Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nsimbo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa ninaomba nimshukuru Mungu ambaye ametupa uzima na uhai hatimaye leo tarehe 27 tupo humu ndani. Ninaomba nimpongeze Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia sekta ya madini, ameitendea haki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimpongeze sana Waziri wetu ambaye anafanya kazi nzuri pamoja na Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu pamoja na Makamishna wote wa Wizara, wanafanya kazi vizuri sana wanastahili pongezi kupitia sekta ya madini, tunaona tumepata faida kubwa, mafanikio makubwa yamepatikana kupitia sekta ya madini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo langu nina kata tatu ambazo kuna wachimbaji wawekezaji. Kwa sababu katika maeneo ya kata hizo tatu tuna wawekezaji, lakini kuna wawekezaji wengine na wao ni wachimbaji wadogo wadogo, ninaomba kutengewa maeneo blocks kwa ajili ya wachimbaji wadogo wadogo kwa sababu wachimbaji wadogo wadogo ndiyo nguvu kazi ya Taifa letu, pia ni Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa unakuta katika maeneo yetu, unakuta mtu mmoja ana leseni 100 au zaidi ya 100, tuna vijana, tuna wanawake ambao ni wachimbaji ambapo wakipata fursa kubwa wanaweza kuwasaidia wanawake wenzao, lakini sasa kumekuwa kuna wawekezaji ambao sasa na wao wamekuja kuwa wachimbaji wadogo wadogo katika maeneo yetu. Matokeo yake sasa wale wachimbaji wadogo wadogo wa kwetu wa Tanzania wanakosa fursa ya kuchimba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimshauri Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa sababu kuna leseni ambazo wamefanya utafiti zimeonekana zile leseni hazifanyi kazi. Mheshimiwa Waziri alishaahidi kuwa zile leseni ambazo hazifanyi kazi, atakwenda kufanya utaratibu ili vijana wetu waweze kupata sehemu ya kuchimba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna wanawake vilevile ambao wana uwezo mkubwa tunawaona ambao wanafanya kazi nzuri ya kimataifa, wanajulikana tuendelee kuwapa uwezo ili na wenyewe waweze kuwainua akina mama wenzetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati ya wawekezaji ifuatiliwe, kuna ujanja ujanja kwa wawekezaji. Serikali inapoteza mapato mengi sana kwa sababu mwekezaji anakuja anakwenda kule kijijini moja kwa moja hapitii kwenye Wizara anakwenda kufanya lobbying kwa mwananchi ambaye hana uelewa wowote anamdanganya, anaingia naye ubia, akishaingia naye ubia anaanza kuchimba matokeo yake yule Mtanzania anakuja kupata hasara. Tunaomba hili jambo muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika ofisi za Mikoa wasimamizi wale wa mikoa, Ofisi za Madini wapitie mikataba upya ya wawekezaji. Kwa sababu kuna wawekezaji wengine wameingia kiujanja ujanja wanakimbia hata kutoa mapato ya uhalisia. Sasa kwa sisi Watanzania tunazidi kuathirika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu Serikali iliweka 30%. Serikali imesema 30% kwa ajili ya wawekezaji wa ndani, lakini unakuta katika ile mikataba inakuwa tofauti. Vilevile, mikataba ya Serikali kupitia wawekezaji walishawapa miaka mitatu lakini kuna wawekezaji wengine wanafanya ujanja ujanja hawafuati sheria wanakwenda mpaka miaka mitano au zaidi, sasa hiyo inaendelea kutunyonya sisi Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Serikali isimamie kwa ukamilifu kwa sababu tumeona mafanikio makubwa kupitia sekta ya madini. Sasa kuna watu ambao wameingia katika nchi yetu, wanaitwa wawekezaji ambapo hawa wawekezaji wanakimbia hata kutoa katika maeneo husika, wanatakiwa watoe percentage katika halmashauri zetu, lakini hawatoi.
Mheshimiwa Naibu Spika, wengine wamekaa kwenye vijiji vyetu wanatakiwa watoe huduma katika maeneo ya vijiji vyetu kwenye zahanati, kwenye vituo vya afya, kwenye shule za msingi na sekondari, lakini hawatoi wanajificha. Hivi hao ni wawekezaji au wawekezaji bandia? Mwekezaji kama mwekezaji, tunamjua mwekezaji anatoa misaada katika maeneo ya vijijini katika maeneo yale husika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa ahsante sana, hitimisha muda wako umekwisha…
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nikushukuru sana, lakini ninaomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri. Ninajua Mheshimiwa Waziri ana ahadi na mimi, atakwenda kuangalia nguvu kazi, atahakikisha wananchi wangu wa kata zile tatu Ibindi, Sitalike na Machimboni wamepata maeneo ya kuchimba. Ahsante sana. (Makofi)