Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa fursa hii. Ni neema ya Mwenyezi Mungu amenijalia kuwa sehemu ya Bunge hili, tangu Bunge la Kumi na Moja na Bunge la Kumi na Mbili, lakini kwa mara ya kwanza tangu Mwenyezi Mungu anipe fursa ya kutambulika humu Bungeni na cheti na siyo orodha ya majina, ndiyo nimesimama hapa kuweza kutoa mchango. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, lakini kukishukuru sana Chama changu cha Mapinduzi, chini ya Jemedari Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kipekee ninawashukuru wananchi wa Jimbo la Kondoa Mjini, haikuwa rahisi, lakini yametimia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawatoa hofu, watu wafupi hatuna maneno mengi, lakini huwa tunaonekana kwa vitendo. Wawe na moyo wa subira, Ilani imeeleza vizuri, katika maendeleo, tunamwona Mheshimiwa Rais na Baraza aliloliteua wanaofanya kazi, basi mimi kiraka wao waje wanipime 2030 kwa maendeleo yatakayoonekana ndani ya Jimbo la Kondoa Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii, kama nilivyosema hiki ni kipindi cha tatu, na kila mtu anajua mimi ni mkulima kweli kweli. Ninaweza nisichangie hoja yoyote ndani ya mjadala wowote ama Mkutano wa Bunge, lakini sitaacha kuchangia kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajua, yako mambo huko nyuma tulikuwa tunashauri, lakini hayafanyiwi kazi mpaka yakatugusa. Kipekee ninampongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kweli mwanamama huyu tangu ameingia madarakani amekuwa pioneer wa namna ya kuwekeza fedha na vitendo kwenye Sekta ya Kilimo. Makofi mengi kwake Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tu niongee. Kuna wenzangu waliopata kuchangia jana walisema hatuna kipimo. Mimi ninaomba niwaambie, wakati anaingia madarakani Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, bajeti alikuta ilikuwa shilingi bilioni 294, lakini bajeti iliyomalizika kutekelezeka 2025/2026 ilikuwa shilingi trilioni 1.19.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwape hesabu rahisi kabisa, ingekuwa basi katika bajeti hizi mbili, tumepokea asilimia moja ya matoleo, kule 294 tungekuwa tumepokea shilingi bilioni 2.94. Kwenye hii shilingi trilioni 1.19 tungekuwa tumepokea matoleo ya asilimia moja tu, basi ingekuwa shilingi bilioni 11.9. Kwa hiyo, mwenye macho haambiwi tazama. Leo ninaomba nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuwa na jicho la maono la viongozi wa kufanya nao kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina-declare interest, mimi ni Makamu Mwenyekiti, na nimefanya kazi na Mawaziri wawili. Nimpongeze sana aliyempa kijiti Mheshimiwa Chongolo, Mheshimiwa Hussein Mohamed Bashe. Yeye wakati anapewa jukumu hili akisaidiwa na Mheshimiwa Mavunde waliweka document ya kuweza kupeleka kilimo kuchangia 10% itakapofika 2030. Pia ninampongeza zaidi Mheshimiwa Chongolo, huyu ni kiongozi na ni kiongozi mahiri kweli kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mawaziri wengi hawana continuity wakiingia kwenye Wizara, wanaanzisha mambo mapya. Alikuja kwenye Kamati kutueleza mipango yake, anaanza pale wenzake walipoishia. Uzuri anayo majembe; Mheshimiwa Naibu Waziri Silinde msikivu, anafuata yale maelekezo anapopewa, nawatakia kila la heri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kwa watendaji, yupo kiongozi wao Katibu Mkuu Dkt. Mweli. Haki ya Mungu huyu jamaa hana maneno mengi kama watu wafupi. Yeye ni vitendo na utendaji. Kwa hiyo, nina uhakika Wakurugenzi wote wa taasisi ambazo ziko chini ya Wizara ya Kilimo kazi, wanaifanya na tunaiona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kipimo ni kipi? Kwenye bajeti kuna kutengewa bajeti, kuna fedha, lakini sisi kama Bunge, kazi yetu pia ni kusimamia zile fedha zinazoenda kuhakikisha zinafanyiwa kazi? Niwapongeze Wizara ya Kilimo, fedha ni ndogo lakini kazi ni kubwa. Leo hii unasema huna kipimo cha kuipima Wizara ya Kilimo, lakini Mtanzania maskini wa kawaida kule kwangu Kingale anapokea mbegu ya alizeti ya ruzuku, leo anapokea mbolea ya ruzuku kutoka kwa Serikali yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kipindi hiki cha miaka mitano ya utekelezaji wa bajeti na ongezeko hili pamoja na fedha zinazotoka, mazao ya chakula yamepanda kutoka shilingi 17,000,000 tani, ni mpaka milioni 23,000,000 ongezeko la zaidi ya 38%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mama yangu Mheshimiwa Kilango ametoka kuliongelea utoshelevu wa chakula, tulikuwa tuna utoshelevu 126% leo tuna utoshelevu wa 130%. Utasema huna? