Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipatia nafasi ili niweze kutoa mchango wangu kwenye Wizara yetu ya Kilimo na bila ya kupoteza muda, ninaomba nijielekeze moja kwa moja kwenye hoja. Kwanza ninawapongeza Wizara ya Kilimo, kwa maana ya Mheshimiwa Waziri na timu yako yote, lakini hoja yangu ya kwanza ni suala zima la mbegu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ndani ya Taifa letu tumekuwa hatuna mbegu bora, lakini zinapatikana kwa bei ghali, hususan mbegu ya mahindi, alizeti na zingine. Sisi Mkoa wa Dodoma, alizeti, mahindi, mbaazi na ufuta hizo ndiyo mbegu ambazo tunazitumia kwa wingi. Mbegu hizi zimekuwa ni ghali, lakini nyingi hazimpi tija mkulima. Tumwombe Mheshimiwa Waziri, kupitia taasisi yake ya mbegu, waende wakawasaidie wakulima waweze kupata mbegu iliyo bora na inayopatikana kwa bei rahisi, watakayoweza kuimudu kwenye maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuzungumzia zao la alizeti. Mheshimiwa Waziri, nchi yetu imekuwa ikitumia gharama kubwa sana kuagiza mafuta nje. Hili jambo tumekuwa tukilisema na nimekuwa ninasema kila mwaka wa bajeti, sasa ni takribani mwaka wa 11. Tunazungumzia suala la kujiimarisha kwa mbegu za mafuta ndani ya nchi yetu, ili tuweze kuondokana na uagizaji wa mafuta nje ya nchi. Mheshimiwa Waziri tunaomba watusaidie.
Mheshimiwa Naibu Spika, tupate mbegu nzuri itakayoweza kuleta tija kwa wakulima wa alizeti, lakini itakayoweza kuleta tija kwa Taifa kwa kupata mafuta ya kujitosheleza ndani ya Taifa letu. Fedha tutakazozibakisha kwenye kuagiza mafuta nje, zitumike kwenye mambo mengine ndani ya Taifa letu. Ardhi tunayo, watu wapo, nini kinachoshindikana kwenye suala zima la kutupatia mbegu iliyo bora yenye tija kwa wakulima, ili tuweze kuondokana na adha kubwa tunayoipata ya mafuta ndani ya Taifa letu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo langu lingine ambalo ninatamani kulisema ni suala zima la Mfuko wa Pembejeo. Mfuko wa Pembejeo upo, kwa ajili ya kuwasaidia wakulima, kwa ajili ya kuwapatia pembejeo za kilimo pamoja na mikopo, kwa ajili ya kilimo, lakini kuna changamoto moja kwenye Mfuko huu, wameamua kufanya kazi pamoja na Benki yetu ya Ushirika.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkulima anahitaji power tiler lenye thamani ya shilingi 15,000,000 anaambiwa apeleke hati ya nyumba ama hati ya shamba. Hati za kimila coop bank nao hawazitaki, sasa ninataka watusaidie, uwepo wa Benki ya Ushirika vs Mfuko wetu wa Pembejeo…
NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, ninaomba tujadili kwa sauti ya chini, Mbunge anachangia. Ninaomba tujadili mambo mengine muhimu kwa sauti ya chini.
Mheshimiwa endelea.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru. Hizo dakika zangu mbili utanijazia.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninasema uwepo wa Benki yetu ya Ushirika vs Mfuko wetu wa Pembejeo ambao wameamua kufanya kazi kwa pamoja. Ni kwa nini Benki ya Ushirika inakataa hati za kimila kwenye benki zao, kwa ajili ya wananchi wetu kupata mikopo?
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, ni kwenye suala zima la Mfuko wa Pembejeo. Wamesema wanatoa mikopo ya aina mbalimbali ikiwemo uwezeshwaji wa mbegu, suala la palizi, suala la kilimo na ufyekaji wa mashamba; hivi vitu havifanyiki. Tunaomba, Mheshimiwa Waziri, kama kweli nia na dhamira ya Wizara yake kupitia Mfuko huu wa Pembejeo wa Taifa ni kuwasaidia wakulima wadogo wa kule chini, maneno wanayosema yaendane na vitendo, ili wananchi wetu waweze kuiamini Serikali yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo langu lingine ni suala la Vyama vya Ushirika na Benki yao tena ya Ushirika. Mheshimiwa Waziri, kuna Sheria inayosema kwamba, Chama cha Ushirika kikiundwa kinatakiwa kikae miaka mitatu, ndiyo kikopeshwe. Sasa ninajaribu kujiuliza, hivi kwenye suala zima la hii Benki ya Ushirika, madhumuni na malengo yake ni nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, kama CRDB na NMB wana hayo masharti, leo tena Benki ya Ushirika, ambayo tunategemea hawa wananchi wetu ambao tunawaaambia wajiunge kwenye vyama waweze kupata fursa ya kuwezeshwa kwa urahisi, kunakuwa na hivyo vikwazo! Mheshimiwa Waziri tunaomba, suala la Vyama vyetu vya Ushirika, kama nia na uwepo wa Benki ya Ushirika ni kuwasaidia wanaushirika, tunaomba wasaidiwe bila vikwazo, ili kuwaondolea adha wanayoipata kwenye huduma zingine za kifedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, zile dakika zangu mbili ulizonituliza, ninaomba nimalizie.
NAIBU SPIKA: Malizia Mheshimiwa.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru. Jambo langu lingine ni, suala la stakabadhi ghalani. Ni jambo jema, hatuna shida nalo, lakini ninaomba niseme changamoto kadhaa ambazo wanatakiwa ku-share wenzetu wa Kilimo, Wizara ya Viwanda na Wizara ya Fedha, ili waweze kuzitatua na hatimaye mfumo wetu uweze kufanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza kwenye changamoto ya Mfumo wa Stakabadhi Ghalani ni uwepo wa maghala machache. Tunahitaji maghala mengi, ili yaweze kuwasaidia wakulima wetu; moja, kupunguza gharama ya usafirishaji wa mazao, lakini pili, kumsaidia mkulima huyu kutopoteza mazao anaposafirisha kwa umbali mrefu. Kwenye hilo tunaomba pia, wakati wanajipanga, watusaidie kuwa na maghala yanayotembea, kwa ajili ya kuwasaidia wakulima wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, bei…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Kunti.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, pili ni ulipwaji kwa wakati ili kuweza kuwaondoa wananchi wetu kwenye hizo changamoto. Ninakushukuru kwa muda wako. Ahsante sana na Mungu akubariki. (Makofi)