Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Karatu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi. Kwanza ninamshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia, ninamshukuru Waziri, Naibu Waziri na watu wote kwenye Wizara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu unaanzia kwenye ukosefu wa mbolea kwa Takribani miezi minne sasa. Wizara wamejipangaje kwenye eneo hili la mbolea? Kwa sababu, katika jimbo langu takribani miezi minne sasa upatikanaji wa mbolea ni changamoto. Hii imechukua muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru Serikali inatoa mbolea ya ruzuku, lakini kwa sasa kila mwananchi anapewa mbolea mbili mbili au mbolea moja moja katika jimbo langu, na ninaamini na maeneo mengine katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa je, Wizara wamejipangaje katika upatikanaji wa mbolea? Kama changamoto ni vita inayoendelea katika nchi za wenzetu, mbona kwenye eneo la mafuta inapatikana? Kwa nini Wizara ya kilimo iko nyuma zaidi kuwatetea watu wao katika eneo hili la kilimo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuishauri Wizara. Hivi kulikuwa na ubaya gani kama mbolea inaletwa yenye ruzuku na ambayo haina ruzuku, ili inapoonekana mbolea ina upungufu kwa sababu, lalamiko la wafanyabiashara kwa sasa wanasema ni Serikali. Zile fedha za ruzuku hawaziweki kwa muda, ndiyo maana wafanyabiashara wanachelewa kuagiza mbolea kutokana na ucheleweshwaji wa fedha zile sasa za ruzuku inayowekwa kwa wafanyabiashara wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaonaje sasa kwamba, ilete mbolea ambayo haina ruzuku, ambayo mimi ambaye nitaona mbolea ya mifuko miwili hainitoshi, nitakwenda kununua ambayo haina ruzuku, ili mazao yangu yasiweze kuharibika katika maeneo yetu katika Jimbo letu la Karatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni katika Stakabadhi Ghalani. Mwaka 2025 Jimbo langu la Karatu limeingizwa katika mazao ya dengu na mbaazi na hakuna AMCOS hata moja katika jimbo zima. Vilevile utaratibu mzuri wa watu wetu wakivuna kipindi cha mwezi wa Nane mpaka mwezi wa Kumi, hupeleka mazao sokoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali kwa mwaka 2025, iliingia kwenye mageti kuzuia kwamba, sasa mazao yapelekwe ghalani, wakati huo katika jimbo langu zima hakuna ghala wala AMCOS ambayo Serikali inasema kwamba, tupeleke ghalani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni changamoto kubwa katika Jimbo langu la Karatu, mwaka wa 2025 ilituletea shida kwa sababu hakuna mahali popote pa kupeleka mazao. Chaji zao za kupiga faini watu za kuanzia shilingi milioni moja mpaka milioni tano na wakati huo Serikali haijajipanga kuandaa maghala hayo na hizi SACOSS katika maeneo ya Jimbo langu la Karatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo lingine la mipaka, Serikali yetu huwa kwa sasa wanasema tuna chakula kwa kiwango cha zaidi ya 100%, lakini inapofikia kipindi inapungua asilimia hiyo kutoka chini ya mia moja, wakati kuna upungufu wanasema mipaka yetu ifungwe kwa sababu ndani ya nchi yetu kuna shida ya chakula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama Wizara hii ilikuwa inatafuta masoko, wakati huo soko limeonekana huko nje, Serikali inaanza kusema tuna njaa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, siyo kazi ya mkulima wa Tanzania kwenda kulisha wananchi wa Tanzania, kazi ya mkulima wa Tanzania ni kwenda kulima apate fedha na maendeleo mengine yaendelee ndani ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nchi nyingine za nje zinapokuwa na njaa ndiyo fursa kwa mkulima wa Tanzania kwenda kupeleka mazao yake mahali popote, nchi zingine zote ambazo zina uhitaji wa chakula kipindi hicho. Huko nyuma imetokea na kutaifishiwa magari ya watu, imetokea katika mipaka yetu watu kutaifishiwa magari na mazao, lakini kwa miaka hii minne ya Dkt. Samia Suluhu Hassan tunatoa shukrani kwamba mipaka haijafungwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ninaomba Wizara iendelee kuachia mipaka ili watu wetu wanapopata soko katika maeneo mengine ya nje waweze kupeleka mazao yao. Kama Serikali hii inaenda kutafuta masoko, Serikali hii hii tena inasema mipaka ifungwe itakuwa ni jambo ambalo halipendezi kwa wakulima wetu, tutie wakulima wetu moyo katika eneo hilo la mipaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu la Karatu tulipata bahati ya kupata hela katika eneo la umwagiliaji. Serikali ilitupatia fedha shilingi milioni thelathini na nane na milioni mia tano katika skimu ya Kata ya Baray na Kata ya Mang’ola. Vilevile, Serikali ilitupa fedha shilingi bilioni ishirini na moja kuzuia maji katika korongo la Mto Baray. Hata hivyo, mradi ule wa shilingi bilioni ishirini na moja una changamoto kubwa, sasa tuna miaka mitatu, Serikali ilitoa fedha shilingi bilioni 3.5, kwa sasa mkandarasi yuko site anakaa tu mpaka miaka mitatu na Serikali imetoa fedha. Watu wa tume waliangalie hilo, katika eneo hilo la Mto Baray imetolewa shilingi bilioni 3.5 na mkandarasi yuko site, lakini hakuna kazi inayoendelea kwa sasa ni miaka mitatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo la umwagiliaji mradi wa shilingi 38,500,000,000 ambao uko katika Kata ya Baray na Kata ya Mang’ola unaendelea vizuri na Mheshimiwa Waziri Mkuu alikwenda kuweka jiwe la msingi mwaka huu katika eneo hilo la skimu katika Mto wa Qangdend katika Bonde la Eyasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)