Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Patrick Adkin Mwalunenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbeya Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. PATRICK A. MWALUNENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na mimi kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia hoja iliyoko Mezani, ya Wizara ya Kilimo. Kwanza ninampongeza Mheshimiwa Rais kwa uthubutu wake, toka alipoingia madarakani ameonyesha dhamira ya dhati kwamba, anataka kupandisha kilimo chetu na kutengeneza ajira kwa vijana wetu ambao wamekosa ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, amefanya mambo mengi; la kwanza ni kuasisi mfumo wa mbolea, kwa maana ya ruzuku ya mbolea. Sisi sote ni mashahidi, alipoingia madarakani mbolea ilikuwa inauzwa zaidi ya shilingi 140,000 mpaka shilingi 160,000. Wakati mwingine ilikuwa haipatikani hata kwa pesa hizo, lakini Mheshimiwa Rais alihakikisha kwamba, mbolea inapatikana muda wote kwa bei ya chini ya shilingi 70,000. Hiyo ni hatua kubwa ya maendeleo kwa wakulima wetu wa Tanzania, wanatakiwa wajue.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitendo cha mbolea kuuzwa chini ya shilingi 70,000, maana yake ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya Mama yetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, inalipa gharama ya fedha hiyo na hii imeleta matokeo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba, pamoja na changamoto zote za bei ya mafuta na gharama nyingine zote, bado mfumuko wa bei ya chakula uko chini. Maana yake ni kwamba, Wizara ya Kilimo inabeba gharama nyingi, inatoa ruzuku ya mbolea, inatoa mbegu, miche, na kadhalika. Ndiyo maana unakuta sasa gharama za uzalishaji kwa mkulima zimekuwa siyo kubwa sana na mfumuko wa bei kutokuwa mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Waziri wa Kilimo, ndugu yangu, Mheshimiwa Chongolo na Naibu wake, sina mashaka naye. Tumeisikiliza bajeti, ni nzuri na inaonesha mwelekeo kwamba, vijana wetu wanapata matumaini. Waliomaliza vyuo vikuu sasa wanaweza wakaenda kuwekeza kwenye kilimo kwa sababu, mazingira ni mazuri. Umesema kwamba, ardhi itaenda kupimwa ili kujua inahitaji mbolea ya aina gani kwenye eneo husika, uwekezaji kwenye mabwawa, kwa maana ya skimu za umwagiliaji na ujengaji wa maghala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo yote ni value chain ambayo inaonesha kabisa kwamba, sasa kijana wetu wa Kitanzania ambaye ni msomi, akiamua kwenda kuwekeza au kufanya shughuli za kilimo, atafanya kwa tija, kwani ana uhakika wa kulima, ana uhakika wa kuvuna na ana uhakika wa kuhifadhi yale mazao ambayo yanaweza yakapotea wakati ule wa kuhifadhi baada ya mavuno. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninaipongeza Wizara ni kwamba, wamesema wataendelea kuboresha huduma za ugani, maana katika jambo kubwa ambalo wakulima wetu wanahangaikia, ni shughuli za ugani. Mmea umefika juu, unaanza kushambuliwa na wadudu, unakuta hana taarifa ni kitu gani kimemsibu. Mwisho wa siku inamsababishia hasara kubwa sana mkulima. Kwa hiyo, ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri na timu yake, waendelee hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ninawapongeza COPRA, wanafanya kazi kubwa kwa sababu, haya mazao mengi ambayo hayakuwa na bodi, baada ya kuundwa COPRA, tumeona mabadiliko makubwa kwenye mazao kama ya parachichi, ufuta na mengine yanayofanana na hayo, lakini bado COPRA waongezee nguvu, ili waweze kusajili wakulima wao wenyewe. Waweze kuyaangalia yale mazao yakiwa shambani kwa sababu, imekuwa ni changamoto, mazao mengi yanayokwenda kuuzwa nje ya nchi, yanakuwa na changamoto kwenye suala la ubora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, COPRA wawekewe nguvu waweze ku-control mazao kuanzia shambani mpaka yanakokwenda kuuzwa, ili kuhakikisha kwamba, yanapata bei nzuri na soko la uhakika. Imekuwa ni mara nyingi mkulima amevuna mazao yake, anakwenda kuyapima, anaambiwa mazao haya hayana ubora, anarudishwanayo. Kwa hiyo, ni lazima COPRA iwe ni jicho la kuangalia yale mazao kuanzia kule shambani mpaka yanapokwenda kwa mlaji wa mwisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, ni lazima Wizara ya Kilimo iwe na mahusiano na Wizara nyingine. Wizara ya Kilimo ndiyo Wizara mama, lakini ni lazima iwe na mahusiano ya karibu na Wizara ya Viwanda na Biashara kwa maana ya TAMISEMI, Wizara ya Ardhi, Wizara ya Fedha na ikiwezekana kuwe na kamisheni moja, kiundwe chombo ambacho wanawasiliana kwa karibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, leo hii tukimwambia Waziri atupe takwimu ni viwanda vingapi ambavyo vinazalisha juisi ya matunda? Vimetumia matunda kiasi gani ya kwetu versus yale ma-carbonates yanayoagizwa toka nje, kemikali kwa ajili ya kuzalisha juisi ya matunda?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaona vitu hivyo haviashabihiani. Tunataka watu wetu wanufaike kupitia biashara ya uzalishaji wa matunda. Sasa unakuta takwimu zinakuwa hazipo, mwisho wa siku matunda ya wakulima wetu yanaoza na wakati huo kuna viwanda vinazalisha matunda ya juisi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)