Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mtwara Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ARIF S. PREMJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza nichukue fursa hii kuwapongeza sana Wizara ya Kilimo hususan Mheshimiwa Rais. Ni siku mbili tu zimepita jimbo la Mtwara vijijini tayari tumeshaanza kupokea sulphur na viuatilifu vinaanza kugawiwa kwenye jimbo letu kwa wakulima pia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaongelea kilimo na kwenye kilimo ardhi inahitajika, maji yanahitajika, mbolea inahitajika, hali ya hewa iwe nzuri, lakini bei ya sokoni pia iwe njema ndiyo inaweza ikaleta tija kwa mkulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, factor mbili, hali ya hewa na bei, vitu hivi havipo kwenye udhibiti mzuri wa Serikali. Ninasema hivyo kwa nini? Hakuna mtu ambaye anaweza aka-predict bei ya sokoni, inategemeana na demand na supply na soko la dunia pia. Pia, hali ya hewa hakuna mtu ambaye anaweza akajua kesho kuna ukame au kuna mafuriko na vitu hivi viwili ndiyo vinapelekea wakati mwingine mkulima anapata hasara.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nitoe ushauri na ushauri wangu wa kwanza ni Crop Revenue Insurance. Ni bima ya mapato yanayotokana na mavuno ya mazao. Ni lazima tujikite hapo, hiyo ndiyo bima ya kwanza ili kudhibiti kwamba panapotokea na mfumuko au bei haijawa sawa basi mkulima anaweza akalindwa na hiyo bima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna bima nyingine inaitwa Weather Index Insurance, ni bima ya mazao kulingana na hali ya hewa. Dunia ya sasa hivi imebadilika na wakulima wengi vitu hivi hawavitambui. Kwa hiyo, nishauri Serikali yetu ijikite sana kwenye kutoa elimu hiyo, lakini pia tuangalie jinsi ya kuweka mifumo imara ya kuwasaidia wakulima hao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iliyoko madarakani ni ya Chama Cha Mapinduzi na ukiangalia nembo ya Chama Cha Mapinduzi utaona kuna jembe na nyundo. Jembe lile ni wakulima na waasisi wa chama hiki cha kwetu ni wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna ujumbe ambao wakulima wa Mtwara Vijijini wamenituma na ninaomba kwa unyenyekevu mkubwa nimpatie Mheshimiwa Waziri. Moja, wanasema tozo zilizopo kwenye zao la korosho shilingi 469 zipitiwe tena, ziboreshwe au zirekebishwe kwa kuwa wakati mwingine wanahisi zinapelekea kufanya bei isiwe stable au kushuka. Hilo la kwanza. La pili, kwenye uwiano wa pembejeo, wanapewa robo kilo (gramu 250) kwa kila mti mmoja wa korosho na hilo pia wanaomba waboreshewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, kuna sheria ya manunuzi ya 2023 na PPRA mara nyingi wanasema kwamba 30% iende kwenye makundi maalum. Vijana wa Mtwara, walemavu wa Mtwara, akina dada zangu wa Mtwara wameniagiza hili na mama zangu na shangazi zangu pia, kwamba inapotokea zile tender za ku-supply sulphur, magunia na viuatilifu, basi na wenyewe wapewe kipaumbele kwa kuwa sasa hivi tunachoki-advocate ni kwamba vijana wajikite, tuwapatie fursa na hiyo ni fursa mojawapo. Kwa hiyo, ninaomba sana hilo tulizingatie.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia wengi wameongea, mimi ninatia msisitizo tu. Sukari, ngano, mafuta ya kupikia; tukichukua hivi vitu vyote ni kuanzia trilioni 2.5 mpaka 3.2 ndio tunaagiza. Kwa hiyo tuliangalie na hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ajili ya faida ya muda, ninaunga mkono hoja. (Makofi)