Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nanyumbu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi mchana wa leo ili kuchangia bajeti hii ya Sekta ya Madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote ninaomba nichukue nafasi hii nimshukuru sana Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema ambaye ameniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako hili Tukufu kutoa mchango wangu katika Wizara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, wachangiaji wengi wametoa sifa nyingi sana kwa sekta hii au Wizara hii ya madini na ninaomba niungane nao, ninamshukuru sana Waziri, Watendaji wote kwa kazi nzuri waliyoifanya katika sekta hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, sote ni mashahidi katika ripoti ya Mheshimiwa Waziri ameeleza kwa kina jinsi gani sekta hii inavyochangia uchumi wa nchi yetu. Imeelezwa kwamba ni sekta ya pili katika uchangiaji wa pato la Taifa; na kwa figure ambazo amezieleza kila mwaka kutoka mwaka wa fedha 2023/2024 na mwaka wa fedha 2025/2026 hadi mwezi Machi sekta hii inaendelea kukua na kukua; na inaonekana kwamba karibu 11.9% imeongezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, cha kufurahisha zaidi ni ukusanyaji wa maduhuli ambao unakwenda moja kwa moja Hazina. Sekta hii ukiangalia kila mwaka nayo inafanya maendeleo makubwa sana. Ukiangalia mwaka jana mwaka wa fedha 2023/2024 sekta hii ilikusanya shilingi milioni kama 900 hivi ambazo zilikwenda Hazina. Mwaka wa fedha 2024/2025 fedha zimeongezeka na kufika karibu bilioni moja pointi something. Kwa hiyo utaona kabisa kwamba ongezeko la takriban 49% kwenye sekta katika ukusanyaji wa maduhuli limefanyika katika Wizara hii ya Madini, hongera sana kwa ndugu zangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni udhibiti na usimamiaji wa utoroshaji wa madini. Wameonesha jinsi gani sekta ya madini kwa kushirikiana na Serikali wameweza kudhibiti watoroshaji wa madini. Tumeweza kuona bilioni 3.3 zimeweza kudhibitiwa, madini yenye thamani hiyo hayakuweza kuondoshwa na yamezuiliwa. Ninawapa hongera sana kwa kufanya kazi nzuri sana kwa kuzuia madini haya ambayo yalitakiwa kutoroshwa nje ya utaratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninawapongeza sana Tume ya Madini, taasisi ambayo iko chini ya Wizara ya Madini, pamoja na STAMICO. Zimefanya kazi nzuri sana kwa kutoa leseni. Kwa upande wa Tume ya Madini takriban leseni 8,000 zimetolewa; na STAMICO imefanya majukumu yake kikamilifu kwa kufanya utafiti, kutoa mafunzo jinsi gani ya kuchimba, kuchenjua, kuangalia hifadhi ya mazingira na kadhalika. Kwa hiyo hongera sana sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, ninawapongeza sana Wizara, wameeleza pale kwamba hadi sasa hivi tunazo kampuni sita ambazo zinashughulika na refining ya dhahabu. Kwa kweli hili jambo ni la kujipongeza sana. Ni kampuni za Kitanzania; na moja ya kampuni hizi kuna kampuni ambayo inaongozwa na mwanamama inafanya kazi vizuri sana. Hongereni sana Wizara kwa kuhakikisha kwamba sekta hizi za watu binafsi, za wazalendo zinashiriki kikamilifu katika uchumi wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, rai yangu kwa Mheshimiwa Waziri, hizi sekta binafsi ambazo zimeshughulika katika kuanzisha refining za dhahabu zetu je, zinazo ithibati? kama zinazo au hazina, Wizara ihakikishe kwamba zinapata ithibati ili ziweze kutambulika kimataifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo ninaomba pia nichangie katika changamoto ambazo zipo, hususan katika jimbo langu. Ndani ya Jimbo la Nanyumbu tunayo pia madini ya dhahabu. Wananchi wa kule wanakumbana na changamoto zifuatazo; ninaomba Mheshimiwa Waziri anisaidie jinsi gani ya kukabiliana na changamoto hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tumezungukwa na Hifadhi ya Lukwika Lumesule; na ndani ya hifadhi ile kuna madini ya dhahabu. Ule ni ukanda kutoka Msumbiji ambao unaingia hadi katika nchi yetu; tunayo madini ya dhahabu lakini madini yale yanashindwa kuchimbwa kwa sababu watu wa TFS na watu wa TAWA ni vizingiti vikubwa, hawaruhusu vijana wetu kwenda kuchimba. Sasa ninaomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja atueleze; je, sisi watu wa Nanyumbu tuwe waangalizi tu wa yale madini au kuna utaratibu ambao unatakiwa ufanywe ili wananchi wale waweze kunufaika na madini hayo?
Mheshimiwa Naibu Spika, leo ukienda Ushirombo kuna utaratibu mzuri sana umeandaliwa; wananchi wameweza kwenda katika hifadhi, wamechimba madini na hifadhi ya mazingira inaendelea kulindwa. Kwa hiyo ninaomba utaratibu ule nao ukatumike kwa wananchi wa Jimbo langu la Nanyumbu ili vijana waweze kunufaika na madini hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi watu wa Nanyumbu tulikuwa na kituo cha uuzaji wa dhahabu; tukafanya sherehe kubwa kwenye ufunguaji wa kituo kile, lakini leo kituo kimefungwa bila taarifa yoyote. Ninaomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atueleze ni lini kituo kile kinafunguliwa? Vijana wanahangaika wanakwenda kilomita 54 kwenda kuuza dhahabu zao ilhali tulikuwa na kituo ndani ya jimbo letu. Ninaona kwamba hii si sawa kile kituo kufungwa. Ninaomba kile kituo kifunguliwe ili vijana wetu waweze kunufaika na madini hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo ningeomba sana, watu wetu wa STAMICO waje kule watoe mafunzo kwa vijana wetu. Vijana wanahitaji mafunzo. Inaonekana kama suala la madini kuna ukanda fulani ambao ndiyo unatiliwa maanani; sisi watu wa huku ndiyo tunaojikokota; hebu na sisi watunyanyue, watu wa STAMICO…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Yahya.
MHE. YAHYA A. MHATA …waje kusini kutuletea elimu na vijana wetu waweze kuchimba madini hayo na kupata faida.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja. Ahsanteni sana. (Makofi)