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tumefika Tanzania Afrika Mashariki ndiyo nchi ya kwanza kumiliki ndege yetu ambayo inaenda kuua kwelea kwelea. Utasema huna cha kuwapima? Leo Mheshimiwa Rais watangulizi wake wawili waliacha eneo la umwagiliaji la ekari 600, yeye leo kwa bajeti hii ambayo bado tunamwombea Raymond apande fungu maalum hela ziendelee kwenda kwenye miradi ya umwagiliaji, amefikisha ekari 983,466 ndani ya miaka yake tu hii mitano ya utekelezaji wa bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti unafanyika. Leo tunaona TARI ilikuwa imekufa; leo tuna center of excellence kwenye utafiti ndani ya nchi yetu, utasema huna cha cha kuwapima Wizara ya Kilimo? Mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayaona, tutaendelea kuyaona. Rai yangu kwa Wizara ya Fedha, kweli ni sisi wanasiasa ndio tunatoa presha, tunataka vituo vya afya, hebu sasa hivi tupeleke kwenye sekta ya uzalishaji kilimo, itatuletea fedha za kujenga hospitali, na kujenga shule. Kwa hiyo, ninaiomba sana Wizara ya Fedha, kilimo kimeonyesha uaminifu na uadilifu, tuwapelekee fedha ili waweze kutuzalishia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la usimamizi, ninaunga mkono, na hii ilikuwa ni maoni kutoka kwa Kamati. Mheshimiwa Rais alitoa vifaa vya ugani, alitoa pikipiki na vipima udongo. Ufanisi wake ukawa mdogo kwa sababu vifaa vile vinasimamiwa chini ya Mkurugenzi. Mkurugenzi pikipiki ile anataka ipeleke mitihani, isiende kwa mkulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba Waheshimiwa Wabunge wenzangu tuunge mkono kwenye kwenda kuanzisha National Agricultural Extension Services Agency ili kule mashambani kwetu wakulima wafikiwe na wagani. Hili ni jambo muhimu katika usimamizi na ufanisi ili wakulima wetu waweze kupata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona leo watu wanasema BBT hamna chochote, vijana waliomaliza SUA leo wako, Mheshimiwa Njalu shahidi, mimi nimeenda kwa watani zangu Wasukuma kule Simiyu wanasifia wanawaita ma-BBT, wasomi wale kweli wamekwenda kuweka mchango katika kuongeza tija kwenye zao la pamba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, ninaomba nimshauri mambo mawili Mheshimiwa Waziri. Kwanza, ninamwomba, inawezekana wataalamu wake wa Wizarani wanafanya mambo mazuri, sisi tunahangaika hiyo sehemu ya BBT kuna vijana ambao wamesomea marketing na wengine wamesomea mambo ya kompyuta, watafutiwe ofisi wapewe vifaa, kazi yao ni kutafuta masoko nje ya nchi na walipwe kutokana na kamisheni kwa masoko watakayoyaleta. Mtakuja kunishukuru baadaye. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana watu wanapenda kupeleka besenga, nini, vijana wapo. Ninaomba niwasemee, wape vyumba wape kompyuta, wape vifaa na hutawalipa mshahara, utawalipa kwa performance kwa namna wanavyokuletea. Sasa hii ni bajeti. Bajeti ni mapato na matumizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ya mwisho, ninaomba nishauri na ninajua wako watakaofurahia kimoyomoyo, wako watakaonibeza, lakini ni maoni. Liko zao ambalo mimi nataka nishauri kuliko kubanana banana, hebu tuangalie chanzo hiki kipya cha mapato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona na ninampongeza sana kaka yangu Aretas James Lyimo, kwa kazi kubwa anayoifanya katika kupambana na madawa kulevya, lakini niliona kuna boti Bagamoyo imebeba jani linaitwa shajaratul fikra. Kuna wenzangu Mombasa kule wanaitwa shajarat al-fikra, wengine wanaita khat wengine wanaita miraa, wengine wanaita mirungi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikaenda kufanya tafiti kama yale amekamata