Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Katoro
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KIJA L. NTEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nikushukuru sana kwa nafasi hii kwa ajili ya kuchangia Bajeti ya Wizara ya Madini. Kwanza nimpongeze Waziri wa Madini, kaka yangu Anthony Mavunde kwa kazi anayofanya, anafanya kazi kubwa sana. Mheshimiwa Mavunde sifa zake zimevuma sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu moja nimpongeze kwa kutoa leseni katika eneo la Kigosi, alifanya kazi kubwa sana, alikuwa na malengo ya kutoa leseni 6,000 ila akapitiliza akatoa leseni 9,000. Ni 146% zaidi ya kiwango ambacho alikuwa amejipangia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mavunde amekuwa mtu mwema sana wa kutoa maeneo kwa wachimbaji wadogo. Tumeona alitoa eneo lile la Sengerema – Igalula juzi juzi hapa leseni zimeshatoka, watu wamepata ili wakafanye kazi, kwa sababu Waziri anajitahidi kuwasaidia watu ili waweze kufanikiwa zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijielekeze katika eneo ambalo ninataka nizungumzie kidogo kiujumla Wizara ya Madini wanafanya vizuri. Asubuhi ma-RMO wa Mikoa yote hapa nchini walikuwepo, tulitamani kuwapongeza kwa kazi wanayoifanya kumsaidia Waziri wa Madini kutekeleza majukumu katika kila eneo wale ma-RMO wakiongozwa na RMO wangu wa Geita kaka yangu Samwel Shoo, wanafanya kazi kubwa sana kutekeleza majukumu yao na kusimamia sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nizungumzie tu mambo machache. Kwanza niipongeze STAMICO kwa kazi inayofanya nzuri kwa sababu uhalisia Mheshimiwa Waziri wa Madini STAMICO ilikuwa inaelekea kufa, lakini baada ya kuingia wameisimamia wakiwa na Balozi Kamanda Sirro, sasa inasimama inafanya kazi vizuri sana. Mimi niwaombe waende wakaongeze nguvu kwa STAMICO ili iweze kuwasaidia wachimbaji wadogo waweze kufanikiwa zaidi katika utafiti na katika mambo yote ili waweze kufanikiwa kupata mali nyingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie jambo moja ambalo linaonekana kama lina changamoto kidogo. Mheshimiwa Waziri kuna kitu kinaitwa VAT leaching plant. Jambo hili ambalo leo linatuletea changamoto kidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba Mheshimiwa Waziri baada ya bajeti yake akatusaidie basi. Mfano watu wanaotokea Chato wanalipa ushuru na Service Levy, watu wale wenye VAT Leaching, lakini kuna sehemu nyingine hawalipi, kuna sehemu nyingine wanalipa fedha nyingi. Tunaomba basi, kama alivyoweka kwenye madini na akatuwekea wazi kabisa, kwa mfano, kama sisi Geita ametuwekea mpaka na TV, ukienda kupima asilimia zako unaziona, hamna wizi; ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri anafanya vizuri. Maana, kama ameweza kutuwekea uwazi huo, tulikuwa tunapoteza, wakati mwingine unapimiwa tu hovyo hovyo, sasa hivi ukifika unapimiwa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, watu wa VAT Leaching tunaomba basi tuwe na kodi moja. Kama tunalipa shilingi laki tano, yaani nchi nzima tulipe shilingi laki tano, kama vile tunavyolipa royalty 8.7% au 9%. Hii double standard inawaumiza wachimbaji na kuongeza malalamiko makubwa. Ninaamini kwa sababu, Mheshimiwa Waziri ni msikivu, mtendaji na mtu anayeshughulika na mambo mengi, tunaamini atatusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninazungumza jambo lingine la mwisho. Sisi wachimbaji wadogo ni wavumbuzi, lakini pia, kuna msemo unasema kwamba, ni wavamizi. Ninamwomba Mheshimiwa Waziri, wale waliochukua leseni, kwa ajili ya uchimbaji wao, sisi Watanzania wote hatuwezi kupata leseni kwa pamoja, lakini wengine tuna mitaji kununua mawe tu; baada ya bajeti yake kupita, ninaamini tutampitishia maana tunamwamini, ataenda kufanya na tutaenda vizuri, akatusaidie wachimbaji wetu wadogo wadogo ambao leo wanaondolewa kila maeneo kwa sababu ya wenye leseni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninamwomba, hawa wachimbaji wadogo, wanapokwenda kuvumbua madini, kama mwenye leseni hataki wachimbaji wadogo wafanye kwenye eneo lake, kwenye leseni yake, basi muda mchache waondolewe, ili wasije wakachimba kwa muda mrefu halafu mwisho wa siku wanakuja kuambiwa ondokeni kwenye eneo hili nyie siyo wenye leseni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukweli usiopingika ma-RMO wanasimamia sheria na wanafanya vizuri. Wakisema kwamba, jamani hili eneo siyo la kwenu ni la mtu amekata leseni, inatuletea changamoto kwa wachimbaji. Ninamwomba Mheshimiwa Waziri, maana anajua na anafuatilia, basi alibebe hili akalifuatilie. Hawa wachimbaji wadogo wanapoanza kuchimba kwenye leseni zao, watu wanaokuja kuchimba kwenye leseni zao, wale wavumbuzi siyo wavamizi. Mtu mwenye leseni awahi kutuambia kwamba, jamani ondokeni hamtakiwi, lakini akichelewa akatuacha wiki mbili, mwezi mzima, tumeingia na gharama, anakuja kutuambia, inatupa changamoto. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu, yapo mambo mengi ya kuzungumzia, ninaomba, Mheshimwa Rais juzi amezungumza, hatuwezi kupeleka hela kwenye Mfuko wa Vijana wote. Sisi, Mheshimiwa Waziri wa Madini, kuna vijana ambao hawawezi kufanya kazi ya kilimo, hawezi kufanya kazi nyingine, kazi yao ni madini. Tumemshuhudia juzi akiwasaidia wachimbaji kupata fedha kutoka Benki ya CRDB. Kwa kweli Mheshimiwa Waziri amefanya vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninamwomba Mheshimiwa Waziri kwa sababu na watu wengine wana leseni ikiwezekana atuletee mpango mkakati atakaosimamia wachimbaji wote waweze kupata fedha katika benki ili wachimbaji wetu waweze kuchimba vizuri. Tunaamini kwa sababu ameanza na kwa sababu atapitishiwa bajeti hii, ninaomba tumwombe aendelee kuzungumza na benki zote, siyo CRDB tu, zipo benki nyingine zinazoweza kutusaidia sisi wachimbaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho. Kuna jambo ambalo linatupa shida sana, la CSR. Waziri amesimamia vizuri sana, pamoja na kwamba, zipo changamoto kwenye CSR, lakini kazi yake inaonekana, anaifanya, CSR zinatoka japo changamoto zipo. Ninamwomba basi, ikiwezekana Mheshimiwa Waziri ... (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Mbunge. Muda wako umekwisha.
MHE. KIJA L. NTEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, basi ninamwombea baraka Mheshimiwa Waziri wa Madini. Mungu amsaidie akayatekeleze haya yote. Tunamwamini akayatende kwa uhakika, maana sisi wachimbaji na mimi ni mchimbaji, tunamwamini sana kwamba atatekeleza. (Makofi)