapo. Ninaomba kuwasilisha hoja yangu. Ahsante sana. (Makofi)