Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nichangie kwenye Wizara ya Madini, Wizara ya kaka yangu Mheshimiwa Athony Mavunde.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninapenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri, kwa bajeti yake nzuri ambayo ameisoma. Pili, kwa jinsi ambavyo Wizara hii ameituliza kwa sababu ukifuatilia Mabunge yaliyopita nyuma huko, Bunge la Tisa, la Kumi, migogoro ya wachimbaji wadogo ilikuwa ni mikubwa sana, lakini kwa sasa kumetulia. Tunampongeza sana Waziri, lakini tunaipongeza Serikali kwa jinsi ambavyo inafanya kazi na kwa jinsi ambavyo wanaratibu majukumu mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza pia Mheshimiwa Rais, political will, utayari wa Mheshimiwa Rais kuhakikisha kwamba investment na uwekezaji mkubwa unafanyika kwenye Sekta ya Madini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina mambo machache ya kuchangia. Jambo la kwanza ninalotaka kuchangia, ni kwenye kitu kimoja kinaitwa local contents: local contents kwanza ninamshukuru na ninampongeza Mheshimiwa Waziri. Akiwa kama kijana ameonesha nia ya dhati, thabiti ya kuwatetea vijana wa Kitanzania kuhakikisha kwamba local content ya nchi yetu inalindwa, inasimamiwa na inabaki kuwa sehemu ya Watanzania. Moja kati ya kauli zake ameongea kwenye mimbari hapa ni kwamba, atadhibiti bidhaa zote ambazo zinatoka nje. Ambazo zinaweza kutolewa na Watanzania, zitolewe na Watanzania kwa 100%. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili ni jambo kubwa, kama vijana tuna-appreciate, kama vijana tunatambua kwamba kama Wizara wameamua kabisa kuunga mkono. Kwenye local content Mheshimiwa Waziri ni jambo kubwa kama nchi kwa sababu tuna rasilimali kubwa ya madini. Ukisoma kwenye Ilani ya CCM, inasema kwenye kitabu kidogo, inasema hivi “CCM inatambua kuwa Sekta ya Madini ina nafasi ya kipekee katika kuchangia ukuaji wa pato la Taifa, ukuaji wa fedha za kigeni na ukuaji wa uchumi kwa ujumla”.

Mheshimiwa Naibu Spika, tafsiri yake anakwenda chini anasema wataongeza kufanya utafiti, lakini pia kutenga maeneo maalum kwa ajili ya wachimbaji wadogo. Hii yote ambayo wanaifanya kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo, ni kwamba wanaisimamia Ilani ya CCM na wanatekeleza kile ambacho pia Mheshimiwa Rais kwenye hotuba yake alisema:

“Katika jitihada zetu za kuendeleza Sekta ya Madini, tutapitia upya leseni zilizotolewa ili kubaini ambazo hazijaendelezwa na kuchukua hatua na kuzitoa kwa wachimbaji wenye nia ya dhati ya kufanya uendelezaji wa maeneo husika. Wachimbaji wadogo wamekuwa nguzo ya kutegemewa katika Sekta ya Madini nchini”. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri anafanya lile ambalo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alilihutubia ndani ya Bunge, lakini pia Watanzania wamekuwa wakitegemea kutoka kwao. Kwa hiyo, ninampongeza sana kwa jinsi ambavyo wanalinda local content. Moja, ameweka katika ukurasa wake wa 87 wa hotuba anasema: “Tutarasimisha wachimbaji wadogo ili wawe na sehemu ya mnyororo wa thamani’. Hili ni jambo kubwa kwamba wachimbaji wadogo wamekuwa wakifanya kazi za uchimbaji kiholela, kama Wizara wanachukua hatua ya kwenda kurasimisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri na uzuri Mheshimiwa Waziri wa Fedha leo yuko hapa na hili ni jambo kubwa. Hii bajeti ambayo tunaipitisha hapa, ni bajeti ambayo walitengewa kukusanya shilingi bilioni 124, lakini Serikali imewapatia asilimia nane tu ya bajeti. Mheshimiwa Waziri wa Fedha yuko hapa, wizara hii ndani ya miezi nane imekusanya shilingi bilioni 880 licha ya kwamba tumewapa asilimia nane tu ya bajeti yao, lakini wamekusanya shilingi bilioni 880. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tafsiri yake tukiwapa fedha Wizara ya Madini, tutakusanya fedha nyingi sana za kigeni kwenye nchi yetu, tutakusanya fedha nyingi sana katika maendeleo yetu. Asilimia nane Mheshimiwa Waziri ni fedha ambayo ni ndogo, waiangalie kwa jicho la karibu Wizara ya Madini, kuiwezesha kwa kuipatia fedha kwa sababu bila fedha, hatutawezesha utafiti, bila fedha hatutawezesha kuendeleza hiki ambacho Mheshimiwa Waziri anakifanya kuhakikisha kwamba, tunapata maeneo mengi ambayo ni ya uchimbaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaomba sana kama wameweza kukusanya shilingi bilioni 880 ndani ya muda mfupi wa miezi minane tu, basi tuiombe Wizara ya Fedha iwaongezee fedha iwapatie fedha kwa wakati ili watuletee fedha nyingi za kigeni kwenye nchi yetu na ili waweze kutusaidia kama Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kama kijana tunamtegemea Mheshimiwa Waziri wa Madini kwenye suala la CSR, hii mandatory, CSR ni mandatory, CSR siyo mtu anajifanyia kwa anavyojitakia. Ninampa tu utaratibu mmoja wa Nchi ya Zambia, waliamua kwamba CSR yao wanaielekeza kwenye kujenga viwanja vya nchi yao na wakawa wameisimamia ikafanya hivyo. Waziri kwenye CSR kwenye sheria ambayo tumeipitisha mwaka 2023 Mheshimiwa Waziri, sehemu moja amezungumza hapa chini amesema hivi, ninaomba ninukuu alichokisema, anasema hivi; “Mmiliki wa leseni ya madini atakayeshindwa kutekeleza masharti yaliyoainishwa chini ya kanuni hizi za CSR atakuwa ametenda kosa chini ya sheria na atachukuliwa hatua kwa mujibu wa Kifungu cha 63 cha Sheria” na amesaini tarehe 15 Juni, 2023. