Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Thomas Maganga Kampala

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Katavi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027


MHE. THOMAS K. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Ahsante na nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa rehema na kibali cha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuchangia hoja ya Wizara ya Kilimo. Nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, ndugu yangu Daniel Chongolo, kwa kazi nzuri anayoifanya. Nami nimtakie kila la kheri, Mwenyezi Mungu amsaidie atimize majukumu yake; na sisi wakulima tuna matarajio makubwa sana na yeye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Mheshimiwa Waziri anisikilize vizuri sana. Mheshimiwa Waziri akitaka kumsaidia mkulima wa Tanzania ni lazima achukue hatua za makusudi kuwezesha kuwekeza nguvu kubwa kwenye kilimo cha umwagiliaji. Nimpongeze sana kwa hatua anazozichukua na nimpongeze sana, kwenye Jimbo langu la Katavi pale nina mabwawa matatu. Nina Bwawa la Ipati, Bwawa la Irunde na Bwawa la Ipwaga Masigo; yote haya wamekwishakuja wataalam, wameyafanyia stadi na wamejiridhisha kuwa yanaweza kutoa matokeo kwa wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nimwambie Mheshimiwa Waziri, kwamba hakuna namna anayoweza kuisaidia nchi hii kwenye sekta ya kilimo kwenye angle ya kilimo bila kuwekeza kwenye kilimo cha umwagiliaji. Mabadiliko ya tabia ya nchi yanabadilika kila kukicha. Tutoke kwenye hatua ya kusubiri kilimo cha mvua za masika na vuli twende kwenye kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nimwambie Mheshimiwa Waziri, mwaka wa 60 nchi nyingi ambazo tulikuwa tunalingana nazo uchumi ikiwemo China na Vietnam wamepiga hatua kubwa kwenye angle ya kilimo kwa sababu waliwekeza kwenye kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Jimbo la Katavi tunalima sana tumbaku. Kwenye zao la tumbaku tumeingia kwenye kilimo cha mkataba (contract farms), linafanya vizuri sana. Na kwenye kilimo cha mkataba Mheshimiwa Waziri limeitoa zao la tumbaku kule likokuwa mpaka sasa Jimbo la Katavi ni wazalishaji wakubwa wa zao la tumbaku kwa sababu ya kilimo cha mkataba, lakini ukiangalia (contract farm), kilimo cha mkataba hakina sheria. Imefika wakati sasa Wizara kuja na mkakati mahsusi wa kuleta mabadiliko ya Sheria ya Kilimo cha Mkataba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nimwambie Mheshimiwa Waziri kwamba, kuliko sasa tulivyo, wakulima wanalima na wanaingia mikataba ya hiari; mikataba ya hiari ni very risk kwenye maisha ya mkulima; nimwombe sana kaka yangu Mheshimiwa Chongolo, kilimo cha mkataba lazima uingie kwa makusudi kuwekeza kwenye upande wa sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, kwa sababu muda ni mfupi, nimwombe Mheshimiwa Waziri, tunayo taasisi yetu ya COPRA inafanya kazi vizuri sana; lakini changamoto waliyonayo COPRA watumishi wachache na taasisi ni changa. Hii taasisi iongezewe bajeti. Ushauri wangu kwa dada yangu Irene; anafanya kazi vizuri sana, lazima na yeye sasa utoke nje ya boksi aingie kwenye kuwahamasisha wakulima kwenye kilimo cha mkataba. Yaani lazima atoke kuhamasisha kilimo, asiwe sasa amekaa anasubiri wakulima wanalima kazi yake ni kukusanya ushuru. Atoke, atoke akahakikishe anawahamasisha wakulima waingie kwenye kilimo cha mkataba. Hii ni kwa sababu ni kilimo cha mkataba pekee yake ndicho kinachoweza kumkomboa mkulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la pamba lilikufa sababu ya kilimo cha buyaga buyaga. Sasa kilimo cha mkataba katika nchi hii ndicho kitakachokwenda kumkomboa mkulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa nne ni kuhusu kilimo cha bangi. Umefika wakati Taasisi yetu ya TARI itoke nje ya boksi ikafanye utafiti wa kilimo cha bangi kwa ajili ya huduma za kitabibu. Si haya wanayowatazama na wanayofikiri kwenye watu wengine. Nchi nyingine kama Uholanzi, Venezuela, Mauritius, wanatumia kilimo cha bangi kwa ajili ya shughuli za kitabibu. Sasa hapo ukiongea kilimo cha bangi watu wote wanawaza negative hawaendi positive, hatuwezi kutoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, TARI wasijifungie ndani, watoke nje watwambie; kama kweli tafiti zinaonesha hiki kilimo kinaweza kutusaidia kwa ajili ya huduma za kitabibu kuna shida gani kuleta sheria hapa?...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Thomas Maganga.

MHE. THOMAS K. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.