Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. EXAUD S. KIGAHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika hotuba hii ya Wizara ya Kilimo. Kwanza, ninamshukuru sana Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, aliyetujaalia kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu siku hii ya leo. Pili, ninachukua nafasi hii kutoa pongezi za kutosha na nyingi kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi kubwa anayoifanya sekta tunayoiongelea leo, sekta ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatoa pongezi za kutosha pia kwa Wizara ya Kilimo chini ya Comrade Chongolo, mkulima mwenzangu ambaye kwa kweli amekuja na mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo na huu ni mwanzo mzuri. Ahsante sana na pongezi zote kwa Wizara nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaanza kwa kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja katika hotuba hii ya bajeti ya Wizara ya Kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ninashukuru sana, Waziri, mkulima mwenzangu na mimi hii ni Wizara yangu, ni mkulima katika sekta ya chai, ninakushukuru sana. Changamoto ya sekta chai kwangu mimi, Jimbo la Mufindi Kaskazini, kilimo ni maisha kama walivyosema wengine lakini sisi chai kwetu ni maisha. Yeye anajua mimi nimelelewa kwenye chai na chai ndiyo kila kitu kwetu. Leo hii changamoto ya chai chini ya mwekezaji ambaye wengi wamemsema DL Group kwa kweli ni changamoto kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii, wananchi wenzangu, wakulima wenzangu na wafanyakazi wengine, moja; mwekezaji huyu anadaiwa zaidi ya shilingi 5,000,000,000 kwa michango ya wafanyakazi katika kile Kiwanda cha Itona. Pili, wakulima wadogo wanaopeleka chai katika kiwanda kile hawajalipwa kwa zaidi ya miaka karibu miwili sasa. Tatu, wazabuni waliokuwa wanapeleka tenda pale nao wanadai. Kwa hiyo, ni changamoto kubwa katika maeneo mengi ikiwemo pale kwangu Mufindi Kaskazini katika Jimbo lile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wengi sasa ambao tuliwahamasisha kulima chai katika Kata za Ihanu, Mdabulo, Ihalimba, Ifwagi na maeneo jirani wana changamoto kubwa. Mwekezaji huyu pamoja na mambo mengine, analima chai, lakini amekuwa na changamoto kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale tuna makampuni mawili, DL Group na Brown. Brown anafanya vizuri, changamoto aliyonayo yeye hatuielewi, kama walivyosema wenzangu tunadhani labda mwekezaji huyu ana nia ovu au hana nia njema. Tukasema mhujumu kwa namna moja au nyingine. Wizara ya Kilimo tunaomba wachukue hatua tuone namna gani tunawakwamua Watanzania ambao wanategemea kilimo na hasa Jimbo la Mufindi Kaskazini na maeneo mengine ambayo tunalima chai. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Iringa inashika nafasi ya pili sasa kwa GDP per capita, baada ya Dar es Salaam ilikuwa Mbeya sasa tunakuja juu. Mengi haya katika Mkoa wa Iringa GDP per capita inatoka Wilaya ya Mufindi na moja ya maeneo ambayo yanatoa fedha nyingi ni kwenye sekta ya kilimo ikiwemo chai. Hatuko tayari kuona tunashuka kwenye GDP per capita kuwa namba mbili kwa sababu ya wawekezaji ambao hawafanyi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye sekta ya chai ninashukuru, lakini niseme kidogo kwenye maeneo mengine, kwenye umwagiliaji kama walivyosema Wabunge wenzangu, tunadhani maendeleo sasa kwenye sekta ya kilimo tukuze umwagiliaji. Kwenye Jimbo la Mufindi Kaskazini tunayo skimu ya umwagiliaji ya Ikweha ambayo imekwama kwa zaidi ya miaka 10. Zaidi ya shilingi 800,000,000 ziliwekwa pale, mradi ule umekuwa sasa wenzetu wazungu wanasema white elephant. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shilingi 800,000,000 zimelala pale na sisi kule tulikuwa tunatumia mabonde haya kwa kilimo a.k.a vinyungu, wanajua ni bustani zile za mabondeni. Baada ya kuboreshwa imekuwa sasa haifanyi kazi, badala ya kuboresha sasa imekuwa ni uharibifu, wananchi sasa wanashindwa kuzalisha kwenye eneo lile la bonde. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba, Tume ya Umwagiliaji iliahidi mwaka jana ikaja kukagua, wakasema wanaleta fedha mpaka leo kimya. Tunaomba mradi huo wa umwagiliaji wa Ikweha ukamilike mapema kama ambavyo Rais amekuwa akitaka kilimo kiendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni kuhusu mbolea. Nimshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya kuzalisha mbolea hapa nchini. Tuna INTRACOM lakini pia tuna kile cha Minjingu, wananchi sasa wameanza kuamini mbolea zinazozalishwa ndani. Niiombe Serikali yangu na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ana nia njema, tuone namna gani; moja, kuhakikisha kwamba tunawawezesha wawekezaji wa ndani ili wazalishe kwa tija ili tuendelee kufaidika na uwekezaji wa ndani na kuhakikisha kuwa wakulima sasa wanaanza kuzoea na kuona mbolea ya ndani inaweza ikafanya vizuri zaidi kuliko ya kutoka nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipatia muda. (Makofi)