Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Florent Laurent Kyombo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkenge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa nafasi ya kuchangia Bajeti ya Wizara ya Kilimo. Kwa nafasi kabisa, kwanza ninamshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mageuzi makubwa ndani ya sekta hii. Tunaona BBT zimeanza na afua nyingine ambazo zinaendelea ndani ya Wizara ya Kilimo. Kwa nafasi ya pekee ninampongeza sana Mheshimiwa Daniel Chongolo na msaidizi wake ambaye ni Mheshimiwa David Silinde.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kusema haya maneno machache, kwamba Mheshimiwa Chongolo hayuko pale kwa bahati mbaya. Ukiangalia katika maneno Matakatifu Daniel alikuwa ni nani? Alikuwa ni mtu anayetafsiri maono ya Mfalme Nebukadreza na yeye Mheshimiwa Rais amemweka hapa akatafsiri maono yake ndani ya Wizara ya Kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakumwacha peke yake, akamwongezea Mheshimiwa David, ambaye ni Daudi. Daudi alikuwa kijana mdogo, kwa kombeo na jiwe aliweza kumuua Goriati na maisha yakaendelea. Kwa hiyo, tunamwomba atafsiri ndoto za Mheshimiwa Rais katika kilimo. Mtume Daudi, huyo David aende kule chini kuhakikisha kwamba maono ya Mheshimiwa Rais yanaweza kufika. Hiyo collabo (Collaborate) ya watu wawili Daudi na Daniel ukiunganisha na Mtendaji Mkuu wa Wizara ndugu yangu makini sana Gerard Mweli, ninaamini wataenda mbele na Makatibu Wakuu wawili pamoja na viongozi wengine ndani ya Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita katika maeneo manne. Eneo la kwanza ni kuhusiana na masoko ya mazao, lakini eneo la pili katika eneo la kimkakati la kilimo cha umwagiliaji la Bonde la Mto Ngono na eneo la tatu ni maboresho ya vibali ndani ya COPRA na mwisho nitashauri katika maendeleo ya Tume ya Ushirika. Katika masoko ninaendelea kupongeza juhudi za Mheshimiwa Rais, ameendelea kujenga masoko katika maeneo mbalimbali ndani ya nchi. Hapa sasa tunaona masoko matano yanaendelea kujengwa katika Halmashauri za Ngara, za Tarime, Kyerwa pamoja na Kahama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ni shahidi, wanaendelea kubainisha kujenga masoko ya mazao katika maeneo ya Rusumo, Namanga pamoja na Kasumulu na Holili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Chongolo amekuwa Mtendaji wa Chama, hivyo anaijua nchi hii vizuri. Eneo la Mutukula ndani ya Wilaya ya Misenyi ni eneo linalofanya kazi kubwa ya biashara ya mazao nje ya nchi. Ukiangalia katika takwimu Mwaka wa Fedha 2023/2024, zaidi ya tani 300 zimeuzwa pale, mwaka uliopita tani 50,000. Nimwombe Mheshimiwa kwa ajili ya Wanamisenyi, aweke mazingira mazuri ya ushindani ndani ya Wilaya ya Misenye eneo la Mtukura. Nimwombe akija kuhitimisha atuambie ni lini anaenda kujenga soko la mazao ndani ya eneo la Mutukula ili tuweze kufanya biashara shindani na wenzetu wa Nchi ya Uganda na maono ya Mheshimiwa Rais yaweze kufikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kuhusu eneo la kimkakati la Bonde la Mto Ngono. Tunajua Bonde la Mto Ngono, Mheshimiwa Waziri wamekwishaliainisha, lina hekta 16,000, linajumuisha wilaya tatu ndani ya Mkoa wa Kagera, is a game changer ya uchumi wa Mkoa wa Kagera; na Wilaya ya Misenyi tunaona katika eneo la Nkenge, Buchurago, Buturage, pamoja na Burembo ni maeneo yote. Ukienda Wilaya ya Muleba yapo maeneo saba, ukienda eneo la Bukoba Vijijini yako maeneo saba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amesimamia upembuzi umekamilika, usanifu umekamilika, wakandarasi wamepatikana, leo majadiliano ya kusaini mkataba yamechukua muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Daniel mtafsiri ndoto na maono ya Mheshimiwa Rais, ninamwomba aje kuhitimisha kutuambia je, ni lini mikataba hiyo inaenda kusainiwa ili Bonde la Mto Ngono tuweze kupata mazao na iwe game changer ya uchumi ndani ya mkoa wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, COPRA inafanya kazi vizuri, inatoa vibali. Ombi langu, kwa ajili ya Wanamisenyi na wananchi wengine ambao wanapata vibali vya mazao; tunatoa kibali cha tani 100 tu ilhali pembeni mtu anao mzigo wa tani 1,000, anazo tani 500. Niombe kiwango hicho kiongezwe. Vijana wanakuwa wamekwishapata mazao, yako pembeni wanasubiri kibali kimoja. Kwa hiyo akitoa kibali cha tani 1,000 au tani 2,000 inampa nafasi mfanyabiashara kufanya vizuri na kuondoa gharama zingine ambazo anaweza akazipata kwa sababu ya usafirishaji. Kwa hiyo niombe idadi ya vibali tani ziongezeke; lakini na muda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba mfumo upo unafanya vizuri na taasisi yetu inafanya kazi vizuri, niombe Mheshimiwa Waziri, asimamie vizuri kazi inayoendelea ndani ya COPRA muda wa kuidhinisha vibali angalau masaa machache kama mtu ame-comply vigezo vyote apewe kibali aendelee na biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa mwisho ni katika Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania. Mheshimiwa Rais amefanya kazi katika Tume hii, imekuwa na maendeleo makubwa. Tunaona leo Benki ya Taifa ya Ushirika imeanzishwa, tunaona viwanda vilivyokuwa vimekufa sasa vimefufuliwa, tunaona kumeanza kuwa na mfumo ndani ya Tume ya Ushirika ambao umeunganishwa na mifumo mingine. Kazi nzuri inafanyika. Tunaomba Wizara iunge mkono, kuisaidia kwa sababu mambo yanayotekelezwa ndani ya tume hiyo mengine katika vyama vya ushirika hawaungani nayo kwa sababu ya maslahi. Tuwape nguvu waweze kusimama na kutekeleza maono ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo bima ambayo imeanzishwa kwa ajili ya wakulima. Mkulima akilima iwe ni mafuriko, iwe ni mvua ya mawe, iwe ni upepo, mkulima anakuwa-compensated kwa ajili ya mazao yake. Vilevile tunaona wameleta mizani mizuri ya kupima mazao ya mkulima ya electronic, mkulima hapunjwi mazao yake; lakini hayo mambo yana vipingamizi kule kwenye vyama vya ushirika. Tume wapewe nguvu ili iweze kusimama vizuri na kuhakikisha kwamba maono ya Mheshimiwa Rais yamekamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajua nimevumiliwa, ninashukuru. Kwa maono ya Mheshimiwa Rais ya Daniel na Daudi ninaomba wakafanye kazi ili tuhakikishe kwamba Wizara yetu inaendelea kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)