Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Anne Kilango Malecela

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Same Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya na uhai. Niwapongeze Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Naibu Waziri, Katibu Mkuu kwa kutuletea hotuba nzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kuchangia nizungumze kitu kidogo. Mimi ninasema kwa moyo wangu wa dhati kabisa, ninawapongeza sana wakulima wa Tanzania wote kwa ujumla wao. Hakuna Taifa ambalo linapaswa kujivuna kama Taifa linalojitosheleza kwa chakula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tunajitosheleza kwa chakula kwa sababu wakulima wamesimama imara, na wanafanya kazi bila kuchoka. Ninamwomba Mheshimiwa Rais akisimama, anapoongea, ajivunie kwamba anaongoza Taifa ambalo linajitosheleza kwa chakula 128% na linalisha na nchi nyingine jirani ambazo hazina chakula. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, itoshe, sasa nianze kuchangia hotuba hii ya kilimo kwa vipande viwili. Nitaanza kwa umuhimu wa sekta ya kilimo nchini. Kwanza, kilimo ndicho kinachotupatia chakula Watanzania. Kwa hiyo, umuhimu wa kilimo ni kwamba tunapata chakula cha uhakika. Kama sasa hivi nimetoka kusema kwamba kilimo kimetupatia chakula takribani 128% hadi asilimia 130.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kilimo, kidogo jamani tunachangia, watu msubiri kidogo, kilimo ndicho kinachosaidia sekta ya viwanda ikue kwa sabbau kinahakikisha kwamba kinatoa malighafi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, kilimo kinachangia takribani 30% ya pato la Taifa. Kilimo kinatoa ajira kwa 65.5%. Sekta ya kilimo inatoa 65% ya malighafi inayotumika kwenye viwanda. Kilimo ni uti wa mgongo, kwa sababu kinachangia takribani 56% ya fedha za kigeni katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninaiomba Serikali, kwa sababu ya umuhimu wa kilimo, yote hayo niliyozungumza sasa ninaiomba Serikali ifanye jitihada ya kupima ardhi ili ijue mbolea ya kutumia isitumie mbolea tu ambayo Jimbo langu la Same Mashariki ni Jimbo la Kilimo lakini wakati mwingine niseme ukweli, kwamba, Serikali wanapeleka mbolea sehemu ambazo hiyo mbolea haihitajiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaiomba Serikali wawe wanapima ardhi ndipo wapeleke mbolea. Pia, Serikali ifanye jitihada sana ya kuwafikishia wakulima mbolea kwa wakati, hili ni tatizo. Serikali haifikishi mbolea kwa wananchi kwa wakati, na wakati mwingine wanapeleka ya kupandia, wananchi hawahitaji ya kupandia. Pia Serikali wahakikishe wananchi wanapata mbegu nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, upajikanaji wa pembejeo ni kitu muhimu sana. Sasa, ili wananchi waweze kulima vizuri na wapate asilimia kubwa watulishe Watanzania na nchi Jirani, lazima Serikali nao wajitahidi sana kuhakikisha kwamba vile vyote vinavyohitajika wanavipeleka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niingie kwenye suala la umwagiliaji. Nimshukuru sana Mheshimiwa Rais pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo. Mimi jimbo langu linalima mazao makubwa mawili; linalima tangawizi, pia linalima mpunga na mahindi. Mazao yote niliyoyazungumza yanahitaji umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepata fedha za umwagiliaji. Kwanza ninaishukuru Serikali, fedha za kwanza ambazo wameniletea nimepata mradi wa shilingi bilioni 1.7. Huu ni mradi wa Kata ya Myamba na sasa hivi upo kwenye matazamio. Mradi wa pili wa umwagiliaji ni mradi wa shilingi bilioni 6.9 ambazo zimekwenda Ndungu na Kihurio.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa unyenyekevu mkubwa ninamshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan, ninaishukuru sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Sasa hivi tunamalizia Aprili, mwezi Januari Serikali imenipatia shilingi 44,159,672,317.40. Ninamshukuru Mheshimiwa Waziri sana, ninamshukuru mno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha hizi zimeletwa jimboni kwangu kujenga bwawa la umwagiliaji, kwa sababu sasa wanaolima tangawizi ni Tarafa ya Mamba Vunta na Tarafa ya Ndungu, wao ndio walioko milimani na ndiyo chanzo kikubwa cha mito. Wao kwa sababu wanalima tangawizi sana, yale maji ya kule juu yote wameyachukua. Wananchi wanaolima mpunga tarafa ya chini wanakuwa hawana maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ikaona, ikaja ikanipa shilingi bilioni 44, inanijengea sasa bwawa kubwa sana. Bwawa hili linajengwa kwenye Kata ya Lugulu Kijiji cha Vumba. Bwawa hili litahudumia takribani wakulima 21,523. Bwawa linatarajiwa kuanza kuhifadhi takribani lita bilioni 5.84, na bwawa hili litahudumia Kata ya Ndungu na Maore. Mkandarasi ameanza ujenzi tarehe 11/2/2026. Niliondoka kama siku nane hivi kwenda kumwona mkandarasi. Bwawa hili linatarajiwa liwe limekamilika tarehe 10/2/2029. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Same Mashariki, nasimama hapa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Wakulima wanahitaji umwagiliaji sana, na 100% ya wananchi wa Same Mashariki ni wakulima. Ni kweli tunapata mvua, lakini mvua haitoshelezi, tunahitaji sana umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa fedha hizi na bwawa hili ambalo linakwenda kujengwa sasa, ni lazima wananchi wale wamechanganyikiwa niseme ukweli. Ndiyo Waheshimiwa Wabunge niwaambie, watu hamjui ni kiasi gani Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anapendwa na wananchi. Wananchi wanampenda Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan sana kwa sababu anajali wakulima mno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisingependa kusema zaidi, niseme Mheshimiwa Waziri wa Kilimo apokee shukurani kutoka kwa wananchi wangu, japo Mheshimiwa Waziri hanitazami, lakini naomba anitazame kujua kweli kwa unyeyekevu mkubwa, namshukuru sana. Ninamshukuru Mheshimiwa Rais, ninamshukuru Naibu Waziri wake, ambaye ninamwomba baada ya kumaliza bajeti hii, tusafiri naye twende akamwone mkandarasi yule, akauone na Mto wa Saseni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli mimi sina cha kulalamika, ninaishukuru sana Serikali, upande wa kilimo jimboni kwangu, ahsanteni sana. (Makofi)