Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Edward Olelekaita Kisau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kiteto

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi. Ninampongeza Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu na timu nzima ya Wizara ya Kilimo kwa kazi kubwa ambayo wanafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na Waheshimiwa Wabunge waliotangulia kuwapongeza wakulima wote nchi nzima. Wakulima wanafanya kazi kubwa, ukisikia Taifa lina chakula cha kutosheleza, kazi hii inafanywa na wakulima wa Tanzania nzima hii. Kwa hiyo, tunawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo ni maisha, ni zaidi ya biashara, ni zaidi ya uti wa mgongo, ni zaidi ya mgongo wenyewe, ni maisha. Sifa ya kilimo, sifa nyingi sana zimeshatajwa kwamba Watanzania 65% mpaka 75% wanategemea kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami ninadhani hata hizi data, unajua kutokutegemea kilimo maana yake kuna mtu hali kabisa. Kwa hiyo, ni more than 75%. Kama hulimi, si unauza; kama huuzi, si unakula; sasa si unategemea kilimo. Kwa hiyo, kwa kweli tumpongeze Mheshimiwa Dkt. Samia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama walivyosema wengine, bajeti ya kilimo kuongezeka mara tatu, mara nne kwa kipindi cha miaka mitano ni kazi kubwa sana. Kazi nyingine kubwa aliyofanya ni kumchagua Katibu Mkuu Mstaafu wa Chama cha Mapinduzi, rafiki yangu Mheshimiwa Chongolo. Yeye ni zaidi ya Waziri. Sio Waziri tu, ni Waziri halafu ni Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake nini? Yeye anajua nchi hii yote, ameizunguka. Anajua kila mahali, kila kona ya nchi hii. Kwa sababu Chama cha Mapinduzi kinatunza misingi, sisi kazi yetu ni kuisimamia misingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tungependa kwa kweli wakulima kama unavyosikia kwa Wabunge hawa, kila Mbunge amependa kuchangia kilimo kwa sababu kinawagusa Watanzania wote na misingi ya kilimo ni kuzungumza na wananchi wenyewe na kusikiliiza Watanzania wanasema nini kuhusu kilimo. Huo ni msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, msingi mwingine ni Serikali kuendelea kuwekeza na kuweka mazingira mazuri kwa wakulima nchi hii. Tuwe na sheria nzuri, tuwe na masoko mazuri, tuwe na mbegu bora, nzuri na mbolea na zifike kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa ninasoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri hapa ukurasa wa 148 ninanukuu sehemu ndogo tu: “Nawasihi wakulima wa nchi hii kuwa macho na kuhakikisha wananunua mbegu bora kutoka kwa mawakala waliosajiliwa na kukagua kwa makini nembo za udhibiti ubora na kwenye vifungashio na siyo vinginevyo.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi mkulima leo wa kule Emarti kule Kiteto ama Makame ama Longido huko, yuko kijijini kabisa kule atajuaje kwamba kuna nembo, kuna kifungashio? Unajua Wizara ya Kilimo lazima tuongee lugha ambayo Watanzania wa kawaida wanafahamu. Kuna Watanzania wengine wanakutana na hizi mbegu, imenunuliwa na mtu mwingine, kaileta kijijini. Kwanza atajuaje kwamba huyu kasajaliwa; na nani? Ataona wapi? Kwa hiyo, ninadhani Wizara ya Kilimo iongee lugha ya wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Wizara ifanyeni hiyo kazi ya kupambana na wale wanaoleta mbegu. Tusilete jukumu hili kwa wakulima, ni kazi ya Serikali. Tutasaidiana ndiyo, lakini isifanywe kwamba sisi ndio tukague, halafu tukishindwa tuseme sijui nini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwaambia wakulima wangu, kesho ninachangia, yaani leo sasa; nikawaomba mawazo yao. Kwa kuwa Wizara ya Kilimo ni kuangalia misingi, wasikilize wakulima wa Kiteto wanasema nini, tunaomba magari yale ya Mama Samia Suluhu tukachimbe maji mashambani. Maeneo tunayo, tupate kilimo cha uhakika, ndicho wanachosema wakulima. Mwingine anamwambia mwenzake, anasema Waziri yuko sahihi sana, kilimo cha mara moja kwa mwaka cha kutegemea mvua ni mtihani. Ndicho wanachosema wakulima wale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwingine anasema tupatiwe mbegu bora, lakini changamoto kubwa ni bei. Tunomba Serikali iendelee kupambana, iendelee kufikiria mbegu hizi ni ghali, ishuke ili wakulima wapate motisha ya kwenda mashambani. Vilevile, wanaomba na wanasema masoko yawepo na waunganishwe na masoko ya nje. Huyu ni mkulima mdogo sana wa Kiteto. Ndicho wanachosema. Kwa hiyo, tunataka Serikali iweke mazingira mazuri kwa ajili ya wakulima hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa ninaangalia mazao ya chakula tunayaagiza kutoka nje ngano na maziwa. Nimekutana na maziwa sasa nikawa ninawaza, sasa hata maziwa yako kwako huku, sasa rafiki yako wa mifugo utakuwa umemwachia nini? Nyama tu. Anyway, lakini kama tunaagiza maziwa, ngano na mafuta ya alizeti, na tuna ardhi ya kutosha, kweli itatuchukua miaka mingi sana kwenda mwezini which is fine. Angalau huku chini basi na sisi tuwe giants kwenye maeneo haya, na tumepata experience wakati wa UVIKO. Mipaka ilipofungwa hakuna mafuta ya kula. Sasa kwa sababu hatuna namna ya ku-control majanga haya yanayotokea huko duniani, ni afadhali tuwekeze kwenye kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli kama alivyosema Mheshimiwa Prof. Muhongo, commitment tuliyofanya ya Malabo ya…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)