Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika wizara hii yetu pendwa, Wizara ya Kilimo. Niseme tu, mimi ni mmoja ambao wanaamini katika suala la kilimo. Kwa kweli ninaamini kwamba kama kilimo kitapewa kipaumbele, ni kitu ambacho kinaweza kikawasaidia Watanzania wengi katika kuinua maisha yao. Ukweli ni kwamba bado hali ya Watanzania si nzuri kiuchumi, hasa wale wanaohusika na masuala ya kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa muda ni mdogo sana ningependa kujielekeza moja kwa moja kwenye mchango. Niendelee kuipongeza Wizara na kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo wanaendelea kupambana kuona kilimo kinaendelea kuwa ni kitu cha msaada kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitataka niongelee kwenye jambo la mbolea, Mfuko wa Pembejeo kwa ujumla na masuala ya AMCOS, Vyama vya Ushirika hivi, SACCOSS, AMCOS. Ninataka nianze na Mfuko wa Pembejeo ili dakika zitakapokwisha niwe nimeshaongea kitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa napitia Taarifa ya Mheshimiwa Waziri hapa, wanaonesha kwamba wataupatia Mfuko wa Pembejeo shilingi 5,000,000,000 ili uweze kuwafikia wananchi wa chini waweze kupata mikopo yenye riba nafuu. Nikaenda mbele tena nikaona wanasema kupitia huo Mfuko wa Pembejeo kuna dola milioni 35, ambapo nilipofanya calculation nikapata shilingi 91,000,000,000 ambayo itaenda kwenye taasisi za kifedha ili waweze kukopeshwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikashuka chini zaidi nikakuta kipengele kingine, wanasema wataweza kuwapatia wananchi bilioni 21.47 kwa ajili ya mikopo ya riba nafuu kupitia Mkulima Nafuu Loan na Mkulima Loan na mengineyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hofu yangu, kwa sababu huu Mfuko tumeanza kuusikia siku nyingi, tumekuwa tukienda kuwahamasisha wananchi wetu, kwamba Wizarani kuna Mfuko wa Pembejeo ambao unatoa mikopo kwa wananchi; hawajaweza kupata fedha katika maeneo yetu. Wanatuhakikishia vipi kwamba fedha hizi zitaenda kwa wananchi? Kwa sababu fedha iliyokuwa imetengwa kwa mwaka wa fedha uliopita tulisikia hapa, wametuambia imeenda kwenye Benki ya Ushirika, bilioni tano out of bilioni tano point mbili, kama nina kumbukumbu vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ninataka kusema nini? Ni kwamba huu Mfuko mimi kama Mheshimiwa Mbunge wa Wanawake, Mkoa wa Songwe sina imani nao. Ninasema haya nikiwa na ujasiri kwa sababu nimeenda kule Wizarani, nimefuatilia, nimehamasisha wananchi wangu na hakuna hata mmoja mpaka saa hizi aliyepata fedha. Hata tulipokuja hapa ilionesha kuwa ni watu 49 tu katika nchi hii ndiyo walioweza kupata hiyo fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo huu Mfuko tunaomba kama kweli upo na unafanya kazi tuuone kwenye maeneo yetu kwamba unawasaidia wananchi wetu. Pia na hiyo Benki ya Ushirika watafute fedha za kuipa hiyo Benki ya Ushirika, siyo hizi fedha wanazotutengea sisi wananchi ndiyo waende kuzipa hizo Benki za Ushirika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ninachotaka kuongelea ni suala la mbolea. Ukweli ni kwamba mbolea ilikuja, lakini pia kumekuwa na uhuni mwingi kwenye mbolea. Ninayasema haya kwa sababu tumeona tukienda kwenye vikao kule chini wananchi wanatuambia mbolea imefika, lakini unakuta bei inayotajwa ya ruzuku huku ni tofauti na wanayouziwa wananchi. Kwa hiyo tuombe Wizara iongeze usimamizi wa hizi mbolea za ruzuku wanazozipeleka kule chini ili wananchi wapate kwa bei ambayo imelengwa. Hilo nisiongee sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka pia niongelee suala la AMCOS na SACCOSS. Hasa zaidi AMCOS ambao alikuwa anaongea kaka yangu hapa, Mheshimiwa Enosy Swalle. Amesema vyama vya ushirika vina wizi mkubwa. Hata wakisikia Mheshimiwa Mbunge anaongea wanamkasirikia, hawataki kusikia kwamba wao wanafanya uwizi wa kuwaibia wananchi wetu fedha. Alikuwepo hapa kaka yangu Mheshimiwa Mwenisongole, ilikuwa ni ajenda yake ya msingi humu ndani. Walikuwa wanamkamia, wanampania kwamba hatarudi Bungeni kisa tu ameongelea kwa habari ya mambo wanayoyafanya kwenye AMCOS.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunamwomba Mheshimiwa Waziri, kaka yetu Chongolo, Mheshimiwa Naibu Waziri, kaka yangu Silinde na Katibu Mkuu na timu yake kipengele hiki cha AMCOS wakisimamie vizuri wizi upungue huko chini. Wanaoumizwa ni Watanzania wenzetu ambao hiyo ingekuwa ni fursa ya kwao kutengeneza maisha yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha ambazo zimeingizwa na AMCOS kweli ni nyingi, hii shilingi trilioni ngapi iliyotajwa hapa ni fedha nyingi sana. Nimesoma hapa, mwaka huu imechangia trilioni 3.74. Ninavyofahamu mimi, utitiri wa vyama vya ushirika hivi ambavyo viko hapa, si kweli kwamba vyote vinafanya kazi kwa ukubwa huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanapoenda kuvihamasisha viweze kukua watusaidie, waje na mkakati ambao vyama vyote vikue kusiwe na vile vyama wanavyovithamini tu vile vikubwa ambavyo tayari vimeshavijenga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninakushukuru kwa nafasi hii na ninaunga mkono hoja. (Makofi)