Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Haran Nyakisa Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. HARAN N. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, ninaomba nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, nami niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu ambayo imebeba maono ya mapinduzi ya uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa ninaomba nimpongeze sana Mheshimiwa Deogratius Ndejembi, Waziri wa Nishati, kwa kazi kubwa ambayo ameifanya toka amepewa jukumu hilo kubwa la kusimamia Wizara ya Nishati na Madini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninasema hivyo nikiwa ninatoa na ushahidi kabisa, mimi ni Mbunge labda inaweza kuwa ni wa kwanza toka huyu amepewa majukumu haya kufika kwa haraka sana pale ambapo Jimbo langu la Kigamboni lilipata tatizo la low voltage, alifika na kuhakikisha ametoa maelekezo. Ninawashukuru wale wataalam waliweza kuyapokea yale maelekezo na kuyafanyia kazi, mpaka sasa tuna umeme mzuri, wananchi wanafurahia na wanaendelea kuisifu Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nishati ya umeme kwenye kitabu chetu cha dira imeainishwa kama ni kichocheo namba mbili cha kuleta mapinduzi ya uchumi wa Tanzania kuelekea 2050. Sekta hii ya nishati ndiyo ambayo imebeba jukumu kubwa la kuleta mapinduzi ya kiuchumi. Pia nimpongeze Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza hela nyingi katika sekta hii ili kuhakikisha maono yake ya mapinduzi ya kiuchumi Tanzania yanaenda kutokea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unaweza kuangalia kwa mifano, ujenzi wa SGR unategemea kiwango kikubwa sana cha supply ya umeme na Mheshimiwa Rais ameanza hatua kwa hatua, amesimamia ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ambalo mpaka leo hii tunavyoongea linatoa megawati 2,145, kiasi kwamba inasaidia kwa kiasi kikubwa uendeshwaji wa treni yetu hii ya umeme ya SGR. Hii ni hatua kubwa sana katika Taifa la Tanzania, East Africa pamoja na Afrika kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nimesimama hapa kupongeza kwa sababu Jimboni kwangu kule Kigamboni umeme umesambaa kila mahali, lakini Mheshimiwa Waziri kuna vitongoji vichache pale Pemba Mnazi na Kimbiji ambavyo vinahitaji jicho la ziada la Waziri ili viweze kupata umeme na tatizo la umeme kule Kigamboni libaki kuwa historia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaiomba Serikali yangu iweze kuongeza nguvu ya umeme kwa kujenga Kituo cha Kupooza Umeme kingine pale Kisarawe II, tuliongea Waziri nina imani hili analijua na hii bajeti tunayoichangia sasa hivi mradi huu nina imani kabisa utakuwemo. Kwa hiyo, niombe sana, kwa sababu Kigamboni kwa sasa hivi inakua kwa kiasi kikubwa cha ujengaji wa viwanda vikubwa na hatua hii ina mahitaji makubwa sana ya umeme. Kwa hiyo, nimwombe Waziri kile kituo asikiache katika miradi yake ambayo atakuwa ameshaipanga ili wafanyabiashara na wawekezaji waweze kufurahia Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza na kujenga imani katika uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nishati ya umeme imeleta mchango mkubwa sana wa kibiashara katika pato letu la Taifa. Ukiangalia katika ile randama ya Mheshimiwa Waziri amezungumzia kwamba Tanzania pia katika East Africa, sisi pia tunauza umeme nje ya nchi, tunauza umeme Kenya, tunauza umeme Rwanda, tunauza umeme Zambia. Hizi zote ni fedha za kigeni ambazo zinaingia kwenye pato letu la Taifa. Ninaomba nimwambie Mheshimiwa Waziri achape kazi, sisi Waheshimiwa Wabunge tunaangalia na tutamsaidia na tutam-support kwa asilimia zote kuhakikisha malengo yote ya Wizara yanaenda kukamilika bila matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika sekta hii ya nishati, imeimarisha ukuaji wa sekta ya madini namna gani? Ukianza kuangalia migodi mikubwa ya dhahabu, nickel, graphite sasa inatumia umeme, zamani walikuwa wanatumia majenereta, walikuwa wanatumia makaa ya mawe. Haya yote ni maendeleo ya sekta hii ya nishati na mipango madhubuti ya Wizara kuhakikisha wameleta mapinduzi ya uchimbaji kwa kutumia umeme, ambapo wanatumia muda mfupi na uwezekano wa upataji wa dhahabu unakuwa ni mkubwa, ambao unaleta mapato kwa Taifa kwa maana ya ile royalty. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninatoa tu tahadhali au ushauri kwa Mheshimiwa Waziri, Kigamboni ni Wilaya pekee Tanzania inayotunza nishati ya mafuta, matenki yote ya mafuta kasoro matenki sita ambayo yako Mtwara, yapo Kigamboni, lakini Kigamboni hatujaweka miundombinu rafiki ya fire. Ninamwomba sana ashirikiane na Wizara ya Mambo ya Ndani ili tuweze kuwekeza kituo kikubwa cha fire kwa maana ya kuhakikisha yale matatizo ya moto yanapotokea kunakuwa na rescue ya karibu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake tumeshapata matatizo kama haya mara mbili, lakini fire mpaka itoke kule Geza mpaka ije ifike huku inakuwa imeshachelewa na unajua ile ni sehemu ya mafuta yanakuwa yameshapotea kwa kiasi kikubwa sana. Nimwombe sana Waziri jambo hili alizingatie na alifanyie kazi, kwa sababu hata Rais mwenyewe anaendelea kufanya uwekezaji. Juzi ametoka kuzindua matenki sita ya storage ya mafuta, lakini haya yote yanakwenda kuwa na tija pale ambapo tunaweka na vitu ambavyo vinaweza kusaidia pale ajali zinapokuwa zinajitokeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nimechangia kwa maana ya kumpongeza Waziri na kwa niaba ya wananchi wangu wa Kigamboni wananisikia sasa hivi wanampongeza katika ma-group mbalimbali kwa namba ambavyo anafanya kazi. Ninamshukuru sana kwa sababu aliridhia lile ombi langu ambalo nilimwomba kwamba Kigamboni imekuwa kubwa na akaamua kuniletea Mameneja wa Wilaya wawili. Hivi sasa ninaomba nimpe taarifa, wamefika wako site wote wanafanya kazi na mmoja leo hii Meneja wa Mkoa amekuwepo hapa Dodoma kwa ajili ya maonesho ya nishati safi ya umeme. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ina dhamira ya kweli ya dhati kuweza kuleta mabadiliko katika Taifa letu la Tanzania. Pamoja na haya mambo yote, niwaombe Wabunge tufike hatua ya kuishauri Serikali yetu vizuri. Pia tutakuwa tunamsaidia Mheshimiwa Rais kama kila Mbunge wa hapa ndani akibeba yale yote ambayo yakifanyika katika Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuyapeleka kwa wananchi kisawasawa, wananchi wakapata uelewa, ninadhani dhana ya umoja katika Taifa hili itakuwa ni kubwa na itakuwa na tija na italeta mapinduzi na morali ya wananchi wa Tanzania kuweza kufanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda, ninaomba kuunga mkono hoja na ninakushukuru sana. (Makofi)