Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon Abubakar Damian Asenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilombero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana kwa nafasi hii ya kupata dakika tano hizi ambazo nitachangia Wizara yetu ya Kilimo. Kama ambavyo Wabunge wenzangu wamesema mara kadhaa kuhusu umuhimu wa kilimo katika nchi yetu na kadhalika Mkoa wa Morogoro tunasema mara zote ni Ghala la Taifa. Tunaongoza katika nchi yetu katika kilimo cha miwa pamoja na mpunga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kusimama hapa kwa kusema ninaanza na mambo ya kushukuru, lakini nimesimama kwa upole kidogo kutokana na yale mambo ambayo yanaendelea kwa wakulima wetu wa miwa ya sukari, nikipata muda huko nitaelezea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama walivyosema wenzangu Wabunge, tuna imani kubwa na wewe Mheshimiwa Waziri wetu, Mheshimiwa Godfrey Chongolo kwa sababu wewe ndiyo mtunzi wa ilani na umepewa kazi sasa ya kuisimamia ilani. Kama ningelisema kwa Kindamba, Kipogoro ama Kisukuma basi ningesema: “A square peg in a square hole is in safe hands.” Kwa hiyo, sisi tupo salama mikononi mwako. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Waziri anasoma hotuba nimekusikia kwamba Mkoa wa Morogoro tunapata kituo kikubwa cha kibaolojia, tunashukuru sana sana. Tunashukuru sana nimeona kwamba tunapata miradi mikubwa ya umwagiliaji ambao upembuzi yakinifu umekamilika kwa 100%.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Mradi wa Umwagiliaji tuliopata wa Ifakara - Idete hekta 53,000 unaofanywa na SABA Engineering ambao umekamilika kwa 100% upembuzi yakinifu utakaokuwa unajengwa bwawa la maji na pamoja na skimu. Kuna Bonde la Kilombero hekta 19,000 wanafanya wao SABA Engineering umefika 95%, tutakuwa na bwawa pamoja na skimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna Mradi wa Mang’ula Youth Group, tuna Maki - Magombera, tuna Kisawasawa, Kiberege, Mkangawalo na Signal. Hiyo yote ikikamilika itatusaidia kwa kiasi kikubwa sana kuendelea kuufanya Mkoa wa Morogoro kuendelea kuwa Ghala la Taifa na kupunguza athari kubwa za mafuriko ambazo tunazipata Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunashukuru wanafanya pia kilimo cha umwagiliaji katika maeneo ambayo wanakwenda kuchimba visima. Sisi Kilombero maji tunayo yanazidi mpaka yanamwagika kwa wananchi. Hapa ninavyozungumza kuna wananchi zaidi ya 200 wako pale Shule ya Msingi Lipangalala kutokana na mafuriko kuwa katika majumba yao. Sasa endapo tutapata miradi hiyo ya umwagiliaji ambayo inajenga mabwawa kukinga Mto Lumemo itatusaidia sana kupunguza mafuriko kwa kiasi kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri, nilikwenda kukaa hapo kwake na wapiga picha wakapiga picha, nilikuwa na jambo langu nilimpelekea. Kwa heshima kubwa na unyenyekevu mkubwa ninataka kushukuru jambo lile Mheshimiwa Waziri limekamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Katibu Mkuu amenipigia simu ameniita hapa; Katibu Mkuu wa Wizara yake na Mkurugenzi wa TARI ananiambia ule mgogoro wa ardhi kati ya wananchi wa Kata ya Lumemo na TARI walikuwa wanatengeneza kituo cha mbegu. Tuna hekta 98 zilikuwa na mgogoro pale zinazuia TARI kuendeleza kile kitalu cha mbegu umekamilika. Kwamba watasaidia yale ambayo wananchi walikuwa wanayataka angalau wapate malipo kidogo yasaidie kutafuta ardhi nyingine ili wananchi waachie ardhi ile ya TARI. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilifanya ziara pale wananchi waliongea kwa hasira kubwa sana kwamba viongozi mnakuja hapa mnapiga picha mnatuma kwenye mitandao hamtatulii kero yetu. Ninataka nimhakikishie Mheshimiwa, Katibu Mkuu wake ameshanisaidia suala hili na ameniambia limekamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninataka kuzungumzia miwa. Bunge lililopita nilisimama hapa kidete kuomba kiwanda kipya cha sukari kwa sababu miwa ya wananchi ilikuwa inabaki. Sasa kiwanda kipya tumepata, tuna changamoto zinazotokana na hicho kiwanda kipya kuwekezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi kiwanda hicho kime-test miwa ya wakulima lakini wakulima wale hawajalipwa vizuri katika testing ya miwa hiyo. Wanasema walipeleka miwa ya majaribio kiwanda kimesimama na ni miwa walipata hasara wanaiomba Serikali iwakumbuke. Wakulima wa miwa wanasema sasa hivi wanang’oa miwa wanapanda mpunga kwa sababu mpunga unalipa zaidi kuliko miwa. Endapo hilo litaachwa kwa vyovyote vile uwekezaji wa shilingi bilioni 700 za kiwanda kipya hautakuwa na mafanikio yoyote ambayo tulikuwa tumeyaomba huko nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, chonde chonde ninaiomba Serikali, Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri ambao wako hapa; ninamwomba Mheshimiwa Waziri afanye ziara, aende akakutane na wakulima wa miwa wa Kilombero. Sisi tutamwandalia mkutano mzuri azungumze na vyama vile na wakulima wale wasikie.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna matatizo wanazungumza kabla ya sukari kuingizwa nchini ambayo mwekezaji amekuwa ni kisingizio chake, lakini kuna matatizo mengine yametokana na sukari kuingizwa nchini. Wakulima wakati wote wanalalamikia kupunjwa mzani.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba mamlaka ya mizani iende pale iweke kiti ili wakulima wale wanapouza miwa yao ile sucrose (utamu) wasilalamike kwamba wanapunjwa. Wakulima wanasema wameingia mkataba na kiwanda, muwa unaoungua, moto bahati mbaya unavunwa wanakata 10%, lakini Serikali imetoa katazo kwamba miwa inaoungua kwa bahati mbaya inatupwa. Watu wamepata hasara mpaka za shilingi milioni 500 ndiyo huku tunaposema kuna umuhimu wa kuwa na bima ya kilimo na bima ya mazao ili kuwasaidia wananchi hawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu dakika ni tano, anisaidie katika Bunge hili kama atapata nafasi aandae ziara nzuri pale, azungumze na wakulima awasikie wenyewe uso kwa uso ili tuweze kuwasaidia wakulima wetu hawa kwa kiasi kikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na muda ninakushukuru sana. (Makofi)