Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Eng. Ramadhani Hamza Singano

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bumbuli

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. RAMADHANI H. SINGANO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa fursa hii na kwa dhati ya moyo wangu nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema. Nipate fursa pia ya kumshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mama yetu kipenzi mama Samia Suluhu Hassan. Pia, niipongeze Wizara husika, Wizara ya Kilimo kwa kuwa na hotuba nzuri ambayo ipo mbele yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Wanabumbuli nianze kuiunga mkono hoja. Baada ya hapo niende moja kwa moja kwenye zao la chai kule Bumbuli. Hili ni zao la kihistoria, zao la kimkakati na zao la kibiashara. Kata 14 kati ya 18 zinategemea zao hili. Hata hivyo, kuna changamoto ambazo ninaziwasilisha moja kwa moja kwa Wizara ya Kilimo kwa sababu wanazijua nyingi, nitataja hizi chache.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni uwezo mdogo wa kiwanda, kinatumia laini moja mpaka sasahivi, kiasi cha kukatisha tamaa wakulima wa zao la chai. Basi ninaomba iongezeke laini ya pili na ya tatu, ili kuongeza tija katika zao hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, madai na madeni; wakati kiwanda hiki kiliposimama, kabla Serikali haijakitwaa yapo madeni; madai ya watumishi zaidi ya shilingi 800,000,000, lakini na wakulima pia, walikuwa na madai yao, shilingi 12,000,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto nyingine kubwa kwa kiwanda hiki ni pembejeo, hasa mbolea. Kwa bahati mbaya kule Bumbuli, wakala ni mmoja tu, ambaye anashindwa kuweza kuwafikia wakulima wa chai, lakini wakulima wanalalamika bei ndogo, shilingi 366 kwa kilo, ni kiwango kidogo sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo changamoto pia ya barabara kwa sababu, kata 14 kuziunga katika jimbo ambalo lina milima na mabonde ni changamoto kubwa. Kingine ni ukosefu wa mitaji na uwekezaji wa kutosha. Pia, lipo zao la mkonge katika Kata za Tambarare, Kata za Kwemkomole Milingano, Mahezanguu pamoja na Usambara.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa changamoto kubwa ni mbolea na mbegu bora. Wakulima wengi hutumia mbegu ambazo zinachipua pembezoni mwa mashina ambazo siyo bora na hata umri wake ni mdogo. Sasa kwa sababu, kuna ile mbinu ya kisayansi ya tissue culture na tunayo TARI ya Mlingano, basi ipate maelekezo ili iweze kutusaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaenda kwenye eneo nyeti kidogo, nalo ni kilimo cha umwagiliaji, lakini ninajikita zaidi kwenye kilimo cha umwagiliaji wa skimu ndogo ndogo za mbogamboga. Hii ni lazima kulingana na sayari yetu kukumbwa na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi. Mvua haitabiriki, lazima tuwe na benki ya maji na haiwezi kupatikana, isipokuwa kwenye mabwawa. Tija gani itapatikana kwenye maji haya?

Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima tuwashauri wenzetu wa kilimo, tufike mahali kuwe kuna user efficient irrigation kwa maana kwamba, tutumie mbinu za maji kidogo, ambayo tunaita drip irrigation. Hii itapunguza gharama ya umwagiliaji, itapunguza hata changamoto ya magonjwa yanayotokana na unyevu wa maji, lakini pia, itapunguza changamoto zingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima tuwashauri kwamba, kilimo kiwe kilimo hifadhi; yaani kilimo ambacho kinatumia mulching, kule uswahilini tunaita matandazio, lakini ina-cover crop au mimea funiko. Kuwe na uchaguzi wa mazao ambayo yanaweza yakahimili mabadiliko ya tabianchi kwa sababu, Wizara ya Kilimo ni Wizara ya research.

Mheshimiwa Naibu Spika, lazima kuwe na usimamizi madhubuti wa zile water users groups, zisiposimamiwa vizuri mwisho ni migogoro. Ninakumbuka kesi moja kule Moshi, wakulima na kiwanda cha miwa, ilikuwa ni changamoto kubwa kwa hiyo, lazima wasimamiwe vizuri, lakini ni nini faida ya kilimo hiki cha mbogamboga?

Mheshimiwa Naibu Spika, tutaboresha lishe. Ikiwa mbogamboga zinapatikana kwa mwaka mzima, maana yake ni tunaenda kuboresha afya ya jamii. Tutapunguza utegemezi wa kutumia mvua. Tukiongeza mavuno na kipato, maana yake tutakuwa na mbogamboga kwa wingi zaidi, lakini pia, tukiwa tunategemea…

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa, muda wako umekwisha.

MHE. RAMANDANI H. SINGANO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninawashukuru sana Wizara ya Kilimo, lakini ninaunga tena mkono hoja. (Makofi)