Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Jacquline Andrew Kainja

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. JACQUELINE K. ANDREW: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kuongea Bungeni hapa naomba nianze kumshukuru Mungu kwa nafasi aliyonipa, baraka na kibali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru Chama changu Cha Mapinduzi kikiongozwa na Jemedari wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuniteua kuwa Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Tabora ninayetokana na wanawake wa UWT. Ninawashukuru sana akina mama wa Mkoa wa Tabora kwa kunichagua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, moja kwa moja niende kwenye Hotuba ya Wizara ya Kilimo, nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kuwasilisha vizuri. Pia, nimpongeze Naibu Waziri pamoja na timu nzima ya Wizara ya Kilimo kwa kazi nzuri wanazofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wetu wa Tabora kwa 80% tunategemea kilimo, kilimo ndiyo uti wa mgongo na uchumi wetu unatokana na kilimo kwa asilimia kubwa sana. Hivyo, uchumi wetu upo ndani ya Wizara ya Kilimo, hivyo niombe Wizara na nimwombe Waziri aweze kutuangalia wanamkoa wa Tabora kwa jicho la tatu kwa kuweza kutusaidia kupandisha uchumi wetu kuwa wa kiwango kikubwa kutokana na kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna zao la korosho ambalo Serikali ilileta ambalo lilikuwa ni zao jipya kwa wananchi wa Mkoa wa Tabora na wakulima wakalipokea na wakaanza kufanyia kazi lakini bado tuna changamoto katika zao hilo. Changamoto ya kwanza ni masoko, masoko yamekuwa ni changamoto sana. Lakini vilevile viuatilifu vinavyotolewa na Bodi ya Korosho kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026, wakulima wa zao la korosho Mkoani Tabora walilima eka 14,632 lakini viuatilifu vilivyotolewa ni vya eka 1,438, sawasawa na 10%. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unaona kabisa bado mkulima huyu wa korosho hajasaidiwa ikiwa ni zao ambalo la kibiashara na wakulima wameona waliangalie kama mbadala wa tumbaku. Niombe sana Wizara na nimwombe sana Mheshimiwa Waziri awasaidie sana wananchi hawa wa Mkoa wa Tabora waliowekeza kwenye zao la korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nihamie pia kwenye zao la tumbaku. Wananchi wa Tabora tunategemea sana tumbaku kwa asilimia kubwa na tumbaku kwa mwaka huu, msimu huu, bei imekuwa imeshuka sana. Msimu uliopo sasa wa Serengeti mkulima analipwa dola 1.45, lakini gharama za uzalishaji kwa kilo ni dola 1.85 unaona kabisa mkulima huyu amefanya kilimo hiki kwa hasara.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hivyo kilimo hiki ni kigumu sana na wananchi wa Tabora tunagemea uchumi ina maana wakulima wanapopata ndipo wafanyabiashara wengine hawa wanaweza kupata mzunguko wa mahitaji yao. Kama kilimo kikidondoka moja kwa moja mkoa huu unakuwa umedondoka kiuchumi. Niombe sana Mheshimiwa Waziri atuangalie, sisi wananchi wa Tabora kwa ajili ya kupandisha uchumi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe vilevile Wizara kusimamia ahadi zilizowekwa na viongozi wetu wakubwa wa kitaifa. Kwa mfano, Mheshimiwa Rais alipokuwa akinadi Ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi aliahidi viwanda. Tunaomba viwanda hivyo vitano ambavyo vimeahidiwa na Mheshimiwa Rais wakati wa kuomba kura, basi viwanda hivyo vitekelezwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba kiwanda cha kuchakata tumbaku kiweze kupatikana kwa sababu maeneo yameshatengwa, wananchi wameshayaandaa Ilolangulu ambapo ni Uyui na Ifucha ambapo ni Tabora. Tunamwomba Mheshimiwa Waziri tupate kwa uharaka kiwanda cha mbolea. Tunaomba Kiwanda cha Pamba Igunga, tunaomba kiwanda cha nyuzi ambazo pesa zake tayari zimeshatengwa, ni suala la uamuzi tu wa Serikali kuanzisha kazi hiyo kwa uharaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye suala zima la kilimo chenye tija kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji. Tunapongeza sana Serikali na Wizara kwa kutusaidia, Urambo tumepata Bwawa Kalemela A limeshakamilika, lakini bado Mkoa wa Tabora tuna maeneo 47 ambayo yametengwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa ahsante sana…

MHE. JACQUELINE K. ANDREW: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa malizia sentensi…

MHE. JACQUELINE K. ANDREW: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niunge mkono hoja. (Makofi)