Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi jioni ya leo ili nichangie katika Wizara hii ambayo tunaisimamia kwa niaba ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Taarifa yetu tumeiwasilisha na maoni yetu hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda nimpongeze kwa dhati Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ya kuiletea mapinduzi sekta hii ya madini. Hakika takwimu zilizowasilishwa leo, taarifa iliyowasilishwa kwa kina, mafanikio katika kila aina ya kidunia, ngazi ya Afrika na hapa nchini yanatafsiri uthubutu, ujasiri na uchapakazi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Naibu Spika, kana kwamba haitoshi Waziri, Mheshimiwa Mavunde pamoja na Naibu Waziri, Wakuu wa Taasisi zote chini ya Wizara hii, Wenyeviti wa Bodi wote, watumishi wote wa taasisi zote; lakini pia kubwa Maafisa Madini wote wa Mikoa lakini na wadau wote wa sekta hii ya madini ambao wako leo hapa kushuhudia bajeti hii; na kwa kweli kila ukiongea na wadau hao wanamshukuru kwa ushirikiano, kwa usikivu wake. Kuelekea bajeti tumeona namna alivyokutana na makundi mbalimbali ili kuwasikiliza mafanikio yao na changamoto zao. Hongera sana kwa Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu utakuwa mfupi. Kwanza, Mheshimiwa Waziri katika taarifa hii ametuelezea mwenendo wa biashara ya madini duniani. Katika mwenendo huo pia amegusia kuhusu mwenendo wa biashara ya Tanzanite yetu, madini maalum ambayo yanapatikana hapa nchini kwetu Tanzania na kwamba hakuna soko la uhakika na pia thamani yake imeshuka.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na sababu hizo nimwombe Mheshimiwa Waziri, kama ambavyo amekuwa akiwasikiliza wadau; yeye pamoja na Naibu Waziri wake, zipo changamoto ndani ya mfumo wetu wa ndani ya nchi, ikiwemo utaratibu wa kuhakikisha kwamba madini yale hayauzwi nje ya eneo ambalo yanapatikana; jambo ambalo limeonyesha kusababisha kushuka kwa thamani na pia kukosekana kwa ajira. Vilevile limesababisha baadhi ya mashine za kuongeza thamani ya madini hayo nyingi hazitumiki na zimesababisha kuwepo kwa gharama kubwa kwa wachimbaji na wanunuzi wa madini hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Waziri, kwa sababu hili ni la kikanuni na sheria na amekuwa hodari; hata kwenye bajeti hii ameainisha namna walivyofanya maboresho ya Sheria ya Madini Kifungu Namba 123; sisi Kamati kwa niaba ya Bunge tuko tayari kushirikiana naye kufanya mapitio ya sheria na kanuni mbalimbali ambazo zitaleta mchango mkubwa wa madini tuliyokuwa nayo hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilisema, kwamba kazi nzuri ya Mheshimiwa Dkt. Samia na kwa usaidizi wa karibu wa Mheshimiwa Mavunde na Naibu Waziri inaonekana kupitia takwimu; makusanyo ya trilioni 1.43. Tangu Mheshimiwa Mavunde amekabidhiwa Wizara hii na msaidizi wake yeye ni kukusanya trilioni moja na kuendelea, ninawapongeza sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe Wizara ya Fedha kuendelea kuipatia fedha Wizara hii ya Madini; hususan za maendeleo. Bilioni 10 iliyoipatia hata mpaka Machi mafanikio yake ni trilioni moja na pointi tatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sekta hii ni kama ng'ombe aliyenona; ili umkamue vizuri mwezeshe kupitia GST, Tume ya Madini, STAMICO na TEITI kwa kuwapelekea fedha zao za maendeleo. Tume ya Madini inahitaji magari 24 na tunahitaji ndege. Mchakato umeanza, nchi hii inakwenda kupima 18%, tulipo sasa ni 16% ambazo ni tangu tumepata uhuru; lakini Dkt. Samia Suluhu Hassan anakwenda kuweka rekodi mpya ya kutaka kuipima hadi kufikia 18%. Ufanyike utafiti wa kina, tuainishe madini mengine ya kimkakati na muhimu kama ambavyo mahitaji yameongezeka duniani.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaamini Waziri wa Fedha hatashindwa kuipatia Wizara hii; kama ambavyo Kamati ya Uongozi kupitia Kamati ya Bajeti iliamua bilioni 28 tu. Wao wamekusanya trilioni moja, wamewapatia bilioni 82; maana yake wamepeleka fedha nyingi zaidi; niiombe sana Wizara ya Fedha, hiki ni chanzo cha uhakika; kisaidie kufanya utafiti wa kina tubainishe madini yako wapi, tuendelee kuwavutia wawekezaji zaidi kama kazi nzuri inayofanywa na Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nimalizie kwa kumpongeza kwa dhati kwa namna ambavyo kwa mara ya kwanza Serikali hii ya Awamu ya Sita imejenga kiwanda kwenye sekta ya chumvi kule Kilwa. Ameifanya sekta ya chumvi kutulia. Pia sisi Bagamoyo maeneo ya Kitame tunao wadau wa chumvi wamempongeza sana. Sisi Bagamoyo tunayo madini ya ujenzi kupitia Halmashauri za Chalinze na Bagamoyo. Ombi langu, ashirikiane na sekta nyingine ikiwemo miundombinu ya barabara ili maeneo yapitike na madini yaendelee kutoka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mchango huu ninaunga mkono hoja na hongera sana.