Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busega
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nachangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Kilimo. Nataka nizungumze eneo la zao la pamba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri, amezungumza mambo mengi katika zao letu la pamba ambalo takribani 51% mpaka 60% linazalishwa katika Mkoa wa Simiyu. Nimeona katika mpango uliokuwepo wa mwaka wa fedha 2025/2026 ilikuwa ni kuzalisha takribani tani 400,000 za pamba, lakini zilizozalishwa katika mwaka wa fedha 2025/2026 mpaka kufikia Machi, ilikuwa ni tani 222,014 ambayo ni sawa na 55%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaona bado tuna safari ndefu katika uzalishaji wa zao la pamba. Nina mambo mawili ambayo ninataka nichangie hapa. Mheshimiwa Waziri amesema, katika mpango wa uzalishaji wa zao la pamba watajikita katika uzalishaji wenye tija. Ninakubaliana naye, kwani uzalishaji wenye tija ndiyo uzalishaji unaotakiwa sasa hivi, lakini kuna mambo mawili ambayo tunatakiwa kuyaangalia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ni utafiti wa mbegu. Nina wasiwasi na mbegu tunayoitumia sasa hivi, inawezekana imepitwa na wakati ndiyo maana tunahitaji pembejeo na dawa nyingi katika kutibu magonjwa ambayo yanaathiri zao letu la pamba. Ukitumia pembejeo nyingi katika kutibu zao la pamba maana yake ni kwamba tutatumia fedha nyingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona hapa kwenye Taarifa ya Mheshimiwa Waziri, ametumia takribani shilingi bilioni 61 kuhudumia pembejeo katika zao la pamba, na hii ni kwa sababu ya mbegu kutokuhimili. Wadudu ni wengi. Wadudu wakiwa wengi, maana yake ni kwamba tunatumia dawa nyingi na uzalishaji wake unakuwa hafifu kwa sababu, pamba inakuwa ya njano. Sasa nini kifanyike hapa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tujikite katika utafiti wa mbegu zitakazozalishwa ili kuhakikisha kwamba, zao la pamba tunalilima na tunapata, ndipo tutakapoenda kwenye uzalishaji wenye tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni BBT kwa vijana wetu. Ninakubaliana kabisa na Programu ya BBT kwa vijana, na ni jambo ambalo linaenda kuimarisha katika uzalishaji wenye tija. Ninakubaliana na hilo. Hapa nini kifanyike?
Mheshimiwa Mwenyekiti, chukulia mfano, Mkoa wa Simiyu una kata 133, fanya assumption katika kata 133 kata ambazo zinazalisha pamba tufanye ni kata 120. Tumpe kijana mmoja kusimamia shughuli za ugani kwenye kata moja. Tunahitaji vijana ambao watashughulika na BBT, vijana 120. Tukienda na vijana 120, tukawalipa shilingi 600,000 kwa mwezi, tutatumia takribani shilingi bilioni 864 kwa mwaka kwa vijana wote 120. Nini tunataka kupata hapa? Nina imani tija inaenda kupatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uzalishaji wa pamba kwa ekari sasa hivi unaenda kilo 200 mpaka kilo 300. Chukulia kilo 200 bei iwe kubwa, fanya shilingi 2,000. Mkulima atapata kwa ekari shilingi 400,000 lakini tukiwa na tija iliyo nzuri ya kuzalisha kilo 500 kwa ekari moja, mkulima atapata shilingi 1,000,000. Ndiyo maana ya kuwa na tija kwenye uzalishaji wa zao la pamba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali tukiwaajiri sisi wenyewe bila kuwabugudhi, hawa wawekezaji ambao sasa hivi wameenda kwenye kilimo cha mkataba, ambapo mwisho wa muda watataka mkulima auze pamba yake kwa huyu mwekezaji, tukihama huko, Serikali iwaajiri hawa BBT, vijana waende kufanya kazi na wao wawe na logbook ya kuwatembelea wakulima. Mimi nitawaambia wakulima wa Jimbo la Busega, kila mkulima awe na logbook, akifika shambani huyu mtu wa BBT asaini pale kwamba amefika ili tumhudumie Mtanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, hawa BBT na wenyewe wawe na mashamba ya mfano. Kama Waziri mwenyewe, Mheshimiwa Comrade Chongolo, pale kijijini kwake ana shamba, kwa nini BBT hana shamba la mfano?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri huyu BBT naye awe na shamba la mfano kwa ajili ya wakulima walioko kwenye maeneo yetu. Baada ya kusema...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)