Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbulu Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kupata wasaa huu. Ninachukua nafasi hii kwanza kwa namna ya pekee sana kuungana na Wabunge wenzangu na Watanzania kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa baraka zake mbalimbali katika Taifa letu na jamii kwa ujumla. Hatua hii ni kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachukua nafasi hii kumpongeza na kumshukuru sana Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali nzima ya Awamu ya Sita kwa kazi kubwa iliyofanyika ya usambazaji wa umeme katika majimbo yetu nchini. Kwa kweli, kwa namna ya pekee Wizara hii au Serikali kwa ujumla imefanya kazi kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, 2015 baadhi ya majimbo hapa nchini tulikuwa tunapokea umeme wa jenereta ama wa mitambo ya kuzalisha kwa mashine. Tulipofanya ziara maeneo mengine, kuna eneo tulikwenda wakati huo 2015 tukaambiwa ikifika saa nne usiku umeme utazimwa; leo walau kwa sehemu kubwa Serikali imepeleka umeme kwenye maeneo mengi. Hii ni hatua kubwa sana na hasa ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, lakini pia, upelekaji wa umeme kwenye maeneo yetu yote nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachukua nafasi hii pia, kumpongeza sana Waziri, ndugu yetu Mheshimiwa Ndejembi, Naibu Waziri, Wizara nzima na watendaji wote, kazi kubwa imefanyika na Wizara hii ni muhimu. Kila Mbunge hapa atakumbuka maswali na maoni mengi yaliyoulizwa na wananchi wakati ule wa uchaguzi; tulikuwa tunadaiwa sana usambazaji wa umeme, ufikishwaji wa umeme, kwenye maeneo yetu na sasa kwa ujumla, vitongoji vingi vimepelekewa umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni hatua kubwa sana kwa Tanzania. Ni hatua kubwa sana kuwa na umeme wa uhakika katika nchi yetu kwa sababu, Bwawa hili la Mwalimu Nyerere lisingekuwepo nchini, umeme huu tungeupata wapi? Tulishakuwa na kadhia ya umeme kukatika mara kwa mara. Kwa kweli, kwa namna ya pekee tunampongeza Mheshimiwa Rais na wale wote watangulizi wa Taifa letu waliotangulia mbele za haki, tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachukua nafasi hii kwa namna ya pekee kuipongeza sana Kamati yetu ya Nishati, imefanya kazi kubwa sana. Imechakata taarifa, imerahisisha kazi ya Wabunge kwa namna ya kuchangia na kutoa maoni yetu kwa Serikali. Kwa namna ya pekee wameleta taarifa ambayo imeonesha mafanikio, changamoto na pia, namna ya kuyafanyia kazi, kwa namna ya pekee, kwa maonesho ya Wizara, imekuwa kivutio na utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa eneo hili ni kwamba, tutumie media zetu kupeleka maonesho yale kwa Watanzania, ili waone fursa zilizopo pamoja na mafanikio na hatua iliyofikiwa na Taifa letu. Hatua hii ni kubwa sana kwa sababu, yale maonesho yanatuonesha Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere unatuonesha jinsi umeme unavyozalishwa na fursa nyingi zinazokuwepo nchini. Hongera kwa Wizara kwa namna ya pekee. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaeleza pia, umuhimu wa Serikali kuiomba ipeleke bajeti ya Wizara hii. Kweli, kama Wabunge, tunalo deni kubwa la umeme vijijini, deni la kila Mtanzania kuhitaji umeme; maeneo ni mengi, lakini fedha tunazopata Serikali inajitahidi sana kupeleka ingawa bado maeneo ni mengi sana. Mfano ni Jimbo langu la Mbulu Mjini, tunasura mbili, sura ya mji na sura ya vijiji; nina kata 10 zipo vijijini na kata saba zipo mjini.
Mheshimiwa Naibu Spika, pale mjini kati kuna nyumba ambazo hazijaunganishwa na umeme, kutokana na gharama kubwa ya uunganishaji wa umeme kwenye eneo hilo. Ninaamini miji mingi ipo hivyo, unakuta nyumba zilizo ndani ya mita 30 ni nyingi, pengine 70% kuliko zile ambazo zimeunganishwa na umeme. Wananchi wanaoishi mjini siyo kwamba, wote wana uwezo wa kulipa shilingi 300,000 na zaidi katika kuingiza umeme, wengi wao ni wakazi wa kawaida, ni wananchi wa kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee naiomba sana Serikali ije na utaratibu ambao, kama mpango mahususi wa muda mfupi wa maeneo hayo ya mji kuunganishwa hasa nyumba zote zilizo ndani ya mita 30, mita 25, ziunganishwe kwa shilingi 27,000 ili Watanzania waweze kunufaika na umeme. Pia, kwa namna ya pekee huu umeme tunaouita wa ziada uende kwa Watanzania walio wengi, ili waweze kunufaika na umeme na kupata fursa hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo langu la Mbulu Mjini kuna mitaa 58, takribani mitaa nane ni mwaka wa 11 haijafikiwa na umeme japokuwa umeme una miaka 14 katika Jimbo la Mbulu Mjini. Kwa hiyo, hali hii inasababisha wale wananchi wanapenda kuingiza huo umeme kwenye majengo yao, lakini namna ya kupata shilingi 360,000 na namna ya kufanya wiring kwa shilingi laki tatu pengine na kitu, jumla shilingi 700,000, fedha hizi ni nyingi sana kwa mwananchi wa kawaida. Shilingi laki saba siyo elfu sabini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, rai yangu kwa Serikali, iangalie utaratibu huu, Mheshimiwa Waziri ikimpendeza, nimemwomba mara nyingi aje atembelee Jimbo la Mbulu Mjini. Ni mji unaopakana na halmashauri nne; yaani kila Waziri aliyekuja kwenye jimbo langu alikuwa ananiuliza na huku ni mjini? Wale Mawaziri wote waliokuja kutoka 2015; lakini nikwambie kweli, ni mji gani unapakana na halmashauri kama nne nchini?