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tafsiri yake ni nini? Ni kwamba, kuna watu wanafanya kazi hawatoi CSR, wanafanya vile wanavyojisikia wao, malalamiko ya CSR ni makubwa, CSR itatupunguzia kwenye changamoto mbalimbali za shule, kwenye vituo vya afya, kwenye maeneo mbalimbali. CSR siyo hisani, ni sheria. Watengeneze utaratibu kupitia Tume ya Madini kuhakikisha kwamba wanaisimamia CSR ili iweze kuwasaidia Watanzania na iweze kufanya kazi ile ambayo imekusudiwa. Tofauti na hapo tutafanya watu wachimbe madini, waondoke, lakini hawako concerned na jamii yetu ambayo inakaa na madini hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunatamani Wizara hii isimamie CSR, isimamie CSR ili maneno yote ambayo yanatoa, yanahusika na uchimbaji wa madini tuweze kupata. Sisi kama Makete tumepata fedha ya BARRICK, walifanya vizuri sehemu fulani kwenye CSR. Tunatamani na migodi mingine iweze kuacha hiyo fedha kwa sababu ni sheria na wameitunga wao wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ninaweza kuipongeza Wizara kwenye gold reserve. Tanzania kihistoria na Watanzania lazima wafahamu tumekwama kwa mara nyingi sana kuwa na gold reserve, ni Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan pekee mwaka 2024 ndiye aliyeweza kuwa na gold reserve kwenye nchi yetu. Toka mwaka 1997 ambapo tulikuwa na Mineral Policy ya mwaka 1997 lakini na Mineral Act ya mwaka 1998, tulijaribu kuwa na gold reserve tukashindwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2024 Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuwekea reserve ambayo hadi sasa tunaelekea karibu tani 23 tunaenda kuzifikia ambapo kihistoria tunaenda kuwa wa sita au wa tano barani Afrika kwa kuwa na gold reserve kwenye nchi yetu. Ukiwa na gold reserve tafsiri yake ni nini, unalinda shilingi yako, unalinda uchumi wako lakini muda wowote jambo likitokea mnaweza mkauza gold reserve na mkafanya jambo lingine. Hili ni jambo kubwa katika nchi kuwa na gold reserve.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumpongeze Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi alivyoamua yeye mwenyewe kwa makusudi ya dhati wamepita Waheshimiwa Marais wangapi, tumeshindwa kuwa na gold reserve. Kuwa na gold reserve ni ulinzi wa nchi yetu, kuwa na gold reserve ni heshima kwa Taifa letu, kuwa na gold reserve inatupelekea kwenye taswira kubwa katika uchumi na ukuaji wa Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hili ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri. Kubwa wanawahakikishia assurance wachimbaji wadogo kwamba kuna soko la kuuza wanapopata changamoto ya wanunuaji, BoT inahusika kwenda kununua. Hii wanawapa assurance ya soko, ni kitu kikubwa kwa vijana wetu kwenye nchi yetu, ni jambo kubwa ambalo nilitamani kuchangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama kijana mwenzake ninawaomba Waheshimiwa Wabunge, tuiunge mkono Wizara hii, tuwapitishie bajeti yao, tuwape fedha wakafanye hiki ambacho wamekifanya, kama ndani ya miezi nane wamekusanya shilingi bilioni 880 kwa fedha ambayo wamepewa asilimia nane tu ya fedha waliyoiomba, ni vyema nikawashawishi Wabunge wenzangu tuwaunge mkono na tumuunge mkono Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tuko tayari kum-support na tunasema wazi kwamba kazi anayoifanya Waziri tunaiunga mkono, hizo leseni ambazo zimefutwa azisimamie ili Watanzania wapate haki na watendewe haki. Zaidi wana utaratibu wanakwenda kuufanya kwenye suala la ubia, ninashukuru kwamba wana mkakati kwa wale Watanzania ambao wanaingia ubia na watu wa nje katika uchimbaji wa madini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wameona changamoto ambayo inajitokeza, Watanzania wanapigwa na wanaumizwa, wameunda mkakati ambao unaenda kuwa-support ikiwa ni kuhakikisha kwamba kunakuwepo na kanuni ambazo zinamlinda zaidi Mtanzania kuliko mazingira ambayo anakutana nayo kwa sasa. Hili ni jambo kubwa kwetu na sisi kama Watanzania tunafurahi. (Makofi)