Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Korogwe Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CHARLES M. NJAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Nami nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, na Naibu wake; Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo pamoja na Wakurugenzi wake wote kwa namna ambavyo wameleta wasilisho zuri katika bajeti yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze pia kwa kazi nzuri ambayo inaonekana kwa miradi mbalimbali ambayo wanaendelea kuitekeleza katika Wizara ya Kilimo. Wizara ya Kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa letu. Kwa kuzingatia hilo, tunaona fursa kubwa ambayo ipo kupitia kilimo katika nchi yetu hasa kutengeneza ajira nyingi zaidi wa vijana wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kufikia uongezaji wa ajira kwa vijana wetu wa Tanzania nafikiri tunapaswa tufanye mambo mawili makubwa. Jambo la kwanza ni vizuri tukawekeza zaidi katika utafiti kama vile ambavyo wenzetu upande wa madini wanafanya utafiti ili kuondoa uncertainties zilizopo katika wachimbaji, vivyo hivyo tunatakiwa tufanye utafiti wa kutosha katika mbegu, katika ardhi na aina ya mazao ambayo yanaweza kuwa katika maeneo tofauti tofauti ili kuondoa uncertainties kwa vijana wanaotamani kwenda kuingia katika kilimo zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo pia ni vizuri kuliwekeza kwa nguvu kubwa ni upande wa masoko wa mazao ambayo tunaenda kuzalisha tukiweka nguvu katika maeneo haya mawili, tutakuwa tumewashawishi wakulima na hasa vijana kuingia zaidi katika kilimo kwa kuwa watakuwa na uhakika mtaji wanaoupeleka katika eneo fulani la kilimo wana uhakika wa kuvuna na wana uhakika pia baada ya kuvuna wanalo eneo la kwenda kuuza mazao yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika upande wa masoko, Waheshimiwa waliochangia jana, baadhi nimesikia wakiongelea vizuri kazi nzuri iliyofanywa na COPRA. Ninafikiri ni wakati mwafaka sasa Mheshimiwa Waziri ukaona namna gani unaenda kuwekeza zaidi katika taasisi hii ili iweze kutafuta masoko zaidi na kuwahakikishia wakulima masoko ya bidhaa ambazo wanakwenda kuzizalisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo tunatakiwa tuliwekee nguvu na ninampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo ameshaifanya na Mkurugenzi wa Tume ya Umwagiliaji ambao wamefanya kazi kubwa mpaka sasa, lakini bado tunayo kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha kwamba tunaendeleza miradi ya umwagiliaji katika maeneo mengi ya nchi, kwa kuwa hili nalo ni eneo ambalo litakwenda kuleta uhakika kwa wakulima badala ya kuendelea kutegemea mvua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo letu la Korogwe Mjini tunamshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, tuna miradi miwili mikubwa ya umwagiliaji. Tunao mradi wa umwagiliaji katika Kata yetu ya Kwamdolwa, tunao pia mradi mkubwa wa umwagiliaji katika Kata yetu ya Kwamsisi. Miradi hii miwili kwa ujumla wake inagharimu takribani shilingi bilioni 29.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, ninamwomba Mheshimiwa Waziri, katika bajeti yake na hasa atakapokuja kufanya finalization, angalau atupe tumaini kwa sababu miradi hii imekuwa ikisuasua kwa muda mrefu sana. Tunahitaji twende tukaone utekelezaji wa miradi hii inatekelezwa kwa kuwa inaenda kuleta chakula kwa wananchi, lakini pia inaenda kutengeneza ajira nyingi kwa watu wa Korogwe Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine kwa upande hasa wa jimbo langu, sisi ni miongoni mwa wazalishaji wa zao la mkonge na wananchi katika Jimbo la Korogwe Mjini wameonyesha utayari wao kwa kuwa wengi wamejikita katika kilimo cha mkonge, lakini tunayo changamoto ya upungufu wa mashine za kuchakata mkonge, mashine za corona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, alivyopita katika wakati wa kampeni katika Jimbo la Korogwe Mjini na Korogwe kwa ujumla aliahidi kutuletea mashine hizi za uchakataji wa mkonge katika Jimbo la Korogwe Mjini na Korogwe Vijijini pia. Ninamwomba Mheshimiwa Waziri aone namna gani tunakwenda kupata sasa hizi mashine za corona katika eneo letu ili katani inayozalishwa isiende kuharibika kwa kukosa mashine za uchakataji wa mkonge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninafikiri tuna fursa katika eneo hilo. Tunazalisha mkonge kwa wingi, lakini tunasafirisha mkonge nje. Hata hivyo, tunayo fursa ya kuanzisha viwanda vya kutengeneza final products za mkonge ambazo pia zitakwenda kutusaidia kukabiliana na products ambazo zinaharibu mazingira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna wenzetu wanazalisha korosho, wanazalisha kahawa ambayo sisi tukiwekeza katika uzalishaji wa gunia tunaenda kuleta vifungashio ambavyo vitakuwa ni rafiki kwa mazingira, lakini pia tunaongeza ajira kwa maeneo ambayo tunazalisha mkonge hasa Korogwe na eneo lote la Mkoa wa Tanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Korogwe Mjini tuna vikundi vingi ambavyo vimejikita katika uzalishaji wa mboga mboga, lakini changamoto tunayokutana nayo ni kwamba wakati mwingine akina mama wale na vijana wanapopeleka mbogamboga sokoni, zinakosa wateja kwa wakati huo. Ombi lao kubwa la namna ya kuboresha biashara yao na kilimo chao cha mbogamboga ni kupata cold room ambayo angalau hata kama watakwenda sokoni na watakosa wateja, basi mboga zile zisirudi kuharibika na badala yake ziwe zimetunzwa na kuwe na uhakika wa kuuzwa wakati mwingine unaofuata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunamsihi sana Mheshimiwa Waziri aangalie katika bajeti yake namna gani tunaweza tukapata cold room kwa ajili ya storage ya mbogamboga na matunda yanayozalishwa katika Jimbo letu la Korogwe mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kupatiwa kiwanda cha kuchakata haya mazao ambayo ni perishable kama namna ya mojawapo ya kwenda kufanya storage na hasa nyanya ambazo zinazalishwa na wakulima hawa wadogo wadogo katika eneo letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie katika zao la machungwa. Sisi Tanga tunaamini hakuna eneo linalozalisha machungwa bora zaidi ya Mkoa wa Tanga. Sasa tunaomba kupatiwa kiwanda cha kutengeneza juisi za matunda. Korogwe ilikuwa na Kiwanda cha Tang Gold ambacho baadaye kilipewa mtu binafsi ambaye ameshindwa kukiendesha. Hata hivyo, Mheshimiwa Rais alivyopita katika Jimbo la Korogwe Mjini wakati wa kampeni alisema kiwanda kile kitarudishwa kwa wananchi na kiendelee kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba tuone namna gani sasa tunaweza tukaanza ku-process matunda yetu ndani ya eneo la Korogwe badala ya kusafirisha machungwa kwenda nchi jirani halafu baadaye tuletewe tununue kwa bei kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)