Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busokelo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. LUTENGANO G. MWALWIBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara yetu hii Wizara muhimu ya Kilimo. Pia, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, ndugu yangu Chongolo pamoja na Naibu Waziri na viongozi wote kwa maana ya watendaji katika Wizara hii ya kilimo kwa hotuba nzuri ambayo wametuletea hapa iliyojaa matumaini na dhamira njema ya Mheshimiwa Rais jinsi ya kuweza kutatua changamoto na kuwasaidia wakulima katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuchangia hilo, pia ninapenda kumpongeza Mheshimiwa Rais jinsi ambavyo ameonesha dhamira ya dhati ya kuweza kuleta mabadiliko kwa nia anayoonesha. Bajeti hii ilikuwa shilingi bilioni mbili miaka minne iliyopita, lakini leo ameipeleka mpaka kufikia kiwango cha karibu shilingi trilioni 1.9. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichangie mambo machache, mambo mengi mazuri yanafanywa na Wizara hii kama nilivyoeleza utendaji wa Mheshimiwa Waziri haujawahi kutiliwa shaka kutoka akiwa Mtendaji Mkuu wa chama chetu, lakini pia Naibu Waziri tunamfahamu pamoja na watendaji wengine wote wakiongozwa na ndugu yangu Gerald Mweli ambaye rekodi yake haina mashaka yoyote. Tunaomba tutoe mchango mchache kwenye maeneo machache ambayo tunaomba yaboreshwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wananchi wa Jimbo la Busokelo tunao mtanzuko katika eneo la chai. Chai imeongelewa na Wabunge wengi. Wawekezaji wa chai TATEPA kule wamegoma kununua chai ya wakulima na mpaka hivi ninavyoongea wakulima hawana sehemu ya kuweza kuiuza chai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vilifungwa kutoka mwaka 2024, Kiwanda cha Mwakaleli mwaka 2024 na mwaka 2025 Kiwanda cha Tukuyu. Hali hiyo imezorotesha sana maendeleo katika eneo la Busokelo. Sasa nimeongea na Mheshimiwa Waziri mara kadhaa na ameonesha dhamira jinsi anavyokwenda kushughulikia jambo hili akishirikiana na wataalamu wengine. Ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja kufanya majumuisho hapa atueleze ni jinsi gani anakwenda kutusaidia, kwa sababu mgogoro uliopo, wananchi wanatakiwa kuuza chai kwa shilingi 256 ambapo mwekezaji anataka na bei elekezi ya Serikali ni 366.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wananchi wanataka kujua, ni nini msimamo wa Serikali kwa mwekezaji huyu ambaye kimsingi ana mambo mengi anayoyafanya, yanaonesha kabisa kwamba ameshindwa kusimamia yale ambayo yalimfanya awe mwekezaji katika eneo lile? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba mwekezaji huyu Mheshimiwa Waziri afanye maamuzi magumu kama alivyochangia jana Mheshimiwa Mwanyika kwamba ikiwezekana aondolewe kwa sababu pamoja na mambo mengine, wenzetu wamempa mkopo mwingine wa shilingi bilioni sita, bado hanunui chai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu mkopo, wananchi ambao wana 30% wataendelea kudaiwa katika deni hili. Jambo hilo hatutaweza kulikubali kwa sababu ni sehemu ya dhuluma. Tunayo imani kubwa na Wizara hii, tunayo imani kubwa na Mheshimiwa Rais ambaye ametoa maelekezo kwamba wawekezaji wa namna hiyo wasipewe nafasi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nilikuwa ninataka niongee kwa uchache kwa upande wa maparachichi pia. Mheshimiwa Waziri ninaomba nimshukuru sana Mkurugenzi wa Bodi ya Chai, tumeshirikiana kwa kiwango kikubwa kupambana katika kutatua jambo hilo. Baadhi ya mambo ninajua alitamani yangefanyika, lakini Wizara inayo nafasi ya kuweza kusaidia kuona namna gani tunaweza tukavuka kwa pamoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vivyo hivyo, nilikuwa ninaomba kwa upande wa parachichi. Ziko parachichi ambazo wanasema ni za daraja ya kwanza na daraja la pili. Wanapokwenda kununua unakuta wanaziangua hizi na wanamwambia mkulima kwamba parachichi zako ni za daraja la pili. Sasa hapo inakuwa ni changamoto sana kwa wakulima wetu. Tunaomba wenzetu wa COPRA pamoja na kazi nzuri wanayofanya, waweze kuwatumia wagani waliopo maeneo yale waweze kuwasaidia wakulima wetu ili kuondoa dhuluma hiyo na kuweza kujua. Tusingependa kuwa na maparachichi ya daraja la pili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuchangia katika eneo la mbolea. Tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuweza kuhakikisha kwamba anatoa mbolea ya ruzuku na wenzetu wa TFRA hapa wanafanya kazi nzuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Ndugu yangu Joel, amekuwa anafanya kazi nzuri ya udhibiti, pamoja na wenzake, wanasimamia vizuri na kuhakikisha kwamba, hatuna changamoto zile za mwanzo za mbolea tulizokuwa tunapata, ambazo zilikuwa hazikidhi ubora. Katika kufanya jambo hilo, tumeona mikakati mizuri ambayo wamesema katika kutuletea mbolea, lakini pamoja na hivyo, ninataka niishauri Serikali, isikubaliane na wazo la kuuza Kampuni yetu ya Mbolea Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali lazima ijue kuna maeneo ambayo kampuni nyingine hizi tunataka pia nazo ziboreshewe mazingira, haziwezi kupeleka mbolea. Ndiyo maana Serikali ni lazima iwe na mashirika kama hayo, kama ilivyo kwenye mafuta na maeneo mengine, ili yale maeneo ambayo wafanyabiashara wataona hakuna faida, basi wenzetu wa TFC wanaweza wakaifanya kazi hiyo nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa pia, ninampongeza Mkurugenzi, Ndugu Msote, na wenzake, wanafanya kazi nzuri. Tuwaongezee nguvu tuweze kuhakikisha kwamba, wenzetu hawa wanafanya kazi iliyokusudiwa. Ninawashawishi Wabunge, kama Mheshimiwa Rais amesema anakusudia kuacha tabasamu kwa Watanzania, moja kati ya sekta na eneo ambalo tunaweza tukapata matokeo ya kuwa na mguso wa moja kwa moja kwa wananchi ni katika Wizara ya Kilimo. Ninaomba Serikali tuhakikishe kwamba, tutakapoipitisha bajeti hii, fedha inakwenda kama jinsi ambavyo imepangwa.