Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Asha Juma Feruz

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. ASHA J. FERUZ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika Wizara hii ya Kilimo. Awali ya yote ninapenda kuchukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, hakika mama huyu amefanya mapinduzi makubwa sana katika sekta ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue pia fursa hii kuwapongeza Waziri wa Kilimo, Naibu Waziri wa Kilimo, Katibu Mkuu wa Wizara hii pamoja na watendaji wote kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuhakikisha kuwa tunapata pembejeo, tunapata mbegu na tafiti zinafanyika, utafutaji wa masoko unafanyika, viuatilifu vinapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sasa nijielekeze katika mchango wangu leo. Mchango wangu wa kwanza nitauelekeza katika eneo la mikopo ya wanawake na vijana. Ninaomba Wizara hii sasa ichukue hatua za makusudi katika mikopo ya vijana na wanawake kupitia ule Mfuko wa AGITF.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sana Wizara hii iangalie kwa jicho la kipekee vijana wetu wanaohitimu katika vyuo vikuu ambao wamesomea kozi za kilimo. Kama tunaweza kumpatia kijana huyu mkopo wa elimu ya juu kabla hana hata haya maarifa ya kilimo, basi kijana huyu niombe aangaliwe kwa jicho la tatu pale anapohitimu masomo yake katika course za kilimo anapokwenda kuomba mkopo katika Benki ya Kilimo ama taasisi zinazotoa mikopo hiyo, akopeshwe kupitia cheti chake. Kwa sababu tunaamini kijana huyu amepata maarifa na anaweza kwenda kuya-implement na akaleta tija. Kwanza itachochea ajira kwa vijana na pili tutapata uhakika wa wataalam ambao wana-practice kile ambacho wamejifunza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu wa pili niuelekeze katika mazao ya horticulture. Mazao haya tumekuwa tukipoteza 30% mpaka 40% katika post-harvest losses. Kwa hiyo, ninaiomba Wizara hii iangalie umuhimu mkubwa wa kuandaa cold rooms katika maeneo ya airport na bandarini. Mkulima au mwekezaji anatumia takriban dola 2,500 katika shipment anapokwenda kusafirisha mazao haya. Umuhimu wa cold room ni mkubwa, mazao ya mbogamboga na matunda tunapoteza pesa nyingi katika maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niishauri Serikali yangu tuangalie katika Bandari ya Mtwara, Tanga, Dar es Salaam, tuzifanye bandari hizi kuwa ni sehemu kubwa ya kujenga hizi cold room au zile warehouse za mazao ili ziweze kufanya usafirishaji mkubwa. Pia, niombe katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, KIA, maeneo ya Tabora na Mwanza, tunaweza tukawekeza hizi cold rooms na zikatusaidia kuokoa pesa nyingi ambazo tunazipoteza kwa kupitia Bandari ya Mtwara.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu wa tatu katika Wizara hii, ninamwomba Mheshimiwa Waziri, tunauza mazao mengi yakiwa ghafi. Tuwekeze katika viwanda vidogo, vya kati na vikubwa ili tuuze end user products. Tukifanya hivyo tutakuwa tumeweka wigo mkubwa wa upatikanaji wa ajira kwa vijana, kwa jamii zetu. Hata yule mkulima na yeye ataona tija ya kile anachokilima kwa maana ya kwamba zao limelimwa hapa, limekuwa processed hapa, pesa za kigeni tutazipata, tutainua pato la Taifa na uchumi wa wananchi wetu utakua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ninaomba nitumie fursa hii kuunga mkono bajeti hii iliyoko mezani na niwatakie kila la heri watekelezaji. Hakika haya yote ambayo wametuletea yakitekelezeka vizuri wananchi wetu watafurahia na kuona kuwa kilimo kwao ni option ya kwanza, siyo ya mwisho baada ya kukosa option zote. Haya yote ambayo nimeyaongea yaende sambamba na uboreshaji wa miundombinu ya barabara. Ahsante sana.