Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Masache Njelu Kasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye Wizara hii muhimu sana, Wizara yetu ya Madini. Kwanza, ninaanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri, hotuba ambayo imesheheni kila kona. Ninampongeza Waziri pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri lakini na wasaidizi wake wengine wote wakiongozwa na Katibu Mkuu. Kwa kweli wanatutendea haki Watanzania hasa ambao wapo Sekta ya Madini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaendelea kuipongeza pia Wizara kwa kuendelea kuongeza mapato. Tumeona hapa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri namna ambavyo tumeweza kwenda kuyafikia malengo ya mapato kutoka makusanyo ya Mfuko Mkuu asilimia tisa mwaka 2023 mpaka leo tumefikia 11%. Haya ni mafanikio makubwa sana na hii yote inaakisi malengo ya Rais, mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa namna maono yake aliyokuwa nayo Wizara kweli wameenda kuyatekeleza kwa vitendo na sisi tunaona. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona pia mapato yao kwa kadri ambavyo waliwekewa malengo kwa mwaka huu ambapo ilikuwa wakusanye shilingi trilioni 1.4, lakini mpaka kufikia Machi ambapo ilikuwa wakusanye shilingi bilioni 900, lakini wamefikia shilingi trilioni 1.03. Haya ni mafanikio wameweza kuvuka lengo kwa zaidi ya 114%, tunawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba wanaweza kwenda kuvuka malengo haya ambayo wamewekewa na haya ambayo sisi tunaendelea kuwashauri, tunaomba sana waendelee kuilinda hii sekta ya uchimbaji vizuri ili wachimbaji wetu waweze kufanya kazi zao kwa uhuru, waweze kuchimba vizuri na malengo yao na malengo ya Serikali yaweze kwenda kutimia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, nimpongeza Mheshimiwa Waziri, aliweza kutekeleza yale maono ya Mheshimiwa Rais kwenda kuzifuta zile leseni za utafiti, leseni ambazo kwa muda mrefu zimeshikiliwa na watu na zilikuwa hazijaendelezwa; wamezifuta na kuzirudisha Serikalini. Hili ni jambo kubwa na kilio cha wananchi na wachimbaji wetu wengi kilikuwa ni hizi leseni nyingi za utafiti kwenye maeneo yetu ambazo zimeshikiliwa na watu na hazifanyiwi kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuzifuta na kuzirudisha Serikalini, nina ushauri mdogo wa nini cha kwenda kufanya. Mheshimiwa Waziri, pamoja na kuzifuta na kuzirudisha Serikalini, tunaomba cha kwanza leseni hizi ziweze kutambuliwa ili wananchi wetu na wachimbaji wetu waweze kuzifahamu. Hii itaturahisishia kwenye utaratibu wa kwenda kuzigawa kwenye leseni ndogondogo kwa maana ya PML. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pale watakapokwenda kuzigawa, wao itawawia rahisi kwenda kuyatembelea maeneo hayo na mtu anapokwenda kuomba leseni hizi kwenye maeneo husika anajua eneo gani ambalo yeye ataweza kwenda kulipata na hii itaturahisishia yale manung'uniko ya wachimbaji wetu wadogo kukosa maeneo ya kufanya kazi, haya yataenda kupunguza kupitia mfumo huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba twende tukayagawe kwenye maeneo ya wachimbaji wadogo lakini muhimu kupitia taasisi yetu ya utafiti GST twende tukayafanyie utafiti maeneo haya ili tunapokwenda kuwagawia wachimbaji wetu wadogo kupitia PML twende tukawagawie maeneo ambayo wao wakienda kuyafanyia kazi wataenda kupata tija, uzalishaji utakuwa mzuri, lakini pia wao wapate na Serikali iweze kupata kupitia kodi mbalimbali ambazo watakuwa wanazilipa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, kwenye hotuba ya Waziri amezungumza hapa mpango mzuri wa MBT. Kupitia hizi leseni ambazo wamezifuta kupitia leseni kubwa za utafiti tuone namna bora na nzuri kwenye zile leseni ndogondogo watakazozigawa na zenyewe waendelee kutenga maeneo ya vijana wetu kwa ajili ya MBT ili wayafanyie utafiti na vijana hawa waweze kugawiwa maeneo haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, zile fedha shilingi bilioni 200 ambazo Mheshimiwa Rais alizitoa na Wizara ya Madini ilizipata, vijana wawezeshwe ili kuyapata maeneo kupitia RASHIA, ndipo ambapo tutakuwa tumewasaidia vijana wetu. Tutakuwa tumewasaidia kwenye utafiti kwenye maeneo haya ya MBT lakini pia maono ya Wizara na maono ya Mheshimiwa Rais tutakuwa tumeweza kuyafikia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mazuri haya kuna baadhi ya maeneo ambayo ninataka kuyachangia. Jambo la kwanza ni jambo la utafiti. Tumeona kwenye hotuba hapa bado nchi yetu eneo la utafiti lililofanyika ni kidogo sana na maeneo mengi ya utafiti yaliyofanyika bado tija yake wananchi hawajaiona.

