Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CUF
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika hii Wizara ya Kilimo. Kwanza nianze na kumshukuru Mungu Mwenyezi kwa kunipa kibali cha kuweza kusimama siku ya leo. Niwashukuru na niendelee kuwashukuru sana wananchi wa Kigoma Kaskazini kwa kuniamini na kunipa heshima ya kuwa mwanamke wa kwanza kuongoza Jimbo la Kigoma Kaskazini na sitawaangusha niko hapa kuwapigania maslahi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma Bajeti ya Waziri wa Kilimo. Nichukue fursa hii kuwapongeza kwa namna ambavyo mnafanyakazi lakini wote tunasema kilimo ni uti wa mgongo. Asilimia 65 ya Watanzania wanategemea kilimo na wote tuko hapa Bungeni tumekuzwa na wazazi ambao ni wakulima na pato la Taifa 29.1% linatokana na kilimo, lakini kilimo Tanzania bado kina changamoto kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri pamoja na kazi ambayo unaifanya na Naibu wako na ninafurahi katika mpango wenu wa 10/30 ambao wamejipanga kuhakikisha kwamba tunatoka tulipo kilimo kinatusaidia kuboresha maisha ya Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwaombe sana, yapo mazingira ambayo kilimo bado ni changamoto. Jambo la kwanza suala zima la zana. 65% ya Watanzania kama nilivyosema ni wakulima, lakini wengi bado wanatumia primitive way, hawana vifaa vya kulimia. Ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri ahakikishe wanawasaidia wakulima. Wakulima wengi wanatumia majembe, wakulima wengi hawana uwezo, wakulima ambao wana uwezo wa kununua trekta au caterpillar ni wachache sana labda ni 10% kati ya 100.
Mheshimiwa Naibu Spika, wengi ukija kama kule Jimboni kwangu Kigoma Kaskazini wengi wanatumia majembe. Wizara iweke miundombinu ya kuwasaidia kama ni mikopo Benki ya Kilimo wawape wakulima mikopo wanunue vifaa vya kufanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo wakulima wa Tanzania ni changamoto kwao ni suala zima la masoko. Leo Watanzania wanalima mazao, lakini wengi wao hawajui mazao wanakwenda kuyauza wapi baada ya kuvuna? Ukiangalia kwa mfano, ndani ya Jimbo la Kigoma Kaskazini kule kwetu Manyovu Kusini watu wanalima sana kahawa na ni moja ya sehemu ambayo kahawa bora inatoka ndani ya Jimbo la Kigoma Kaskazini - Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, hawa wakulima ambao wanatumia pesa, wanatumia gharama, maisha ni magumu, lakini wakishavuna hawajui wapi wanakwenda kuuza kahawa yao. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, siku zote ninaamini katika competition hata ndani yawezekana ukiwa na mke mmoja yuko peke yake akavimba sana kwa sababu yuko peke yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hawa wanaokuja kununua mazao ya hawa wakulima wa kahawa Kigoma yuko mtu mmoja Chama cha Ushirika cha Kanyovu ndiye anayenunua mazao, hii kahawa ya wakulima wa Kigoma Kaskazini. Maana yake ni kwamba hana competition anapokuja kwenye soko atanunua kahawa kwa bei anayoitaka yeye kwa sababu hakuna mtu mwingine anayekuja kununua ile kahawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri atuletee watu wa kuja kununua kahawa yetu. Watuletee watu wa kuja kununua mazao yetu, tusitegemee mtu mmoja. Tutafute watu kutoka nchi mbalimbali, tuna kahawa nzuri sana, lakini mazao mengine kama pamba na parachichi Tanzania tunazalisha product ambazo ni very quality na pure.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda katika nchi za wenzetu unaweza ukashangaa na ninatamani sana tuchukue kilimo kwamba ni very serious kwa sababu ndiyo asilimia kubwa ya Watanzania tunategemea. Nimshauri Mheshimiwa Waziri tuwekeze sana katika kilimo cha umwagiliaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo ukienda Morocco unaambiwa Morocco wana uwezo wa kukaa miaka sita hawajaona mvua, lakini wamepiga hatua katika kilimo kwa sababu wana mabwawa ya umwagiliaji. Kwa nini sisi Tanzania tuna mvua, tuna ardhi yenye rutuba, lakini ukija hapa miaka yote tunazungumza skimu za umwagiliaji? Kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri tuwekeze katika skimu za umwagiliaji, tuna ardhi yenye rutuba, kule Kigoma tuna mabonde, tuwekeze tuweze kulisaidia Taifa na litoke katika umaskini.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka nizungumzie suala la mbolea…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kiza, muda umekwisha, unga mkono hoja tuendelee.
MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Naibu Spika, dakika moja…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa malizia sentesi ya mwisho…
MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Naibu Spika, sawa. Jambo la mwisho, Mheshimiwa Waziri ni suala zima la mbolea hapa watu wanasema mbolea inafika, tusemeni ukweli na Mheshimiwa Waziri afanye research, ashuke chini, akutane na wakulima, asitegemee hao watu waliokaa maofisini wampe majibu sahihi, wananchi huko wanalalamika hawapati mbolea kwa wakati…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa ahsante sana.
MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)