Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Mwanahamis Athumani Munkunda

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. MWANAHAMISI A. MUNKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nami ninaipongeza Wizara kwa kazi kubwa ambayo wameifanya kwa kweli, hakuna ambaye atapinga kwamba, wachimbaji wadogo nchi hii wamesaidiwa sana. Ni ukweli usiopingika kwamba, wachimbaji wadogo hawa Wizara hii imewabeba sana kupitia STAMICO, lakini pia, ndiyo wamekuwa nguzo kubwa ya uzalishaji mkubwa wa madini ambao uko ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaona kwenye bajeti yake mauzo ya dhahabu nje ya nchi yameongezeka na yameweza kuchangia zaidi ya 52.5%. Mchango huu wa mauzo ya nje unachangiwa na wachimbaji wadogo nchini. Tuwapigie makofi na tuwapongeze sana wachimbaji wadogo wote nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba, wachimbaji wadogo baada ya kuwa wametengewa maeneo yao, wamefanya kazi nzuri sana, ambayo inaonekana. Wamechangia ndani ya nchi yetu, lakini pia, kwenye halmashauri zetu wamechangia sana. Ninamwomba Mheshimiwa Waziri aendelee kutenga maeneo. Juzi tumeona kuna leseni zimekuwa surrendered, basi leseni hizi pia, zigawiwe kwa wachimbaji wadogo ili waendelee kuongeza tija na inachangia pia upatikanaji wa ajira kwa vijana pamoja na wanawake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sekta hii pamoja na mambo mengine yote, imekumbwa na changamoto nyingi sana toka ilipofanyiwa marekebisho mwaka 2017, lakini pia, toka walivyotambuliwa wachimbaji wadogo bado wameendelea kukumbana na changamoto mbalimbali kwenye maeneo yao wanayofanyia kazi. Kwa mfano, kwenye maeneo yaliyorasimishwa ya wachimbaji wadogo bado ziko tozo za halmashauri ambazo ni chechefu, ambazo zimeendelea kuwasumbua wachimbaji wadogo na kuua mitaji yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, uchimbaji mdogo ni sawasawa na wajasiriamali wengine wote ambao wamekuwa wakipewa mikopo ya 10% kwenye maeneo yetu ya halmashauri. Wamekuwa pia, hawapati usimamizi mzuri, hasa wanapopata changamoto za tozo, za ushuru, kwenye halmashauri zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, mchimbaji mdogo huyu amepewa leseni ameanza kuchimba, lakini amepewa leseni hii bila hata kufanyiwa just a basic simple geological, geophysics. Ameanza kuchimba kwa mtaji wake, anamaliza kuchimba, aende sasa kufanya uchenjuaji anakutana na tozo ya mawe; hili Mheshimiwa Waziri liko pale kwenye Mgodi wetu wa Mwakitolyo. Kila mfuko mmoja wa mawe anaotoa mchimbaji mdogo anatozwa 1,000 mpaka 2,500, lakini tozo hizi, Mheshimiwa Waziri, zinakinzana na Sheria Mama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa mfano, ili aweze kuzalisha kilo moja ya dhahabu, mchimbaji mdogo huyu, anahitaji kuwa na mawe zaidi ya tani 12,000. Kwa hiyo, ina maana hata kabla hajaanza uzalishaji anapaswa kulipa halmashauri shilingi milioni 12, tozo ambayo ni kinyume kabisa na Sheria ya Madini. Tunamwomba Mheshimiwa Waziri, ninajua halmashauri pia zinakusanya mapato, wakakae chini wafanye harmonization, ili waweze kujua ni tozo zipi basi halmashauri wanatoza kwa sababu, mwisho wa siku ametozwa mawe anakwenda, akichenjua kwa kukamatisha na mercury anatengeneza rundo, anakuja tena kutozwa rundo hilo, wakati analisafirisha kwenda kwenye uchenjuaji wa CIP. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mzigo huo huo pia, akimaliza uchenjuaji akienda kwenye elution, anakwenda sasa kulipa zile tozo ambazo zinatakiwa kwa mujibu wa kanuni, sheria na taratibu. Ana Service Levy halmashauri, ana mrabaha na tozo nyingine nyingi ambazo zipo kwenye Sheria ya Madini. Ninaomba Mheshimiwa Waziri, awasaidie wachimbaji wadogo, hela zao wakichimba, wakizalisha, tunaziona nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo mengi ambayo wachimbaji wadogo wamechimba, uzalishaji wake na faida tumeiona ndani ya nchi yetu. Kwa hiyo, tunaomba sana wasaidiwe kwenye maeneo hayo, ili kupunguza double taxation kwa wachimbaji wadogo. Hiki kimekuwa ni kilio chao na hasa wachimbaji wanawake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni tumeona na ninawapongeza pia, Wizara baada ya kuanzisha hii Kanuni ya Msaada wa Kiufundi. Kanuni hii ya ilitangazwa kwenye Gazeti la Serikali mwaka jana tarehe 25 Aprili, 2025. Ni sheria nzuri ukiipitia, lakini kanuni hizi zimekuwa kichaka cha kuwanyonya wachimbaji wadogo. Ni sawasawa tumemgeuza mchimbaji mwenye leseni anatakiwa apate 30% na yule anayekuja kutoa technical support anatakiwa apate 70%.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kwa jicho lingine unaiona kama ni free carried interest, 70%, anachukua huyu. Huyu anayetoa technical support wengi kwa kweli, ni Wachina; miaka 10 ijayo, miaka 20 ijayo, nchi hii leseni zote za wachimbaji wadogo kwa kisingizio cha kutoa technical support zitakuwa zinafanywa na wageni kutoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ile essence na maana ya kuwapa ajira wachimbaji wadogo na hasa wanawake na vijana, inapotea kwa sababu, ukiangalia kabisa kwa lile jicho la tatu, 30 kwa 70 ni sawa sawa tunampa free carried interest ya 70%. Tujiulize, hivi hii technical support ni ipi? What is the definition? Nini maana ya technical support? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia definition ya technical support ni utafiti ambao Wizara, kwa kupitia GST, wangefanya basic geophysics. Wachimbaji wadogo wakajua tu umbali wa mwamba wa mali ulipo, wakaacha kuchimba kiholela na kupiga ramli ambazo ni chonganishi, wala tusingehitaji technical support.

Mheshimiwa Naibu Spika, kamekuja pia haka kamtambo kanakoitwa CIP, wanakujanako sana hawa wanaokuja kutoa technical support. Tuna vyuo vyetu humu ndani, tuna chuo chetu, tuna wataalam wetu, wako humu ndani, kutoka UD na kutoka maeneo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati anakuja kuhitimisha hoja yake Mheshimiwa Waziri...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. MWANAHAMISI A. MUNKUNDA: ...atupe maana ya hii technical support, ili kuwasaidia wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana. Sitaunga mkono hoja mpaka atakaponijibu jambo hili. Ahsante. (Makofi)