Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Kenneth Ernest Nollo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bahi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninachukua nafasi hii kumpongeza Waziri wa Kilimo kwa kuaminiwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kushika nafasi hiyo. Ninampongeza kwa dhati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna ambavyo, bajeti hii ya kilimo amekuwa akiiongezea fedha kila mwaka hata tumefika katika kiwango hiki kikubwa cha karibu shilingi 1,000,000,000,000. Haya ni mapinduzi makubwa na ukiangalia katika fedha hizo za maendeleo, fedha nyingi zimeenda kwenye suala zima la umwagiliaji kwa hiyo, haya ni mapinduzi makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa zaidi ninaomba Wizara ya Fedha iweze kuongeza nguvu ya kutafuta fedha na ku-finance miradi hii ambayo Wizara ya Kilimo inaitekeleza ili kuweza kufikia malengo. Vilevile, ninachukua nafasi hii kuishukuru sana Serikali, katika Wilaya yangu ya Bahi nimepata mradi wa shilingi 5,600,000,000 pale katika Skimu ya Kongogo. Jambo hili ni zuri na mradi ule ni mkubwa. Hoja yangu tu ni kwamba, wenzetu wa umwagiliaji waweke umadhubuti zaidi mradi ule ambao kwa sasa upo karibu 46% uweze kumalizika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri Chongolo, alipokuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, alifanya ziara pale Bahi, mwaka 2023 na akaelekeza kwamba, Skimu ya Umwagiliaji ya Bahi ikarabatiwe. Ninavyozungumza leo ukarabati wa scheme ile umefanyika. Tumepata karibu shilingi 3,600,000,000 na bajeti yake ni shilingi 5,000,000,000, kwa hiyo, ukarabati ule unaendelea. Kwenye hilo ndugu yangu Mheshimiwa Chongolo, ninamshukuru sana, ziara yake ilizaa matunda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ambacho ninataka kusisitiza ni kwamba, ukarabati huu ambao tumeufanya bado hatujaumalizia, skimu zingine zinaendelea itabidi tukarabati. Bado kuna shida ya miundombinu ya barabara kwenye mashamba na zile skimu, tunaomba Serikali iweze kumalizia kile kiwango kilichobaki, ili tuweze kukamilisha ukarabati huo. Ninaishukuru Serikali imefanya usanifu katika Mabonde ya Mkakatika, Mtitaa na pale Lukali, ninaomba kazi ikamilike ili tuanze sasa kazi ya ujenzi wa skimu, kwenye skimu tatu nilizozitaja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaishukuru Serikali, mwezi Machi nilipata janga la kweleakwelea, wale ndege, katika Vijiji vya Mwitikila, pale Lukali, Ibiwa na maeneo ya Tarafa ya Mndemu. Ninaishukuru Serikali imeleta ndege ile ya kupulizia wale ndege, kweleakwelea, imekuja mara mbili. Ilikuja mara ya kwanza kidogo hawakufa, imekuja mara ya pili, kidogo tumepata ahueni.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka tu kusema, ninamshukuru Profesa Ndunguru kwamba, tumepata ndege ambayo Serikali imeinunua kwa hiyo, accuracy kubwa iweze kuangaliwa katika dawa zinazopuliziwa, ili wakienda kupulizia tuweze kuhakikisha tunawaangamiza wale ndege.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine niongee habari ya kilimo cha ngano, wenzangu wengi wamesema. Kwa kweli, katika jambo hili Ndugu yangu Mheshimiwa Chongolo, kwenye kilimo kuna mambo mengi, lakini aondoke na suala la ngano. Kila mwaka tunatumia fedha karibu dola za Kimarekani 377,000,000 ambazo ni karibu shilingi 900,000,000,000 au all most 1,000,000,000,000, tunaagiza ngano kutoka nje ya nchi. Mashamba tunayo katika maeneo mbalimbali, ninachoomba ni Serikali iweke incentives kwa mashine zile kubwa zinazokuja kwenye kilimo cha ngano, ili tuweze kulima ngano yetu hapa nchini na ikiwezekana tuweze kuuza katika maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili tumefanya kwenye sukari, kwa sasa nchi yetu inajitosheleza kwa kuzalisha sukari ndani ya nchi. Kwa hiyo, jambo hilo tulifanye. Mheshimiwa Waziri, Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikuja kwenye kampeni Bahi, tarehe 9/9, aliahidi kwamba, kupitia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, na jambo hilo lipo, kwamba, maji ya Ziwa Victoria yatakuja mpaka Kanda ya Kati, maji ambayo yanakuja kwa ajili ya umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba ahadi ya jambo hili la kihistoria waweze kulitekeleza, ili tuweze kupata maji, kwa ajili ya umwagiliaji. Mambo haya yataleta mapinduzi makubwa katika Mikoa yetu ya Kanda ya Kati.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)