Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kahama Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BENJAMIN L. NGAYIWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia katika bajeti hii ya Wizara ya Madini. Niendelee kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Kahama Mjini kwa kuendelea kuchapa kazi na kusadifu ile kaulimbiu ya Mheshimiwa Rais ya kazi iendelee.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninawapongeza Wizara ya Madini na kaka yangu Anthony Mavunde, kwa kazi nzuri ambayo wameifanya. Tumeona katika taarifa yao, uzalishaji wa madini katika nchi yetu umeongezeka na mchango wake katika pato la Taifa umeongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kutokea mwaka 2023 mchango wa sekta ya madini umechangia kwa asilimia 9.1, mwaka 2024 umechangia kwa 10.1% na mwaka 2025 umechangia kwa 11.9%. Hii tafsiri yake ni nini? Tafsiri yake ni kwamba tukiwa na utashi wa kusema kwamba tufanye exploration nzuri katika sekta hii ya madini itaenda kufikia hata kuchangia kwa 50% ya pato la Taifa na twende tumpunguzie mzigo mwananchi wa kawaida kwa kumtoza kodi nyingi wakati tuna resources nyingi sana katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiangalia hadi kufikia mwezi Machi, 2026, kati ya lengo la kukusanya shilingi trilioni 1.4 Wizara ya Madini imekusanya shilingi trilioni 1.03, hii ni tafsiri nzuri na ni mwendelezo mzuri sana katika nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona mpango mkakati wa Wizara ya Madini katika kuongeza tija na thamani ya madini katika nchi yetu. Tumeona kwamba wanataka kuiwezesha STAMICO, lakini pamoja na kuiwezesha GST katika kufanya survey kwa kurusha hizi ndege nyuki kwa maana ya drones ili ziweze kufanya utafiti ulio mzuri na kuweza kuwapatia wananchi wetu na wawekezaji wengine maeneo mbalimbali ya kufanya uchimbaji wao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona hadi kufikia Machi, 2026, Wizara ya Madini imegawa karibu leseni 11,674. Hapa ninaomba niweke wazi suala moja kwamba ugawaji wa leseni uendane na kuendeleza vitalu hivi au leseni hizi za madini, kwa sababu gani? Kwa sababu hawa watu wanaochukua hivi vitalu na leseni za madini wanazichukua na wanaanza kuwa wanalipia zile kodi za kila mwaka, lakini hawafanyi mwendelezo. Sheria ya Madini ya Mwaka 2023 inasema, unapopata leseni ya kuchimba madini uanze kuifanyia kazi miezi mitatu tangu tarehe ya kupewa leseni hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hawa watu wanachukua, wanalipia tu kodi halafu wachimbaji wadogo wakienda wakipata madini wanafukuzwa, wanaambiwa hapa tunataka ibaki miti na ndege. Hii siyo haki na nimwombe Waziri wa Madini, nimemsikia juzi hapa amefuta baadhi ya leseni. Ninaomba hapa hata ile Tume ya Madini, isiwe kazi yake kugawa leseni tu, izifuatilie na kuona kwamba zinaendelezwa, kama haziendelezwi zichukuliwe zirudishwe chini ya Serikali au wapewe vyama vya ushirika kule katika kata na vijiji vyetu ili wananchi wetu wapate mahali pa kwenda kufanya shughuli za kuchimba madini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, juzi hapa katika Wilaya yangu na Jimbo langu la Kahama wananchi wameenda wamevumbua sehemu madini, lakini baadaye wakaambiwa hapa ni kwa mwekezaji. Ni kweli kuna mwekezaji lakini tuwaangalie hawa wananchi nao kuwapatia maeneo ya Serikali ambayo wanaweza wakaenda wakachimba na kuendeleza kipato chao. Kwa sababu sekta ya madini hii kule Kahama na kanda ya kule ndiyo uchumi wa kule wa kwetu, sasa wananchi wanapokosa maeneo ya kuchimba kwa kweli tunakuwa hatuwatendei haki wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hawa watu wenye leseni wanapozipata hizo leseni na madini yakapatikana pale wanaingia joint venture, mikataba na wawezeshaji. Kwenye Sheria ya Madini ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, imesema ni wawezeshaji siyo wawekezaji. Kwa hiyo, wanakuja hawa ndugu zetu kutoka Bara la Asia, Wachina wanakuja hapa na teknolojia yao, pale Kamati ya Madini imesema wanaenda kuboresha teknolojia ya Vat leaching na CIP. Hata hivyo, ninataka nikwambie kuna teknolojia inaitwa heap leaching, hii inafanywa na wawezeshaji hawa wa Kichina, wanakuja na teknolojia hii ambayo hawakubali kuipeleka na kuifundisha kwa wazawa ili na wao waweze kupata tija katika uchenjuaji wa madini ya dhahabu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa sielewi Tume ya Madini na hawa wenzetu wa NEMC wanaijua hiyo teknolojia na hizo zote chemicals zinazotumika katika kuchenjua dhahabu au hawajui? Environmental conservation inafanyikaje? Ninaomba sana teknolojia transfer kwa mujibu wa local content katika Sheria yetu ya Madini, iende ikasimamiwe, tusilete Wachina wanatuachia mabonanza, yale madude ya kwenda wanaweka kwenye baa, watu wetu wanaanza kucheza kamari zile za kuweka shilingi mia mbili, mia mbili, anakuja jioni anakusanya, anapata mtaji, anafanya madini, hana mtaji, hana chochote, twende tukaliangalie hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii mikeka tunayo-bet ya Wahindi, tunatandika mikeka inatutosha, haya mabonanza, kwanza hata mapato yake sijui yanasimamiwaje katika Halmashauri zetu kule, kwa sababu sijaona sehemu yoyote wameweka kama chanzo cha mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii sekta ya madini kwetu kama nilivyosema ndiyo uchumi wa maeneo yetu na Majimbo yetu ya kule. Ninamwomba sana Waziri Mavunde, hizi leseni ambazo haziendelezwi zichukuliwe zirudishwe Serikalini, wapewe wachimbaji wetu wadogo, waweze kufanya shughuli za uchimbaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa kuna Vyama vya Ushirika, kwa mfano kuna hiki chama cha ushirika kinaitwa Tanzania National Miners…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Mbunge, tunashukuru kwa mchango wako muda wako umekwisha.
MHE. BENJAMIN L. NGAYIWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana, sitaunga mkono hoja mpaka nipate maelezo hayo kwa mujibu wa maelezo ya wananchi wangu. Ahsante sana. (Makofi)