Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya na kunipa kibali cha kuweza kusimama ndani ya Bunge lako Tukufu na kuweza kuchangia bajeti ya Wizara ya Kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa miradi mikubwa ya umwagiliaji ambayo imewekezwa katika nchi hii. Nitumie fursa hii kufikisha salamu za wananchi wangu wa Jimbo la Itwangi hususan katika Kijiji cha Nyida ambako kuna mradi mkubwa wa shilingi bilioni 14.6 unaoendelea kutekelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitumie fursa hii kumpongeza Waziri, Naibu Waziri na wataalamu wao wote. Mipango ni mizuri, ninachoomba, Wizara ya Fedha watoe fedha na kuwapatia Wizara ya Kilimo ili waweze kukamilisha mipango mizuri waliyonayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajikita katika kilimo cha umwagiliaji. Mradi wa umwagiliaji uliopo katika Kijiji cha Nyida unatakiwa kukabidhiwa tarehe 24 mwezi wa Tano, lakini kuna vitu vingi bado havijakamilika, na kwa sababu ya muda, ninaomba nisivitaje. Kwa kuwa nimeshamwambia Mheshimiwa Waziri mambo mengi hayajakamilika katika Mradi wa Nyida, lakini kwenye hotuba yao wameandika mradi umekamilika kwa 100%. Ninaomba Waziri atakapokuja hapa anipe majibu, ni kwa nini wamesema mradi umekamilika wakati kuna vitu vingi ambavyo havijakamilika ndani ya Mradi wa Nyida? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitumie fursa hii pia kuiomba Wizara ya Kilimo miradi ya umwagiliaji. Katika Jimbo la Itwangi kuna mradi wa umwagiliaji wa Kijiji cha Ishololo. Mradi huu umetekelezwa miaka saba nyuma, lakini haukukamilika, umebakiza kipande kidogo sana mradi huu kwenda kukamilika. Serikali imewekeza fedha nyingi pale, lakini kwa sababu mradi haukukamilika, maji yanaingia na kutoka na fedha ile iliyowekezwa pale na Serikali inakuwa haina maana yoyote kwa sababu maji hayakai. Hivyo, nitamwomba Waziri atakaposimama anipe majibu ya kwenda kukamilisha mradi huu wa Bwawa la Ishololo uliopo katika Jimbo la Itwangi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Itwangi nimesema ninajikita katika umwagiliaji kwa sababu kwa Mkoa wa Shinyanga ndiyo jimbo tunalolima mpunga. Ukisikia mchele wa Shinyanga 80% unatoka Jimbo la Itwangi. Wananchi wa Jimbo la Itwangi kilimo wanachotegemea ni cha maji ya mvua. Tunashukuru na kuipongeza Serikali kwa miradi hii mikubwa ya umwagiliaji. Katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2025 kuna miradi ambayo imetajwa itakwenda kutekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Wizara katika Mradi wa Butini kwenye Ilani ya Uchaguzi, kunatakiwa kwenda kujengwa mifereji 25 ya kusambaza maji kwenye mashamba ya mpunga. Katika Kijiji cha Nsalala, kwenye ilani inasema mitaro ya maji ya kupeleka kwenye mashamba yetu inatakiwa ijengwe mifereji 30.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, katika Jimbo la Itwangi mradi wa umwagiliaji wa Kijiji cha Masengwa umekuwa ni historia. Kila siku yamekuwa ni maneno, unawekwa kwenye bajeti hautekelezwi, lakini katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi mradi huu pia umewekwa kwa kutekelezwa kujengewa mifereji 35 iliyopo ndani ya mradi huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini sana utendaji wa Mheshimiwa Waziri, kwa kazi anajulikana yeye na Naibu wake na watendaji wake. Ninawaomba na kuwasihi sana katika miradi hii ambayo imetajwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi twende tukaitekeleze ili wananchi wa Jimbo la Itwangi kwa sababu ndio zao kubwa wanalolitegemea kwa biashara na chakula, tuwatendee haki kuhakikisha kwamba miradi hii inakwenda kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hii imekuwa ni ya muda mrefu, na imekuwa ikitengewa fedha lakini haikamilishwi. Ninaomba sana, ninaisihi sana Serikali iweze kutoa fedha zinazopitishwa na Bunge kwa ajili ya miradi ya kilimo ambayo imewekezwa ndani ya vijiji vyetu na ndani ya majimbo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hii ya umwagiliaji ikienda kukamilika, hakika tunakwenda kunufaika kwa kiasi kikubwa. Tunaongelea mazao mengine, lakini sioni mtu anaongelea zao la mpunga kwa maana ya mchele. Tunaujua wali ukiwa kwenye Sahani, lakini shughuli yake iliyoko kule ni kubwa, na wananchi wanahangaika kwa kusubiri mvua. Mvua zinapokatika, uhakika wa kuvuna zao hili unakuwa ni wa mashaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaisihi sana Serikali katika miradi yote iliyowekwa ya umwagiliaji, tuhakikishe kwamba inakwenda kukamilika na kulipandisha thamani zao hili la mpunga ambalo kwa kiasi kikubwa ni zao la biashara na ni zao la chakula. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)