Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. NASSRIYA NASSIR ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi hii ya kuchangia kwa mara nyingine tena. Kwanza nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia hadi nikapata nafasi ya kusimama hapa na kutoa mchango wangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi yake kubwa ambayo ameifanya kwenye nchi yetu na ninaweza kusema ni mwanamke jasiri na mama mwenye maono kwa wananchi wake. Ninaweza kusema ni shuhuda namba moja wa Mheshimiwa Rais na kazi zake ni mwanamke ambaye ni very strong, hakuna mfano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru vilevile Mheshimiwa Rais kwa jitihada zake za kutekeleza masuala mengi yanayohusu watu wenye ulemavu katika hali ya ujumuishaji. Tunapoongelea kilimo tunaongelea pia Dira ya Mwaka 2050. Nilikuwa ninafuatilia vizuri Hotuba na hoja ambayo iko Mezani juu ya Bajeti ya Kilimo na nimefuatilia kwa ukaribu na nimejaribu kuangalia kama kuna mahali nitaona kuhusiana na wanawake na vijana katika ujumuishwaji wa masuala mazima ya kilimo na uchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninatamani kujua watu wenye ulemavu wamejumuishwa vipi kwenye programu mbalimbali za kilimo ambazo zinaendelea hapa nchini? Kuna huu Mradi unaitwa BBT, (Jenga Kesho Bora). Ninatamani sana kuona watu wenye ulemavu wamejumuishwa kikamilifu kuhusiana na huu mradi. Kwa sababu na wenyewe pia ni wakulima na wenyewe ni Watanzania na wenyewe wana nguvu kazi, wana uwezo wa kufanya hayo yote kama watu wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo sioni sababu ya wao kuachwa kwenye programu kama hizi wakati zinaweza kuwainua kiuchumi. Hata hivyo, nina imani sana na Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Daniel Chongolo kwa uwezo wake mkubwa na ninaamini kazi yake ni njema katika hii Wizara atakwenda kutujumuisha watu wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu Tanzania kuna watu wenye ulemavu wa kila aina na wapo kila Mkoa na vijana wenye ulemavu wapo wa kila aina na wana uwezo mkubwa, lakini kwa sababu hawashirikishwi, wanashindwa kuonekana, lakini kama wakihitaji kuwashirikisha kwenye programu kama hizi wanaweza kutumia Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu kwenye Mikoa mbalimbali na Wilayani tuko huko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, washirikiane nao ili waweze kupata data kamili ya kuwajumuisha ili kupunguza utegemezi wa kuombaomba, wataomba mpaka lini na wakati wana uwezo wa kujikomboa kimaisha. Mfano mzuri tu Mbeya, kuna wakulima wazuri wenye ulemavu wanalima maharage, wanalima mpunga, lakini kwa sababu hawako kwenye programu hizi jumuishi hawawezi kujua ni namna gani wanaweza kufanya kilimo bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kwa unyenyevu mkubwa kwenye masuala haya ya kilimo na kilimo ni agenda ambayo iko duniani siyo tu Tanzania, kilimo ni kila kitu, kilimo ni maisha; kwa hiyo watu wenye ulemavu pia ni Taifa la kesho kama ambavyo vijana wengine ni Taifa la kesho na wenyewe ni Taifa la kesho na kilimo tunaambiwa kuwa ndiyo uti wa mgongo wa Taifa. Sasa kama kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa tunaachaje kuwajumuisha watu wenye ulemavu na wenyewe wakawa sehemu ya kuchangia pato la Taifa hili? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kwamba sisi kama Tanzania tulikuwa moja ya watu walioridhia Mkataba wa Kimataifa wa Watu wenye Ulemavu na unasema wazi namna gani ya kujumuisha watu wenye ulemavu kwenye shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii. Kwa hiyo, ninaomba Mungu mwezi Juni niweze kupata nafasi ya kwenda kushiriki kwa mara ya kwanza Serikali yetu itakwenda kutoa ripoti ya utekelezaji wa masuala mbalimbali ya watu wenye ulemavu Geneva kama sikosei. Kwa hiyo, nitakwenda kule kwa kifua mbele kwamba Serikali yangu imefanya vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ninatamani kuona miundombinu inarahisishwa kwa watu wenye ulemavu ili waweze kufanya shughuli zao. Kama hapa miundombinu imerahisishwa ndiyo maana ninaweza kuchangia. Kwa hiyo na wao wakiwezeshwa wanaweza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa nafasi na sina maneno mengi na ninadhani nimetumia vizuri muda wangu. Mungu Ibariki Tanzania, Mungu libariki Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kusema haya, niwapongeze Wizara nzima na ninaunga mkono hoja. (Makofi)