Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Edwin Enosy Swalle

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MH. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi nianze kuchangia hotuba hii ya Wizara ya Kilimo ambayo ni hotuba muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, niseme kwamba, nilikuwepo hapa ndani wakati Rais, Samia Suluhu Hassan, anakuja kuhutubia Bunge kwa mara ya kwanza. Nikiwa kama Mbunge wa awamu ya pili, ninaweza kusema kwa ushahidi, Dkt. Samia anawapenda sana wakulima wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata Chama Cha Mapinduzi kinawapenda sana wakulima wa nchi hii. Kwa kiwango ambacho Rais ameongeza bajeti, kutoa ruzuku ya mbolea na kununua mahindi, ni dhahiri Dkt. Samia anawapenda wakulima wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ninatumia nafasi hii pia kumshukuru sana Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Daniel Godfrey Chongolo, kwa hotuba yake nzuri iliyoonesha dhamira ya kweli ya kuwasaidia wakulima wa Tanzania. Ninampongeza pia Mheshimiwa Silinde na wataalam wote wa Wizara hii akiwemo Katibu Mkuu, Ndugu yetu Mweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaongea mambo matatu tu kwa asubuhi ya leo. Jambo la kwanza nianze na ushirika. Nimesoma kwenye hotuba ya Waziri ukurasa wa 117-124, wameongea vizuri kuhusu ushirika, wana mpango wa kuhamasisha wananchi wafungue SACCOS, vikundi viunde SACCOS na kadhalika. Ushauri wangu kwa Serikali, ndugu yangu Dkt. Ndiege ninajua ananisikia vizuri sana. Tatizo kwenye ushirika ni vyama vya ushirika kuwaibia wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Njombe kwa mfano, maeneo mengi vyama vya ushirika vimeibia wakulima fedha. Lupembe wananchi wangu wameibiwa fedha, Makambako ambako Mheshimiwa Waziri ametoka pale na nimsemee yuko hapa. Pale Makambako chama cha ushirika kimekula fedha za wakulima, ukienda Igumila, ukienda Njombe. Ninamwomba Mheshimiwa Waziri wa Kilimo kwenye hotuba hawajasema wana mpango gani wa kuwasaidia wakulima walioibiwa fedha zao kwenye ushirika ziweze kurejeshwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo muhimu sana, waje na huo mpango mahsusi watuambie wakulima hawa kabla ya kuhamasisha kufungua SACCOS zingine, watuambie wananchi ambao hela zao zimeibiwa wanawasaidiaje fedha iweze kurudi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kuhusu zao la parachichi. Sisi Mkoani Njombe kama wakulima wa zao la parachichi, wananchi wengi wanalima haya matunda. Changamoto kubwa ni juu ya uhifadhi wa mazao ya parachichi. Wananchi wa Lupembe wamenituma, niiombe sana Serikali kwenye mpango wake ambao inakwenda nao watusaidie kujenga cold rooms kwa ajili ya kuhifadhi matunda ya parachichi ili kusudi yaweze kuwa na bei nzuri na yasiuzwe kwa kutupwa kama sehemu ya reject. Hii ni hoja muhimu, jimbo la Lupembe wanaomba kujengewa cold room na hata wananchi wa Makambako kwa Mheshimiwa Waziri wanahitaji cold room pia kwa ajili ya matunda ya parachichi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni zao la chai. Ninaipongeza sana Wizara hii, nimesoma kwenye hotuba, kwa mara ya kwanza zao la chai limeandikwa angalau kwa page nne. Hongera sana kwa Mheshimiwa Waziri, ameandika page nne kujadili zao la chai na hapa ninampongeza sana pia Mkurugenzi wa Bodi ya Chai, dada yangu Beatrice Banzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wameandika mipango humu kwenye hotuba hii kwamba wana mpango wa kulikwamua zao la chai. Ombi langu Mheshimiwa Waziri, wananchi wa Lupembe wamelia kwa muda mrefu kutaka kiwanda chao kirejeshwe. Ninamwomba Mheshimiwa Waziri, wamesema kwenye taarifa hii, wakirudi ofisini baada ya bajeti hii wakarejeshe kiwanda cha wakulima wa Lupembe tuweze kwenda mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, wamesema zao la chai duniani bei imepanda kutoka shilingi 2,450 mpaka shilingi 4,000. Ninataka niiombe sana Serikali, badala ya kujadili kupunguza bei ya chai, tufikirie kuongeza bei ya wakulima wa chai hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine pia kwenye chai, sisi watu wa Mkoa wa Njombe wanaweza wasituelewe, tunaposema kuhusu viwanda vya DL, hatusemi personal. Viwanda hivi vilichukuliwa vikiwa vinafanya kazi, lakini baada ya viwanda vyote vile kuwa vimechukuliwa sasa havifanyi kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma kwenye taarifa kwamba wanakwenda kufanya tathmini. Mheshimiwa Waziri, waende wakafanye tathmini viwanda vya chai, kama wawekezaji hawa wamekiuka masharti, wachukue hatua wapewe watu wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwa asubuhi hii pia niseme kuhusu pembejeo za wakulima. Wananchi wetu ni kweli wanapata mbolea na mbegu, lakini masoko ya uhakika kwenye mazao wanayovuna, bei ambayo wanalima na bei ambayo wanauza haviendani! Tunaiomba Serikali iwasaidie wakulima wapate bei nzuri ya kuuza mazao yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hoja hizo tatu, ninaunga mkono hoja hii ipite kwa kishindo ili Waziri akafanye kazi yake. Ahsante sana. (Makofi)