Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Eng. Amosy William Maganga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kwanza nichukue nafasi hii kukushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuwa mmoja wa wachangiaji katika Wizara hii muhimu sana Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna mashaka na wala hakuna wasiwasi wowote kwamba ni kweli tunapokwenda ni kuzuri na tukizingatia kwamba kweli Wizara yetu ya Kilimo imepata watu shupavu ambao tunaona kwa kweli wanatupeleka kule ambako Watanzania tunakutaka.

Mheshimiwa Naibu Waziri, hivyo nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, lakini nimpongeze sana Naibu Waziri wa Kilimo, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu pamoja na Watendaji wote kwa kazi nzuri wanazozifanya. Kazi wanayoifanya inaonekana Watanzania tunaiona, wanafanya kazi mbalimbali hasa tunaona wanavyohangaika katika utafutaji wa masoko, tunawapongeza sana. Sisi wakulima wa tumbaku soko letu liliyumba, lakini chini ya uongozi wa Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan tunaona masoko ya tumbaku yanapatikana, hivyo tunawapongeza sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaona kazi nzuri za tafiti wanazofanya, wanafanya tafiti kwenye mbegu, viuatilifu pia kwenye afya ya udongo. Niseme kwamba waongeze kasi katika afya ya udongo. Tuna matatizo makubwa sana katika maeneo mbalimbali ya nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kule kwetu Sikonge Waziri ni vigumu sana sasa hivi kupata angalau magunia 10 ya mahindi kwa ekari moja ni kazi kubwa kwelikweli. Pamoja na kwamba utatumia input zote, utatumia mbolea zote, mbolea ya kupandia, mbolea ya kukuzia pamoja na kuzalishia na taratibu zote za kilimo umezifuata, lakini imekuwa changamoto kwelikweli kupata hata gunia 10. Tunaomba hili kwa kweli lifanyiwe kazi kubwa ili kusudi suluhu ya afya ya udongo iweze kupatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pongezi zote hizi kwa Wizara ya Kilimo, lakini nilete sauti ya wakulima wa tumbaku hapa Tanzania hususani wakulima wa zao la tumbaku Wilayani Sikonge. Kwa kweli kitendo cha bei ya tumbaku kushuka na wakati uleule bei ya mbolea kupanda kimeleta mkanganyiko mkubwa sana kwa wakulima wa zao la tumbaku hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, msimu uliopita bei ya tumbaku kwa wastani ilikuwa ni dola 2.559. Hii siyo kwamba wastani huu ulipatikana Sikonge, hapana ni kwa nchi, hii ni kwa taarifa ya Wizara. Ukienda kwenye randama ukurasa wa 44, tani zilizouzwa zilikuwa tani 185,772 na fedha zilizopatikana zilikuwa milioni 475 plus. Ukichukua hiyo ukagawa unapata wastani wa dola 2.559, wakati huo mfuko wa mbolea ya NPK tunayoitumia ilikuwa ni dola 60.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa msimu huu mfuko wa mbolea umekwenda mpaka dola 63.89 wakati bei ya tumbaku kwa wastani ni dola 1.95, hili ni anguko kubwa sana kwa wakulima wa tumbaku.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimependa sana dhima ya Wizara katika mambo mengi ambayo yamewekwa kwenye hiyo dhima, lakini kuna sentensi moja inasema kuboresha maisha ya Watanzania. Kweli tuendee kuyaboresha maisha ya Watanzania, lakini huu msukosuko wa bei kupanda na kushuka ninadhani ni vizuri tuangalie kama tunataka kuona kwamba kweli tunaboresha maisha ya wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa najaribu kuangalia kwa nini bei ya mbolea imepanda namna hii. Nimejaribu kupitia maandiko mbalimbali, nikaja kuona kwamba bei ya kuzalisha kilo moja ya NPK ya mbolea pale Zambia ni wastani wa Kwacha 17,500 kwa tani. Kwacha moja ni sawa na dola 0.053, ukizidisha 0.053 kwa hiyo 17,500 unapata wastani wa kuzalisha tani moja ya mbolea ya NPK kule Zambia ni takribani dola 972 na point. Sasa ukizigawanya zile kwa mifuko 20 ambayo ndiyo tani moja unapata wastani wa dola 46.375.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Maganga, ahsante sana, malizia sentensi ya mwisho.

MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sana kwamba, Serikali iangalie namna ya kupunguza hizo tozo ambazo ni nyingi sana, kwa sababu toka 46 mpaka 63 ni hela nyingi sana. Tunaomba wapunguze ili kusudi wananchi waweze kupata tija.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)