gizani, yaliyokamatwa ni mangapi? Ina maana tunamfaidisha jirani bila sisi kujua, ana soko kubwa, na anapata hela kupitia sisi. Nikaenda kujifunza zao hili la kati, na leo ninashukuru wageni wa Kisomali walikuwepo ndiyo soko kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Somalia inakusanya mapato zaidi ya milioni nane kwa mwaka kutokana na biashara ya mirungi. Kenya inaingiza dola milioni 300 tena kwa zile nchi ambazo ziko wazi; Tanzania hatuhesabiki kwa sababu sisi tunaletewa gizani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, dunia nzima mzunguko wa zaidi ya dola bilioni tatu kwenye zao hili la mirungi na huko nyuma nimeulizia ulizia Tanzania ilikuwa inaruhusiwa, sasa mimi sina ushahidi na kinga ya Bunge inilinde. Ninasikia kuna kiongozi fulani alikuwa na rafiki anatumia, sasa lile starehe nilivyofuatilia la wastaarabu hawapendi bughudha hawezi kusikia mtu amekula mirungi kapigana…
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mariam Malizia muda wako umeisha.
MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimalize.
MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, vitu vya msingi vinaongea vya kushauri…
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ile biashara huwezi kusikia mtu kamrushia chupa anayekula mirungi kwa ustaarabu. Sasa yule rafiki yake akawa anamchelewesha muda wa kuonana naye, kwa hiyo, tunaomba Hansard zituonyeshe. Siyo dhambi, tujue lile Bunge lililotunga sheria, walitumia vigezo vipi? Leo ukiangalia madhara, inasema mirungi inasababisha kansa. Twendeni Ocean Road…
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa muhimu sana.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mariamu muda wako umemalizika.
MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya sigara ambayo inatokana na zao la tumbaku, na mirungi wapi wagonjwa wengi wanaosababishiwa kansa? Twendeni tukajifunze. Wanasema mirungi inasababisha social dependence. Tuulize, zile pombe kali zinazozalishwa huko Babati Sungura na kadhalika, zipi ambazo zinaharibu vijana wetu? Ni mirungi ama hizo pombe?
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mariam umeeleweka, lakini hilo liko nje ya uwezo wa Mheshimiwa Waziri, inabidi irudi kwenye sheria. Kwa hiyo, umeeleweka.
MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimalizie. Sheria zinaletwa kwa Miswada, nadhani Serikali, nami sio Mwanasheria, ndio maana tunashauri na yeye anao watafiti, ninadhani ana vyombo vingi ambavyo wanaweza kwenda kufuatilia. Kwa hiyo, twende tukajiridhishe kwamba kweli madhara ama hizo element za ulevi ndani ya mirungi na kwa vitu vingi leo wanasema mirungi inaleta madhara kiafya…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mariam muda umepita sana.
MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaulize, energy drink na mirungi ipi ambayo inaleta madhara zaidi kiafya. Muda umefika tutafakari, kwa sababu zao hili linaleta mapato mengi na pia nimefuatilia Kenya inapeleka Djibouti, Kenya inapeleka mirungi Somalia, mpaka Israeli Yerusalamu...
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Mariam, hiyo ni kazi ya Serikali, umeeleweka.
MHE. MARIAM D. MZUZURI: …mirungi inapelekwa kama zao la biashara katika nchi hiyo.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mariam.
MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninapenda kumalizia kwa kumpa sifa sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa, lakini Comrade Chongolo. Ama hakika Mheshimiwa Rais hajakosea kumleta Wizara ya Kilimo kwanza ni muumini wa kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakumbuka hata uanzishwaji wa Benki ya Ushirika, moja ya mafanikio makubwa ndani ya Wizara ya Kilimo yeye ndio mwanahisa wa kwanza kununua hisa kati ya benki hiyo.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mariam unawanyima fursa wengine.
MHE. MARIAM D. MZUZURI: …alikuwa Katibu Mkuu ambapo anaenda kufanya ziara ya kichama, lakini anakagua miradi ya kilimo. Kwa hiyo, mzigo amepewa mtu sahihi. Kama Kamati…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)