Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduma
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia fursa hii kuchangia bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na shukurani. Kwanza ninamshukuru sana Mwenyezi Mungu ambaye ametuwezesha kukaa hapa siku mbili na leo tunakwenda kuhitimisha baada ya kujadili bajeti yetu ya Wizara ya Kilimo. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa imani yake kwangu kwa kuniteua na kuwa Naibu wa Waziri wa Kilimo. Ninaahidi kulipa imani kwa imani, nikitambua wajibu wangu kwa nchi yangu, Rais wangu, pamoja na chama changu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nipeleke shukrani zangu za kipekee kwa Waziri wangu Mheshimiwa Comrade Daniel Chongolo. Waziri bora kabisa na mtu makini. Amekuwa akitupa uongozi mahiri kabisa katika Wizara na miongozo yake imekuwa mizuri kwelikweli. Ni mtu anayesikiliza, ni mtu anayetaka tubadilishe Wizara iende ikamhudumie mkulima wa chini kabisa, ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri. Nina hakika Mheshimiwa Waziri ana upendo mkubwa sana na sisi kama wasaidizi wake tunajifunza sana kutoka kwake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwashukuru sana Katibu Mkuu, Manaibu Katibu Mkuu, Wakurugenzi wote wa taasisi zote za Wizara, wamekuwa wakitupa ushirikiano mkubwa hata leo tunapojadili mafanikio ya Wizara ya Kilimo ni matokeo ya michango yao na ushauri wao, ambao sisi kama wasimamizi wa sera tumekuwa tukizisimamia ili zilete matokeo yenye tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, niende katika ufafanuzi wa hoja, na niseme tu kiukweli, Wizara ya Kilimo tangu Mheshimiwa Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameingia madarakani, imekuwa ni Wizara yenye tija na matokeo makubwa sana. Ndiyo maana hata leo katika Bunge lako Tukufu utaona katika siku mbili Waheshimiwa Wabunge wengi wameomba kuchangia, kwa sababu wanaona kuna fursa kubwa, kuna matokeo makubwa na hatua kubwa imepigwa tangu Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeingia madarakani.
Mheshimiwa Naibu Spika, wengi wanafahamu, wakati wa mapinduzi ya viwanda duniani huko katika miaka ya 1760, kule Uingereza, mapinduzi ya viwanda yalikuja baada ya matokeo ya mapinduzi makubwa ya kilimo; na wenzetu wale waliwekeza katika maeneo makubwa manne. Moja katika eneo la umwagiliaji, eneo la pili waliwekeza katika matumizi ya zana bora za kilimo, eneo la tatu waliwekeza katika matumizi sahihi ya mbolea na eneo la nne waliwekeza katika matumizi ya mbegu bora. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa upi ni mwelekeo wa Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan? Ninataka niwaeleze, haya waliyoyafanya wenzetu, Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Wabunge wote watakuwa mashahidi wa hiki ninachokwenda kukisema.
Mheshimiwa Naibu Spika, cha kwanza, Mheshimiwa Rais wakati anaingia madarakani, bajeti ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ilikuwa bilioni 51.5. Leo tunapozungumza bajeti ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imeongezeka na kufika bilioni 382. Huo ni uthubutu mkubwa wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kwa hiyo, ukiangalia hivyo na hata ukienda kuangalia bajeti mama ya Wizara, wakati anaingia madarakani Mheshimiwa Rais, ya bilioni 294, leo tunazungumza bajeti ya Wizara ya Kilimo trilioni 1.105, ambayo tunakwenda kuipitisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais alituelekeza sisi Wizara ya Kilimo, alisema ninataka sasa tutoke kwenye kilimo cha kutegemea mvua kilimo cha msimu, ninataka kwenda kwenye kilimo cha umwagiliaji. Haya ambayo yalileta mapinduzi ya viwanda, leo tunakwenda kuyatekeleza. Cha kwanza tunapozungumza leo, tunatekeleza miradi ya umwagiliaji 146 yenye thamani ya Shilingi za Kitanzania trilioni 2.4, ipo inaendelea na utekelezaji wake na wakandarasi wako kazini. Hii ni nia ya Mheshimiwa Rais ya kuhakikisha tunatoka kwenye kilimo cha msimu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais ameelekeza, tuwe na Gridi ya Taifa ya umwagiliaji, kutoa maji Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika kupeleka katika mikoa yenye ukame. Wewe fikiri unatoa maji zaidi ya kilometa 1,645 kupeleka katika maeneo yenye upungufu, mradi huu peke yake utagharimu zaidi ya fedha za Kitanzania trilioni 2.5. Eneo la umwagiliaji peke yake litakuwa zaidi ya hekta milioni tatu. Mikoa ambayo itanufaika katika maeneo hayo ni mikoa 12, wilaya 24, na vijiji 441; na kutakuwa na mabwawa makubwa