Mheshimiwa Naibu Spika, amezungumza hapa Mikoa ya Lindi, Geita na mingineyo kwamba yalifanyiwa utafiti na baadhi ya maeneo ambayo yalienda kufanyiwa utafiti wakishirikiana na Barrick ikiwemo Nyang'hwale, Nzega, Igunga na mengineyo. Tunaomba Serikali iwekeze kwa nguvu kubwa katika maeneo ya utafiti ndiyo itakuwa ukombozi kwenye Sekta ya Madini, lakini pia tutaenda kuzalisha zaidi kuliko hiki ambacho tunazalisha sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano kwenye Wilaya yangu ya Chunya. Leo maeneo mengi ambayo wachimbaji wetu wanaendelea kufanya uchimbaji hayajafanyiwa utafiti. Wanafanya uchimbaji wa kawaida, lakini tunaweza kuzalisha kwa wastani sasa hivi ni almost kilo 400 kwa mwezi, ndiyo tunayozalisha sasa hivi, ni fedha nyingi. Hizi kilo 400 kwa mwezi ukipiga wastani kwa bei ya shilingi 360,000, kwa bei ya leo, tunapata zaidi ya shilingi bilioni 142 ambayo tukilipa kodi ya moja kwa moja zaidi ya shilingi bilioni 12 tunalipa kwa mwezi Serikalini, ni fedha nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukienda kuyafanyia utafiti maeneo mengi ndani ya Wilaya ya Chunya tutatoka uzalishaji wa kilo 400 kwa mwezi tutakwenda kukimbilia kwenye kilo 500 kwa mwezi. Ndivyo ambavyo Serikali itapata, wachimbaji wetu watapata lakini na uchumi wa nchi yetu utazidi kukua na kwenda mbele zaidi. Ndege nyuki zinaruka lakini sisi kule kwetu Chunya hatujaziona. Mheshimiwa Waziri, ninaomba na sisi Chunya tunahitaji ndege nyuki ili ziweze kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine la msingi na muhimu ni suala la umeme kwa wachimbaji wadogo. Tunafahamu Serikali chini ya mama yetu Samia Suluhu Hassan imeendelea kufanya vizuri kwenye upande wa umeme, imepeleka vijiji vyote na sasa tunakwenda kupeleka kwenye maeneo ya vitongoji vyote kufikia 2030. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lazima Wizara ije na mpango kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati. Ninaomba Mheshimiwa Waziri, kama hatanieleza jambo la msingi kwa namna ambavyo atapeleka nishati ya umeme kwa wachimbaji wangu wadogo Wilaya ya Chunya, leo ninashika shilingi hapa simwachii kwenye mshahara wake ili kuhakikisha kwamba umeme unaenda kwenye maeneo ya wachimbaji wangu wilaya yangu ya Chunya na wao waweze kunufaika, wapunguze gharama ya uzalishaji kutumia mafuta. Hivi ndivyo tutakavyoweza kwenda kuwasaidia wachimbaji wetu wadogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kubwa na la kimsingi ni hili jambo la technical support. Tumeona namna ambavyo leo tumekuwa na raia wa kigeni wengi sana kutoka Bara letu la Asia, wale wenye macho madogo madogo, wamezagaa wengi kwenye maeneo yetu ya uchimbaji. Hakika huko tunakokwenda tunaenda kutengeneza janga lingine kubwa zaidi. Wameingia kwa kuleta utaalam kwenye maeneo ya uchimbaji, lakini ukienda ground kule na vibali vyao vinavyoeleza kitu wanachokwenda kukifanya kule ni tofauti na malengo ambayo yamekusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunaona raia hao wanafanya uchimbaji mdogo mdogo ambao Watanzania na wachimbaji wetu wadogo wangeweza kufanya. Wanaendesha mitambo, wanaendesha mpaka maguta mpaka boda boda ambazo ndiyo ajira za vijana wetu, lakini wao leo ndiyo wanazozifanya hizo. Kuendesha ma-excavator ni ajira ambazo siyo za kitaalam, vijana wetu wanaweza wakafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lazima tuone namna nzuri na bora za kuweza kusimamia vibali vyao na wao waweze kufanya kazi iliyowaleta na siyo tu kufanya kazi iliyowaleta, tunataka waje walete technical support, waambukize Watanzania ili Watanzania wapate ule utaalam tuweze kujiendesha wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi tukawa tunaendelea kuwatumia wao miaka hadi miaka. Wamefika hatua sasa hivi wanaingia mikataba na wachimbaji wetu wadogo hawa, mikataba kandamizi, mikataba ya kuchimba kwenye maeneo yao, maeneo ambayo ni hatarishi sana. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Mbunge kwa mchango wako.

MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa kunipa nafasi na ninaunga mkono hoja. (Makofi)