Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia muda wa kuchangia. Waheshimiwa Wabunge, safari yetu ya mwaka 2050, gari au injini kubwa itakayotufikisha huko ni kilimo, lakini kufika huko lazima uchumi ukuwe kwa kiasi cha 10% kufikia ile dola trilioni moja, na ile fedha ya mtu mmoja mmoja dola 7,000, ni kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo kama mnakumbuka mwezi Februari nilitoa mchango wangu hapa nikasema, kufanikiwa vision 2050, kilimo kichangie 35% ya GDP, halafu uchumi wa gesi uchangie 25%, halafu uchumi wa madini 20% na utalii 15%. Sasa nitatoa mapendekezo, lakini kwanza nianze kwa kusema kwamba, kwa niaba ya wananchi wa Musoma Vijijini naiunga mkono hii bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Wizara inafanya vizuri na viongozi wa Wizara wanafanya vizuri, na isitoshe tarehe tisa mwezi wa Tano, 2026 tunaenda kumkabidhi mkandarasi mradi mkubwa ambao ulianzishwa na Mwalimu Nyerere mwaka 1974. Tumekaa miaka 52 mradi umesimama. Shukrani za kipekee sana apelekewe Mheshimiwa Rais, kwa sababu amefufua kitu ambacho kilikuwa kimesimama toka mwaka 1974 mpaka leo hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, mafanikio ya kilimo ni lazima tuwe tunayatathmini kama kweli tunaenda vizuri, na tathmini ya kwanza kabisa ni mfumuko wa bei. Mfumuko wa bei, mchango mkubwa ni bei ya chakula sokoni. Mataifa yenye uchumi mkubwa, mfumuko wa bei ukifikia asilimia mbili wanalalamika sana. Uchumi mdogo unaoendelea kama wa Tanzania haupaswi kupata mfumuko wa bei zaidi ya 5% kwa mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunafanya vizuri, tuko chini ya 3.5%, kwa hiyo, pongezi kubwa sana Wizara ya Kilimo, kwa sababu mmeweza kudhibiti mfumuko wa bei kwa kuhakikisha chakula kipo kingi cha kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipimo kingine cha mafanikio ya kilimo chetu ni food security. Tuna akiba ya chakula. NFRA inafanya vizuri, kwa hiyo inamaanisha Wizara inafanya vizuri na Serikali inafanya vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tathmini nyingine ni sera tulizojiwekea, zipo za hapa nchini. Ninachukua hizi kubwa kubwa kidogo; kwanza ya AU, Julai, 2003, palikuwa na Maputo Declaration, Marais wetu walionana Maputo, wakakubaliana kwamba nchi za Kiafrika, kwa kila mwaka angalau tutumie siyo chini ya 10% ya bajeti ya Taifa iende kwenye kilimo. Sasa bajeti aliyosoma Mheshimiwa Waziri ni shilingi trilioni 1.1 na ya mwaka 2025 ilikuwa ni trilioni 1.2. Sasa na ninyi Wabunge nawaachia zoezi la kufanya hesabu rahisi, chukua bajeti hii tuliyosomewa na bajeti ya 2025. Je, tumefika 10% kila mtu atapata jibu lake hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sera ya pili, vilevile ya AU 2014, Malabo Declaration, Equatorial Guinea. Marais walikaa wakasema tuongeze kasi kwenye ukuaji wa kilimo. Huwezi ukakua kati ya asilimia sita mpaka 10% kwa kila Taifa, halafu tuwekeze uwekezaji mkubwa. Hii Public Private Partnership haikuanza leo. Hata Marais wetu walisema tuwekeze kwenye kilimo zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kigezo kingine ambacho ni muhimu cha UN, SDG’s (Sustainable Development Goals). Goal namba mbili, inasema zero hunger by the year 2030. Yaani dunia nzima ikifika mwaka 2030 pasiwe na njaa, lakini tathmini imefanyika, dunia haijafanikiwa, kwa sababu mwaka 2025 karibu 23% ya wakazi wa duniani hapa walikuwa na misukosuko mikubwa sana ya upatikanaji wa chakula, ambayo imeongezeka kutoka 13% mwaka 2013. Kingine ni kwamba mwaka 2025, vijana, watoto milioni 35.5 walikuwa na utapiamlo. Kwa hiyo, hatujafanya vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote ninayaweka, unilindie muda wangu, kwa sababu nakuja kutoa mapendekezo kwa nini ninaweka nguvu tuweke nguvu kwenye kilimo cha mazao ya chakula, ndiko ninakoelekea huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, binadamu, yaani tuna Mataifa yote duniani, ni Taifa moja tu ambalo haliagizi chakula, linajitegemea. Binadamu anahitaji virutubisho saba (seven nutrients). Nchi pekee ambayo haiagizi, (hii ni ripoti imetoka mwaka huu) ni nchi ya Guyana, iko Latin America, kaskazini mwa Brazil. Guyana ndiko ilikuwa kwao Prof. Walter Rodney kwa wale waliosoma kitabu chake. Hiyo tu, ndiyo haiagizi chakula. Kwa hiyo, inamaanisha hata Mataifa makubwa yote yanahitaji kuagiza chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo yangu sasa, uchumi kufikia tulioupanga 2050 na sekta ya kilimo kuchangia 35%, cha kwanza, tuongeze utafiti mkubwa sana kwenye mbegu, seed research na utafiti mkubwa kwa kilimo kwa ujumla. Kama ambavyo huwa nawatolea mfano wa India na China, kwa mwaka China wanatumia dola bilioni 10 kufanya utafiti. India wanatumia shilingi bilioni sita kufanya utafiti. Kwa hiyo, sisi kufanikiwa Sekta ya Kilimo lazima tuongeze utafiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha pili, kilimo cha umwagiliaji. Tunaenda vizuri, lakini lazima tupanue umwagiliaji mkubwa na mdogo. Mkubwa ni kama huo unaoenda kufanyika Musoma Vijijini, lakini hapo sikia, umwagiliaji mkubwa; lile Bwawa langu la Bugwema, umwagiliaji wa Bugwema tunaoenda kumkabidhi mkandarasi tarehe tisa mwezi ujao, gharama yake ni shilingi bilioni 48.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwa na schemes kama hizo 10 karibu ni shilingi bilioni 500. Ninawaeleza, bajeti tu tunayoisoma hapa haiwezi kufanya mapinduzi makubwa ya kilimo cha umwagiliaji, haiwezi. Kwa hiyo, badala yake ni kama Wabunge wengine nimewasikia jana wanaongea. Ni lazima tutafute fedha za pembeni. Mataifa yote, hata waliofanya kazi kwenye mashirika makubwa wanajua. Kuna kitu kinaitwa extra budgetary funds, haziji kusomwa humu, lakini zinatafutwa kwa kazi mahususi na huko ndiko tuelekeze kwenye kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano ni kwamba, ukilima ngano kwa kutegemea mvua ya kawaida unavuta tani moja kwa ekari moja, lakini ikiwa ya kumwagilia ni kati ya tani tatu mpaka tano kwa ekari moja. Nchi inayofanya vizuri sana kwa ngano Afrika sasa hivi ni Ethiopia, kwa sababu ya umwagiliaji mkubwa kweli kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pendekezo la tatu, Tanzania lazima tuwe na viwanda vya zana za kilimo. Kilimo cha jembe la mkono hakiwezi kutekeleza vision 2050, hata cha mkokoteni. Kwa hiyo, zana za kilimo ni kwamba, nina mfano mzuri, sisi tuko chini sana, lazima tuongeze. Ukichukua trekta nchini Tanzania kwenye kila hekta 1,000, Tanzania tuna trekta 3.6, lakini India kwenye hekta 1,000 wana trekta 20, China hekta 1,000 wana trekta 45.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha nne tuwekeze kwenye viwanda vya mbolea. Kwa ile urea, kiwanda tunachotaka kukijenga kutokana na gesi yetu, hesabu zimeshapigwa, yaani TCF moja (One Trilion Cubic Feet) of natural gas inaweza ikazalisha tani milioni 28 za urea. Kwa hiyo, tuna gesi ya kutosha, hatuna sababu kwa nini tusiwe na viwanda vya mbolea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kwamba Watanzania tunatumia mbolea kwa kiasi cha chini sana. Tunatumia wastani wa kilo 20 kwa hekta moja, lakini wataalamu wa kilimo na FAO inasema angalau tutumie kilo 50 kwa eka moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho natoa maoteo ya biashara duniani, kwa nini twende kwenye mazao? Hili ndiyo la mwisho sasa wa maoteo. Soko la Dunia, kwa hiyo hakuna kusema kwamba hatuna masoko, dunia nzima ni soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2030 tutakuwa watu bilioni 8.5 duniani. Mahitaji ya chakula yanapaswa kuongezeka kwa percent kati ya 30 na 40 ya uzalishaji wa sasa. Mwaka 2050 tutakuwa watu duniani bilioni 9.7, mahitaji ya chakula yataongezeka kwa kati ya 50% na 70% ya uzalishaji wa sasa. Kwa hiyo, dunia inahitaji chakula, na Tanzania tuwekeze kwenye chakula, na thamani ya masoko nayo itaongezeka ndiyo pointi ya mwisho hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tulime mpunga mwingi? Mwaka 2033 thamani ya soko la mchele au mpunga duniani litakuwa la shilingi bilioni 392 na watu duniani 50% ya wakazi wa dunia hii wanatumia mchele, mpunga, utakavyouita kama chakula kikuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2033 soko la ngano duniani litakuwa la shilingi bilioni 270 na watu 40% ya wakazi wa dunia hii wanatumia ngano kama chakula kikuu. Hata kahawa, mikoa inayolima kahawa, soko la dunia mwaka 2034, kahawa itakuwa na thamani ya shilingi bilioni 380. Wale wa maua ifikapo mwaka 2030 Soko la Dunia litakuwa na thamani ya shilingi bilioni 52.

Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo, ninadhani nimeweza kuwashawishi kwa nini tujikite sana kwenye kilimo cha chakula kwa ajili yetu na kwa ajili ya dunia. (Makofi)