Mheshimiwa Naibu Spika, halafu sasa wale waliopo kule pembezoni wanaonekana wapo mjini katika tamko lile la Serikali. Ushauri wangu ni kwamba, maeneo hayo yafanyiwe tathmini, eneo la mji tuorodheshe majengo yote, ambayo yana sifa ya kuunganishiwa umeme tuone utaratibu wa umeme, tunatafuta programu ama mpango wa muda mfupi utakaokuwa unaleta marejesho hata kwa watumiaji baadaye, ili wananchi hawa ambao kwa muda mrefu wamesubiri umeme waweze kuunganishiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Programu ile ya UMETA, katika jambo hili wala tusifichane, kuna majengo ama kaya ndani ya hata miaka 15 hawajafikiwa na umeme kwa sababu, unakuta kwenye jiografia yetu tunavyoishi tuna milima na tuna umbali wa jengo hadi jengo. Majengo haya yapo mbali sana ambapo nyumba moja inahitaji nguzo 40 wakati sisi kwenye kitongoji tuna nguzo 20, hawa hawatafikiwa haraka.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa Serikali ni tutafute mpango wa kupata kile chombo cha UMETA, ili kwenda kuwawekea. Sasa hivi wananchi wengi vijijini wanatumia solar, kwa ajili ya kukodisha ama kukopa. Serikali ione fursa hii ya kupeleka hivi vyombo ama kile chombo cha UMETA kwa kila jengo ambalo linaonekana umbali uliopo hatuwezi kufikisha umeme kwa haraka, halafu tumkate kwenye matumizi wakati anatumia, mwananchi anaendelea kutumia umeme. Kwa nini ninazungumza hivi?
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwa sababu, nguzo 20 pengine zinaisha kwenye nyumba kama tano kwa mjini. Kwa sababu, nyumba moja itahitaji nguzo tatu ama nne hadi kufikiwa, lakini tukiwa na UMETA hiki chombo tulichotumia zamani, sasa hivi sijui kama tumebadilisha kwa jina lingine, lakini kina msaada mkubwa sana, kwa ajili ya kuwasaidia wananchi ambao wanalipa gharama kubwa katika kukodisha solar kutoka kampuni mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni, haya maeneo yanayohitaji ujazilizi yaainishwe, yapewe kipaumbele kwa kuzingatia majengo mengi na kwa kuzingatia ukaribu wa majengo, ili kuona kama zile nguzo 40 katika ujazilizi zinafikisha pengine hata nyumba 80 ama pengine hata nyumba 100 kulingana na jiografia ya majengo yalivyokaa. Ninaiomba Serikali yangu kwa namna ya pekee kuchukua hatua za kuainisha maeneo yenye fursa ya uwekezaji wa umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna eneo lenye uwezo wa kuzalisha umeme kule Mbulu ambalo linaitwa Maporomoko ya Mto Hhayno. Kampuni nyingi zimeenda, ninadhani ni kwamba, wakienda wakaona gharama ni kubwa wanaacha, lakini ninaona lile eneo ni fursa. Timu ya Wizara iende Mbulu Mjini ikatembelee Maporomoko ya Hhayno ione jinsi ambavyo ina fursa ya kuzalisha umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkondo wa Mto Hhayno maji yake yanatiririka mpaka katika Tarafa za Babati, lakini kwa kule juu kuna fursa ya kuzalisha umeme. Tuweze kuona maeneo kama haya na mengineyo, pamoja na umeme wa joto jua na wa upepo kwa maeneo haya, ili tuone fursa hizi Watanzania wanazishika na zinatoa mchango kwa Serikali na kuongeza uzalishaji wa umeme nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na yote niliyoyazungumza, Serikali ifanye utaratibu wa kufanya mapitio ya shule zetu. Tathmini inaonesha nyumba nyingi za walimu hazina umeme nchini na uwezo wa REA, mwananchi kupata shilingi 330,000 au yule Mwalimu kutoa shilingi 330,000. Mchango huu wa shilingi 330,000 au aongeze na sabini, ili afanye wiring, kwa Mwalimu ni shilingi 700,000 hataweza.
Mheshimiwa Naibu Spika, unakuta Mwalimu anakaa kwenye jengo ambalo halina umeme lakini REA imeshafika miaka mitatu. Maeneo hayo yawe na programu maalum na Waziri akija atoe maelekezo mahsusi ili nyumba zote za walimu, zahanati zote na makanisa pamoja na nyumba za watumishi wengine na yale majengo mengine ambayo kwa namna moja au nyingine yana fursa ya kutumia umeme kwa wingi na kwa mahitaji muhimu yaweze kuunganisha ili umeme wetu uwe na tija na Watanzania wanufaike kwa namna ya pekee. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na muda ninaomba niunge mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)