Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa nafasi. Tunazungumza Wizara ambayo 80% ya Watanzania wanaitegemea, ni bahati mbaya kwamba muda ni mchache sana, lakini nitaomba nipite kwa harakaharaka baadhi ya maeneo muhimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, wataalam wa Kilimo waliopo kwenye maeneo mbalimbali hasa kwenye kata na wilaya: wenyewe ni wataalam wa kilimo, lakini wachache ambao hata wana mashamba darasa. Shughuli ambazo wanafanya haziendani na kazi ambazo wanafanya, watu wetu wanashindwa kujifunza. Ukimwita Afisa Kilimo aende kwenye shamba unakuta mkulima ni mtaalam kuliko Afisa Kilimo. Inabidi jambo hili Mheshimiwa Waziri alione, watu wafanane na kazi ambayo wanafanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika shule mbalimbali za msingi na sekondari, kuna maeneo ya mashamba ya shule. Mashamba haya, ama yanakodishwa na walimu au walimu wanalima vyakula vyao vya biashara, lakini wazazi wanatakiwa wapeleke vyakula shuleni, kwa nini watoto wasilime mashamba yao ya kitaalam halafu wapate chakula hicho badala ya kupelekewa chakula shuleni kwao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wataalamu wa vyuo hapa hata SUA, wataalam wetu maprofesa wanafundisha kilimo, lakini jioni wao wanaenda kufungua bar badala ya kufungua mashamba darasa. Hili nalo pia ni kitu ambacho kina-discourage wanafunzi, unamfundisha namna ya kulima vizuri, lakini kazi ambayo walimu wao wanafanya sio hiyo ambayo wanawafundisha darasani.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto, Tarime inalima kahawa, hakuna mnada wa pamoja, mnada upo Bukoba, Mbinga, Mbozi na maeneo mengine. Unamtaka mkulima wa kahawa kutoka Tarime asafirishe kahawa apeleke maeneo niliyoyataja, ni changamoto. Ninaomba jambo hili liangaliwe. Bei ni ya chini sana, hakuna hata viwanda vidogo vidogo kukoboa kahawai li waweze kuboresha thamani ya zao hilo katika eneo lile, inasababisha watu kung’oa kahawa na kuanza kulima mahindi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mahindi yenyewe yanalimwa Tarime soko ni Kenya, hata jimbo langu hakuna gulio, hakuna ghala, hakuna wakala wa pembejeo ni changamoto kubwa. Hili ninaomba Mheshimiwa Waziri, anisaidie namna ya kulitatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, Tarime wanalima ndizi, wanalima mihogo, wanalima viazi vitamu, mazao yote yapo Kenya, sasa hii Mheshimiwa Waziri anisaidie bei ya mazao haya yote ni nzuri Kenya kuliko Tanzania. Maana yake Kenya ukipeleka ni watu binafsi wanaweza wakaamua wakanunua, wakasema watakulipa kesho kutwa na wasikulipe na watu wanadhulumiwa wanapata hasara. Hili pia ninategemea pia nipate msaada kwa kufanyiwa kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwa sababu ya muda. Hivi ni lini tutaacha kuagiza ngano kutoka nje ni lini? Ni lini tutaacha kuagiza sukari kutoka nje? Ni lini viwanda vya ndani vitatengeneza juice kwa matunda yaliyopo Tanzania hapa ili watu wetu waweze kupata soko? Haya ni mambo ya muhimu Mheshimiwa Waziri, akiyafanyia kazi atatusaidia kwa maelekezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, ni lazima Serikali ifanye utafiti, ipo imani ambayo tumejengewa sana, mwenzangu amesema hapa asubuhi kwamba pale kwangu, mimi ni Mbunge wa Tarime Vijijini lakini ukienda maduka ya Kenya ukiona jani la mgomba maana yake unauza mirungi, hapa Tanzania hairuhusiwi lakini wale wanapata fedha nyingi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini kusiwe na udhibiti wa mazao yakalimwa kimkakati na kuwekwe sheria kali ikafanya kazi. Kule kwangu hakuna pembejeo kwa maana ya mbegu, mbolea lakini zao la bangi lenyewe halihitaji mbolea, halihitaji mbegu bora, halihitaji mvua, halihitaji kupalilia. Kilo moja ya mahindi pale ni shilingi 650, kipisi ambacho kinalingana na mkono wangu hapa ni shilingi 2,000 na kuendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu ni nini? Kuna matumizi ya bangi ya kitaalam; ganzi wakati wa operesheni, watu wenye shida ya usingizi, mambo ya saratani na vitu vingine. Unaweza kuelekeza wakalima kwa usimamizi, wazazi wanatuambia wamevuta bangi wengine miaka 90 mpaka 100 hawana madhara. Sasa zao hili kwa sababu ni watu wanapata fedha na maeneo mengine linakubalika ni vizuri Serikali ikafanya utafiti, madhara yakadhibitiwa, lakini tukapata fedha katika eneo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, haya ni mambo ambayo yapo, tumeshaaminishwa, lakini tukifanya mchakato wa kitaalam na kisayansi, tukauze nje. Cocaine ni madawa ya kulevya, lakini kiwango kidogo kipo kwenye soda ya kuoga na watu wanakunywa. Cocaine ni madawa ukipatikana ni ajabu kubwa duniani kote, lakini kuna watu wanapata fedha kwa njia hii. Kwa hiyo na sisi hizi ni fursa ambazo tunaweza kuzitumia na kutafuta.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa, Mheshimiwa Waziri, akitaka Watanzania wakulima wanufaike, ni kutafuta masoko ya mazao ambayo watu wanalima. Kama watu watalima kwa nguvu kubwa kwa jasho halafu mazao hayana soko, tutakuwa hatujawasaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na ninaunga mkono hoja ya Comrade mpigaji, Mheshimiwa Chongolo na ndugu yangu Mheshimiwa David Silinde. (Makofi)