Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nsimbo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa ninaomba nimshukuru Mungu ambaye ametupa uzima na uhai muda huu tuko mahali hapa. Ninaomba nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa ajili ya sekta ya kilimo, Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri, Katibu Mkuu, watendaji wote wa sekta ya kilimo, ninaomba niwapongeze sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa jimbo langu ni wakulima wa tumbaku. Zao la tumbaku limeporomoka kwa kiwango kikubwa sana na mwaka huu wananchi walihamasika walilima sana kutokana na miaka miwili ya nyuma kwa sababu walipata fursa kubwa ya mapato makubwa. Mwaka huu wananchi wakakopa, wakalima, matokeo yake pembejeo imekuwa juu, zao limeshuka kwa kiwango kikubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ajili Waziri ni msikivu, tunaomba watuangalie kwa jicho la tofauti kupitia wananchi kwa sababu wananchi wamekopa, pesa hawana, matokeo yake yatakuwa ni magumu sana katika zao hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba tumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuleta kampuni mbalimbali ambayo ziliongeza mapato makubwa kwenye zao la tumbaku. Sasa zao la tumbaku limeporomoka kupitia hali ya uhalisia wetu wa dunia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba tuishauri Serikali, sasa hivi ni kipindi cha kujenga kiwanda katika maeneo yetu. Kama kiwanda kikijengwa Tabora, kiwanda cha mbolea haya yote yatapunguza ile kero ambayo iliyotokea mwaka huu. Tunaomba sana kuishauri Serikali tujenge Kiwanda cha Mbolea katika Mkoa wa Tabora. Maana yake Tabora itatulisha Katavi, Kigoma na Shinyanga, wote tutachukulia mbolea Tabora. Tunaiomba sana Serikali ituangalie kwa jicho la tofauti ili wananchi wetu waweze kupata unafuu kidogo kwa ajili ya pembejeo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika jimbo langu nina skimu za umwagiliaji. Skimu kama nne zote hazijafanya kazi, wakandarasi hawapo site ina maana kuwa hawajalipwa. Ninaomba Skimu ya Usense, Skimu ya Itenka, Ugala pamoja na Uwila. Skimu zote hazina mkandarasi kwa ajili ya uendelezo wa miradi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kwa sababu kilimo cha umwagiliaji ndiyo uti wa mgongo wa Mtanzania. Tukiendeleza kilimo cha umwagiliaji tutapata manufaa makubwa kwa Watanzania. Ninaomba mwaka huu wa fedha wakandarasi warudi site ili kilimo hiki cha umwagiliaji kiweze kusonga mbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimpongeze Waziri kwa kusimamia, sasa hivi tunaona uboreshaji wa AMCOS zetu pamoja na Benki ya Kilimo inafanya kazi vizuri, inakopesha, wakulima wanafurahi. Hata sisi Benki ya Kilimo ilikuwa haitufikii, lakini sasa hivi Benki ya Kilimo inatufikia. Mheshimiwa Waziri tunaomba tukupongeze sana, lakini uongeze juhudi kwa sababu kilimo ndiyo uti wa mgongo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mazao yanayolimwa katika Jimbo langu la Nsimbo, pamba ninalima. Ninaona safari hii kidogo zao la pamba lina unafuu kwa bei. Ninaomba nikupongeze Mheshimiwa Waziri wananchi wangu wanaolima pamba watanufaika, lakini bado kuna zao la ufuta bado halijakaa vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, mazao yote hayo ni mazao ya kibiashara wananchi wanalima, tunaomba basi ili waweze kufanikiwa tuwekewe mazingira bora na mazuri kwa ajili ya AMCOS zetu ili waweze kufanya kazi vizuri na mafanikio yawe makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nishukuru sana ninaomba kwenye zao la tumbaku tuwaangalie wananchi kwa jicho la tofauti kwa sababu wameporomoka. Sasa hivi wamekuwa na wasiwasi kwa sababu hawajui hatima ya mwakani wataingiaje katika kilimo cha tumbaku.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niunge mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana. (Makofi)