Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Asia Abdulkarim Halamga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nichangie katika bajeti ya Wizara ya Madini kwa mwaka 2026/2027. Nianze kuchukua nafasi hii kumpongeza sana Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuhakikisha anakuwa kinara wa kuhakikisha kwamba anazibeba sekta zote ili ziendelee kutoa nafasi ya uchumi na kutoa nafasi ya ajira kwa Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kuendelea kumpongeza kwa moyo wa dhati kabisa Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Peter Mavunde, Naibu wake, Katibu Mkuu na timu nzima ya Wizara ya Madini. Ameendelea kuwa kielelezo kwa sisi vijana wa Kitanzania. Akipewa nafasi anaweza kuwasaidia Watanzania wenzake.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kuendelea kuhakikisha kwamba anaendelea kuilinda na kufanikisha dhamira njema ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuendelea kutoa ajira na kuleta tabasamu kwa Watanzania. Mheshimiwa Waziri amekuwa ni kielelezo katika Wizara zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kuipongeza sana Wizara hii ya Madini, kwa sababu ukiingia katika Afrika leo Tanzania tunaweka historia kuwa wa nne katika uwekezaji wa sekta ya madini kutokana na mazingira bora. Mazingira haya bora ya kiuwekezaji hayajaja kwa bahati mbaya, yamekuja kwa sababu tuna nchi iliyotulia, tuna Rais ambaye anavutia wawekezaji, nchi ipo salama; na ndiyo maana leo tunajivunia kuwa nafasi ya nne ukiachana na Botswana ya kwanza, Morocco ya pili na Zambia ya tatu. Tunaiweka historia ya Tanzania kushika namba nne katika Bara la Afrika. Hii ni kazi kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuipongeza Wizara hii. Tumemwona Mheshimiwa Waziri hivi karibuni. Ameendelea kuwaona akina mama na vijana. Akina mama wa Tahoma ni hivi karibuni tumemshuhudia ametoa mashine za pampu zaidi ya 10 kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wanawake wanaendelea kuinuka katika sekta hii ya madini. Bado haitoshi, kuna watu ambao walikuwa wanazichezeachezea leseni (PL) Mheshimiwa Waziri amezichukua; zaidi ya leseni 40; amezirejesha Serikalini kwenye Wizara ya Madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuzichukua leseni hizi hakwenda kuziweka Wizarani zikae kama mzigo, bali azipeleka huko kwa vijana wa Kitanzania na kwenda kutoa ajira kwa vijana, akina mama pamoja na Watanzania wa kawaida. Hongera sana kwa Mheshimiwa Anthony Peter Mavunde, Waziri wa Madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna ng'ombe anayeweza kutoa maziwa bila majani. Tunapoongelea Wizara ya Madini ni Wizara ya pili ya kimkakati kwa Nchi yetu ya Tanzania inayoingiza fedha za ndani pamoja na fedha za kigeni. Hakuna namna yoyote; hapa tunaongea na Mheshimiwa Waziri wa Fedha, ni lazima tuwekeze katika sekta ya madini, tuwape fedha za kutosha ili twende sasa kwenye utafiti.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninasema hivi kwa sababu tulichokiona na kukigundua, ardhi ya Tanzania karibu kila sehemu kuna rasilimali za madini. Tuna madini ya kila aina. Kwa hiyo ni lazima sasa tujikite kutoa fedha ili kuweza kufanyika utafiti wa madini yaliyopo na pia kugundua madini mapya kwa sababu ardhi yetu ina madini ya kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kumwomba sana Mheshimiwa Waziri; kwenye Tanzanite tunaomba atusaidie. Tunajua hali ya kidunia, lakini tutafute namna ya kulinda Tanzanite kwa sababu ni kitu cha kidunia na kimeporomoka bei na pale kuna Watanzania ambao ni biashara yao ya kila siku. Sasa ajira zimeanza kupungua.

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kumpongeza kwa kuendelea kutoa leseni kwa zaidi ya vikundi 21 pale Mji wa Mererani, Wilaya ya Simanjiro.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi watu wa Mkoa wa Manyara tuendelee kumpongeza Mheshimiwa Waziri. Nje ya Tanzanite ameendelea kumulika kwa jicho la kipekee kuona na maeneo mengine ikiwemo Hanang’, Mbulu na Babati Vijijini yanakuwa ni fursa kubwa ambazo zitakuja kuwasaidia vijana wa Kitanzania. Jimbo la Hanang tunayo chumvi ya kutosha. Rasilimali ile ni rasilimali ya Watanzania. Nimekwishaiongelea hapa toka nikiwa Mbunge wa Viti Maalum; lakini sasa ninaomba Mheshimiwa Waziri alibebe hili na hatimaye ile chumvi ya Hanang iweze kutoa ajira kwa vijana wa Hanang pia vijana wa Kitanzania na kuleta fedha za ndani pamoja na fedha za kigeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuchukua nafasi hii kusisitiza wawekezaji wote kuendelea kutoa CSR zinazostahili. Wanatuachia mashimo, fedha wanazozichangia ni chache sana. Tuombe sana Mheshimiwa Waziri asimamie kwenye hili ili fursa hii adimu na adhimu katika Taifa letu la kupewa madini, Mwenyezi Mungu ametubariki, lazima tuone sasa tunaingiza pato, lakini watu hawa wanapoondoka na manufaa, basi waweze pia kutuachia manufaa na sisi, kwa maana ya kupata huduma za afya, maji na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kuendelea kusisitiza hasa kwenye suala la utafiti. Ni lazima tuongeze utafiti kwa nguvu zetu zote ili tuendelee kuona kwamba sekta hii inaendelea kutoa pato la Taifa kupitia fedha za kigeni pamoja na fedha za ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara hii imeendelea kutoa mazingira mazuri; na hapa niendelee kumpongeza Dkt. Samia Suluhu Hassan; zamani ilikuwa mtu ukisikia unaenda kwenye madini inaonekana moja kwa moja unaenda kutapeliwa na inawezekana ukakaliwa kikao cha ukoo; lakini kwa sasa sekta ya madini unaona kila mtu anaikimbilia. Inaweza kuwa na tija kwa mwananchi mmoja mmoja na itakuwa na tija kwenye pato la Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa anayoifanya kwa vijana na akina mama wa Kitanzania. Niendelee kuomba, suala la utafiti ni suala muhimu ili tuweze kuwasaidia vijana, akina mama na wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi na ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)