Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa nafasi hii adhimu ya kuchangia siku ya leo, lakini nimshukuru sana Allah Subhanahu Wataala kwa siku nzuri kama ya leo, siku yangu ya kwanza kuchangia hapa Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze sana Wizara kwa kazi nzuri waliyofanya ya kuandaa bajeti nzuri na hongera sana Mheshimiwa Waziri kwa bajeti nzuri aliyoileta Mezani. Katika bajeti hii Mheshimiwa Waziri ameonesha kwamba kuna maeneo yaliyorudishwa Serikalini ambayo walipewa wachimbaji wadogo wakati huo wakashindwa kuyafanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa inavyoonekana kwa kuwa yamerudishwa Serikalini pia watarudishiwa wale wachimbaji ambao sasa wanaweza kuyafanyia kazi vizuri. Ninaishauri Serikali maeneo hayo watakapopewa hao wachimbaji wadogo wadogo, ni vema sasa wakasaidiwa kufanya uchunguzi, lakini pia wakasaidiwa kuangalia maeneo hayo ambayo yana madini ili wapewe maeneo ambayo yako tayari wakijua madini yanapatikana sehemu gani ili kuwa-empower lakini pia kuwapunguzia gharama zisizokuwa na sababu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nimpongeze sana mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya, lakini kwa upendo mkubwa anaotuonesha Watanzania. Mama yetu Samia Suluhu Hassan ameweka jicho lake kwenye sekta ya madini kupitia Mpango wa MBT wa kuwawezesha akina mama, vijana na walemavu na wao pia kuonekana kwenye sekta ya madini wanashiriki vilivyo ni jambo zuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunampongeza sana Rais wetu kwa jambo zuri hili alilolifanya kwa kweli anaonesha ni jinsi gani anavyotaka kuwasogeza Watanzania wa hali ya chini kwenye uchumi wa kati. Ushauri wangu kwa Serikali, ninaishauri Serikali kuweka mikopo isiyokuwa na mazingira magumu ili kuwasaidia wachimbaji hawa wadogo ili na wao waweze kujimudu yaani mikopo ya bei nafuu, lakini pia wapewe mafunzo kwa vitendo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wanapopata mafunzo kwa vitendo na wao inawasaidia kuwafanyia kazi zao kuwa nyepesi. Niendelee kumpongeza sana Waziri wetu kwa juhudi kubwa anazozifanya, lakini pia kuwawezesha wananchi wetu hususan akina mama kwa kweli Mheshimiwa Rais hakukosea kumchagua, kazi zake tunaziona kaka yetu aendelee yuko vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe pia tuweke juhudi kubwa kuhakikisha tunawawezesha wananchi wetu hususan akina mama kupata ujuzi wa kuongeza thamani ya madini yetu hasa kwenye madini ya vito. Tunapofanya jambo hili kwa sababu Watanzania wengi hususan wachimbaji wadogo wanakuwa hawana ujuzi huu, tunapowapa ujuzi huu inasaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, Mkoani kwangu Mara pale Musoma Mjini tuna soko kubwa sana la madini, lakini wanawake wa pale Musoma Mjini hawana ujuzi wowote wa vito, wanaona tu watu wanakuja wananunua madini wanaondoka. Pia, pale wapo vijana ambao wangefanya kazi hizo. Kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, mafunzo hayo sasa yawe ya haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuiona fursa hiyo. Mama yetu Samia Suluhu Hassan alivyoitangaza kupitia Wizara yetu ya Madini basi na mimi moja kwa moja nikaongea na vijana, akina mama na watu wenye ulemavu na hivi wako tayari. Nimekwishaandaa watu 5,000 ambao sasa wanasubiri mafunzo hayo ili na wao moja kwa moja watakapowezeshwa waingie kwenye biashara hiyo ya vito vya madini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri atakavyo-wind up hapa, nitamshukuru sana kama atanikubalia kuja pale Musoma katika Jimbo langu la Musoma Mjini kuja kuangalia wale wanawake wa Musoma Mjini ambao wanahitaji mafunzo hayo na vijana pamoja na walemavu. Niendelee kuipongeza Serikali kwa mipango yake mizuri inayoendelea nayo ya kuwawezesha Watanzania na hasa Mkoani kwangu Mara, ninashukuru wanaendelea vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa Mheshimiwa Rais wa kutunza akiba ya dhahabu ni jambo zuri sana na ni jambo la uzalendo, nimpongeze sana Rais wetu, mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anazozifanya za kuendelea kujali rasilimali ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niishauri Serikali pamoja na kutunza dhahabu, ninashauri Serikali sasa ielekeze jicho kwenye utunzaji wa akiba ya madini ya Tanzanite ambayo ni madini pekee kote duniani yanapatikana Tanzania peke yake. Madini hayo yanaweza kutusaidia kwa sababu hakuna mtu mwingine duniani kote mwenye madini hayo wala nchi yoyote inayoweza kupata madini hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo na sisi ni kitu cha kwetu ambacho tunajivunia ni kitu cha kipekee ni sawa na muse, sisi madini yetu ya Tanzanite ndiyo muse yetu ya Tanzania. Yanapoweza kutokea majanga kama yaliyotokea majanga ya mapigano, majanga mbalimbali, kwa mfano kipindi cha majanga yalitokea ya kimataifa mafuta yamepanda bei yalipotokea majanga haya ya kimataifa, gharama za maisha zimekuwa juu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaweza sasa na sisi wakati huo wao wakipandisha bei mafuta na sisi tunapandisha madini yetu ya Tanzanite bei kwa maana ya kwamba kama kuna mtu anataka kupandisha chake bei basi na sisi cha kwetu tunakipandisha bei ili tubadilishane hiyo…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa ahsante sana.
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana. Ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia kwa mia. (Makofi)