Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Joseph Zacharius Kamonga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ludewa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia bajeti hii ya wakulima, ambao ndiyo 80% wamenituma hapa Bungeni. Kwa hiyo ninashukuru sana na nimpongeze sana Mheshimiwa Daniel Chongolo, kwa hotuba yake nzuri sana ambayo imezingatia maeneo mengi ya wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wananchi wa Ludewa wanaiomba sana Serikali iangalie eneo la mbolea, hasa maeneo ya upatikanaji na vilevile gharama. Nitatoa mifano michache hapa wamenipa kazi hiyo, kwa mfano, mbolea aina ya DAP ambayo wanaitumia sana kwenye kilimo cha viazi, maarufu sana kwa kipalila, ilikuwa inauzwa shilingi 74,000, lakini sasa ni shilingi 85,000. Kuna mbolea aina ya SA, wanaitumia sana pia ilikuwa shilingi 52,000, sasa ni shilingi 70,000. Ipo pia CAN ilikuwa shilingi 62,000 sasa ni shilingi 72,000; na kuna urea ilikuwa shilingi 70,000 sasa ni shilingi 78,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wananchi wa Ludewa wanaiomba Serikali ijitahidi kuangalia hii gharama. Wanatambua kwamba kuna changamoto kubwa kule mashariki ya kati ambapo Serikali inaagiza zaidi ya 90% ya mbolea hapa nchini. Kwa hiyo, wanaomba sana iangalie eneo hili hasa upatikanaji wa mbolea.

Mheshimiwa Naibu Spika, msimu wa mvua nyingi kuna baadhi ya mazao yanaathirika sana na tabia za nchi, kwa mfano kama ukungu. Kwa hiyo, sasa hivi kiangazi wanalima sana kilimo cha umwagiliaji hasa eneo la vitunguu na Serikali iliwaahidi wale wananchi wa Lutemaluchi pale Lubonde, itaenda kuwapelekea Mradi wa Kilimo cha Umwagiliaji, kwa hiyo wanakumbusha. Pale Madilu wananchi wanalima sana vipalila, wanahangaika sana wao wenyewe kutafuta vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo wanamwomba sana Mheshimiwa Chongolo, wana imani naye sana kwa sababu yeye mwenyewe pia wanamfahamu ni mkulima. Kwa hiyo, wanaomba awatembelee na kuna ahadi ya Serikali pale Mangalanyene kwenye kilimo cha chai.

Mheshimiwa Naibu Spika, nipongeze Wabunge wote waliozungumzia zao la chai, kungekuwa na muda wa kutosha ningerudia. Kuna ahadi pale ya Serikali ya mradi wa maji pale kwa ajili ya kumwagilia zao la chai. Kwa hiyo, ninaomba Serikali iutekeleza mradi huu pamoja na ule Mradi wa Bonde la Masimavalafu. Serikali imeshawekeza pale zaidi ya shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo fedha hii ili isipotee ni budi sasa kwa Serikali kutenga fedha kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa Mradi huu wa Umwagiliaji, Bonde la Masimavalafu. Ni mradi ambao zaidi ya watu elfu sita watanufaika kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na kuna ardhi kubwa sana pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyozungumzia eneo la mbolea, ninapenda sana kuishauri Serikali kuagiza mbolea 90% katika nchi ni changamoto kubwa sana. Wakati tuna fursa nyingi za kuwa na viwanda hapa hapa nchini. Nitatoa mfano, makaa ya mawe yale yanayopatikana Ludewa kule Mchuchuma, yamefanyiwa utafiti, yameonekana yana ile Methanol kwa wingi, yana Nitrogen nyingi ambayo wenzetu kule mashariki ya kati wanatumia katika kujenga viwanda vya mbolea. Kwa hiyo na sisi tuna potential hiyo ya kujenga viwanda vya mbolea hapa hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuvishirikishe vilevile Vyuo Vikuu vya Kilimo kama Sokoine na vyuo vingine na taasisi mbalimbali za kilimo kufanya tafiti, kwa nini wakulima wetu kuna aina fulani ya mbolea hawapendi sana kuzitumia ili tuone hizo mbolea zinakosa nini ili tuweze kuongeza. Kwa sababu mpaka wafanyabiashara sasa wanalazimika kufumua ile mifuko ya mbolea hizi zetu ambazo wakulima hawajazizoea sana, wanajaza mbolea, yaani wanaweka mbolea kwenye mifuko ya nje, lakini mbolea inayopatikana hapa hapa, wakulima wakinunua wanaenda kuona matokeo tofauti.

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze Serikali ilianza kuchukua hatua kwa wale ambao walikuwa wanauza mbolea fake, niipongeze sana Serikali katika eneo hilo na niwasihi sana waendelee kuchukua hatua kwa sababu mwananchi akinunua mbegu fake au mbolea fake anapata hasara kubwa na anakata tamaa kuendelea na shughuli za kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, eneo hili liweze kuangaliwa, tujenge viwanda vyetu vya mbolea na zile ambazo zinazalishwa tayari, tupongeze ili kulinda ajira za ndani na viwanda vya ndani. Tuangalie zile zinapungua kitu gani ili tuweze kushirikiana na wenye viwanda kuboresha ili wakulima waweze kuziamini na kuweza kuzitumia kwenye shughuli za kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo ningependa kulisemea ni eneo la barabara za maeneo ya kilimo na uzalishaji mkubwa. Kwa hiyo, Wizara hii ya Kilimo pamoja na kushughulika na mambo ya sera za kilimo na sheria na vitu vingine washirikiane pia na TARURA kuboresha barabara za vijijini ambako ni maeneo ya uzalishaji mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, muda umenitupa mkono, ninaunga mkono hoja na ninashukuru sana kwa kupewa nafasi. (Makofi)