zaidi ya 52. Huu ni uthubutu na nia njema ya Mheshimiwa Rais kwa Watanzania kwenye eneo la umwagiliaji peke yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama haitoshi Mheshimiwa Rais alituelekeza tufanye usanifu wa kina kwenye mabonde yote makubwa hapa nchini; na hiyo kazi inaendelea sasa hivi. Tunavyozungumza tumeshafanya usanifu wa kina na mabonde 10 yanakwenda kutekelezwa; ambapo gharama tu peke yake ya mradi huu ni takribani fedha za Kitanzania trilioni 3.9. Mabonde kama Bonde la Mto Rufiji, Bonde la Mto Kilombero, Bonde la Mto Malagarasi, Bonde la Kamsamba, Bonde la Mto Ngono, Bonde la Mara Valley, Bonde la Lukuledi, Bonde la Ziwa Rukwa, Bonde la Suguti na Bugwema na Bonde la Kasinde. Haya ni malekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye eneo la umwagiliaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais ametuelekeza vilevile, tuhakikishe kwenye miradi ya umwagiliaji ya asili, kwa sababu kuna vijiji vingi vina vile vimiradi vidogovidogo vyenye wastani wa thamani ya shilingi 500,000,000 mpaka shilingi 1,000,000,000, nayo tuitekeleze. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yaani wakati tunaendelea na miradi mikubwa Wizara kupitia tume ifanye miradi midogo midogo. Hiyo ndiyo nia njema ya Mheshimiwa Rais kuhakikisha Tume inamsadia mkulima wa kawaida katika kuongeza tija. Tuna mradi wa uchimbaji wa visima zaidi ya 67,000 ambavyo tutafika katika halmashauri zote. Ninavyozungumza sasa hivi tayari Tume ya Umwagiliaji ina magari 19 ya uchimbaji visima ambavyo tutawachimbia wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, wapo tutakaowachimbia bure kabisa kwa ruzuku ya 100% wapo tukaowachimbia kwa 50% watachangia 50% na wale wenye kipato kikubwa watachangia takribani 75% na 25% Serikali itatoa. Lengo ni kusaidia sekta ya kilimo kwenye eneo la umwagiliaji ili wananchi wafanye kazi ya kilimo muda wote katika msimu wa mwaka. Kwa hiyo, utaona kwenye hilo eneo peke yake la umwagiliaji Mheshimiwa Rais amewekeza nguvu kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ambalo ninataka nilitolee ufafanuzi ni kwenye matumizi ya zana bora ambayo wenzetu walifanya na Mheshimiwa Rais sasa anafanya. Tunakwenda kuwekeza matrekta zaidi ya 10,000 kwa kujenga vituo vya zana za kilimo kwenye halmashauri zote nchini zaidi ya 1,000. Hadi sasa hivi tumekwishafungua vituo 79 kwenye halmashauri 25 nchini. Vyote tunataka mkulima wa kawaida aweze kupata zana za kilimo; yaani matrekta, pawatila; ili yaweze kumsaidia katika kulima na kuongeza tija katika mashamba yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa haya yote unayoyaona tu ni jitihada za Serikali,. Katika eneo la matumizi sahihi ya mbolea, ninyi wote ni mashahidi; wakati Mheshimiwa Rais anaingia madarakani, nchi yetu hii matumizi ya mbolea peke yake yalikuwa chini ya tani 400,000. Leo matumizi yameongezeka kiasi kwamba tija imekuwa kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitatolea mfano tu wa zao la mahindi peke yake, miaka mitano iliyopita hatukuwepo hata kwenye tatu bora, waliokuwa wanaongoza ni South Afrika, Nigeria pamoja na Nchi kama Ethiopia. Mwaka jana Tanzania tulikuwa nchi ya pili kwa uzalishaji wa mahindi tukifuatiwa na South Afrika. Tumezalisha takribani tani 11,000,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa fikiri watu ambao tulikuwa hatupo kwenye records; tija imeongezeka kiasi kwamba haya mazao yaliyokuwa yanaonekana mazao ya chakula, ukiangalia thamani ya mazao, export value yake, yameleta fedha nyingi za kigeni. Kwa mfano, mahindi peke yake yameingizia Taifa letu karibu bilioni 684.9, mchele umeingizia bilioni 619.4, maharage imeingiza bilioni 304.2. Ukienda kwenye ufuta utakuta trilioni mbili, mbaazi utakuta zaidi ya bilioni 824. Hayo ni mazao ambayo yalikuwa yamezoeleka ni mazao ya asili na si ya kibiashara, lakini leo yana tija kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuko kwenye track sahihi. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge tupitishe hii bajeti na nimwombe hata ndugu yetu Mheshimiwa Ado alikuwa anataka Mheshimiwa Waziri amtembelee, lakini mwisho wa siku anasema tusipitishe bajeti, tusipopitisha bajeti Mheshimiwa Waziri hawezi kufika katika eneo lake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwaombe Waheshimiwa Wabunge tupitishe bajeti hii. Ninaamini tuko kwenye track sahihi na tutamsaidia Mheshimiwa Rais na hii nchi itasonga mbele na kilimo ndiyo mkombozi wa Watanzania wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)