Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
Ex-Officio
Constituent
None
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Bunge lako Tukufu. Nitachangia katika hoja kuhusu kuhalalisha matumizi ya mirungi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mariam Mzuzuri ametoa ushauri kuhusu kuhalalisha mmea wa mirungi kutokana na mapato makubwa ambayo nchi zilizohalalisha mmea huo zimekuwa zikipata.
Mheshimiwa Naibu Spika, mmea wa mirungi, umekatazwa chini ya Sheria ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya, Sura ya 55. Ni mmea ambao umeorodheshwa katika mimea ambayo imekatazwa (prohibited plants). Sababu kubwa ya kukataza mmea huu ni athari kubwa za kiafya na kiakili za muda mfupi na za muda mrefu kama ambavyo Mheshimiwa Mzuzuri mwenyewe amezitaja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu pia kwamba katazo hili limekuwepo pia katika ile Sheria ya awali ya Madawa ya Kulevya, Sheria Na.9, isipokuwa tu inawezekana kwamba hakuona kwa kuwa sheria hii tuliifanyia marekebisho kupitia Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2002. Kule kwenye jedwali la kwanza tukaweka mirungi (khat plant) kwamba ni miongoni mwa mimea ambayo ni hatarishi na hairuhusiwi kwa matumizi ya mwanadamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, tafiti mbalimbali zimefanyika duniani, kwa sababu ni jambo ambalo na jumuiya za kimataifa pia vilevile zililiona; na katika tafiti hizo wakati tunajadiliana au tuna-negotiate, United Nations Convention Against Illicit Narcotic Drugs and Psychotropic Substances ya mwaka 1988, tafiti zile zilileta matokeo yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, mmea huu unaojulikana kama mirungu au khat au wakati ule wa hiyo convention waliujumuisha katika zile cathinone au catha edulis, kwamba kwanza unashambulia cardiovascular system au afya ya moyo; pili, mental health system; na tatu, kwa kadri yule anavyotafuna mwisho kabisa inaenda kuishia kwenye ini, kwa hiyo inaenda kuleta liver toxicity ambayo inasababisha athari kwenye afya ya ini. Kwa hiyo hatuwezi tukaja na hoja kwamba mapato iwe faida zaidi kuliko afya ya mwanadamu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkataba huu wa Umoja wa Mataifa dhidi ya Usafirishaji Haramu wa Dawa za Narcotic na Psychotic Substance, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni signatory, kwa maana tulisaini na tuliridhia tarehe 20 Disemba, 1996 na ndiyo ilikuwa sababu hasa kuja kufanya marekebisho ya sheria hii ya mwaka 2002. Kwa hiyo niwaombe Waheshimiwa Wabunge kwamba, afya za wananchi zisiwe at the expense ya mapato au revenue.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ambalo nilitaka nilichangie, ilikuwa ni hoja ambayo ilitolewa na Mheshimiwa Thomas Maganga. Yeye ameishauri Serikali itunge sheria ya kusimamia kilimo cha mkataba (contract farming). Serikali inatambua kuwa mfumo madhubuti wa kisheria kusimamia kilimo cha mkataba ni muhimu sana ili kulinda haki na maslahi ya wakulima na wadau wote wa katika mnyororo wa thamani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe tu taarifa, kwamba zipo sheria katika sheria ambazo tunazo ambazo kwa kiasi fulani zinazungumzia masuala ya kilimo cha mkataba. Kwa mfano, Sheria ya Usalama wa Chakula, Sura 249; kuna Sheria za Kisekta, kama Sheria ya Tasnia ya Pamba, Sura 201; Sheria ya Tasnia ya Sukari, Sura 251; Sheria ya Tasnia ya Korosho, Sura 203; na Sheria ya Tasnia ya Tumbaku, Sura 202.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, lazima tukubali kwamba inawezekana sheria hizi zisijitosheleze na huko tunakokwenda ili kutekeleza malengo ya Dira ya 2050 ambapo tunasema kwamba, kilimo liwe eneo ambalo watu wote watataka kukimbilia, ikiwemo vijana, basi tunaona kwamba ni muhimu tuangalie vizuri kuona kama je, tunakuja na sheria mahususi ya contract farming au tunakuja na kanuni za contract farming. Tulisema na tunaendelea kusema kwamba, hayo yote lazima iwe ni zao la utafiti.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tuna orodha ya sheria ambazo tumeanza kuzifanyia mapitio kwa lengo la kuzifanyia marekebisho. Mifumo ya sheria za kilimo, itafanyiwa mapitio na marekebisho mwaka wa fedha 2026/2027. Kwa hiyo, pale tutakuwa tumekuja na majibu kwamba sasa tumekuja na sheria mpya au mahususi ya contract farming au tutakuwa tunafanya vinginevyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja hii ni nzuri na tunamshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kuileta na tutaifanyia kazi kuona kama tunakuja na sheria mpya mahususi ya contact farming.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa heshima na taadhima ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)