Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. REGINA H. MIKENZE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ili niweze kuchangia katika hotuba hii ya Wizara muhimu kabisa ya Madini, ninakushukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaendelea nitumie nafasi hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ambazo anazifanya na kwa kazi nzuri ambayo anaifanya katika sekta ya madini; ninampongeza sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo moja ambalo nisipolisema nitaona sijaendelea haki, ambalo ninapenda kumpongeza, ni jambo la uwekezaji wa Mfuko kwa ajili ya vizazi vijavyo. Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipokuwa akihutubia Bunge hili Tukufu alisema kwamba katika uongozi wake atahakikisha katika sekta ya madini ataweka Mfuko kwa ajili ya vizazi vijavyo. Alisema kuwa madini siyo mahindi kwamba tukivuna tutapata mbegu tena ya kupanda upya; kwa hiyo vizazi vijavyo visije vikakuta mashimo tu na visipate faida yoyote. Kwa hiyo katika hili ninampongeza sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, maandiko matakatifu katika Kitabu cha Mithali, Sura ya 13 mstari wa 22 unasema: “Mtu mwema huacha urithi kwa wana wa wanaye.” Rais Samia Suluhu Hassan ni Rais mwema, ni Rais anayejali kizazi kijacho ndiyo maana anawekeza kwa vizazi vijavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii pia kumpongeza Waziri wa Madini, kaka yangu Anthony Mavunde kwa hotuba nzuri aliyoitoa siku ya leo. Kimsingi nilikuwa na maswali mengi na mambo mengi najiuliza, lakini kwa hotuba yake amejibu mambo mengi, amenifilisi kwa kina. Kwa hiyo ninawapongeza sana yeye pamoja na Naibu wake na wasaidizi wake ambao wanamsaidia katika Wizara hii ya Madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, nami nijielekeze sasa katika mchango wangu. Mimi ni Mbunge kutoka katika Mkoa wa Geita ambako tunachimba madini. Siku ya leo ningependa kuwasemea wanawake wa Mkoa wa Geita. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili tena sitasita kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia amefanya jambo kubwa la kukumbukwa. Katika miaka yake minne, ametoa leseni zaidi ya 80 kwa wanawake wa Mkoa wa Geita pamoja na vikundi mbalimbali vya wanawake. Tunampongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hilo sasa kuna changamoto ambazo zimejitokeza. Wanawake hawa wamelipokea hili kwa mikono miwili na wamenituma nije nimshukuru. Pamoja na shukrani zao, wanaomba wasaidiwe mitaji kwa ajili ya uchimbaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiwa wakweli kuna mikopo mingi ambayo inatolewa kwa ajili ya wanawake. Kuna mikopo ya 10% kwa wanawake, lakini ni mikopo ambayo haiwezi kuwa na tija katika sekta ya uchimbaji. Sekta ya uchimbaji inahitaji mikopo mikubwa sana, inahitaji kununua mashine kubwa, mitambo mikubwa na mashine za kuchenjua. Kwa hiyo, kwa mikopo hii midogo midogo ambayo inatolewa haiwezi kuleta tija katika uchimbaji na haiwezi kumkomboa mwanamke mchimbaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ili tumsaidie mwanamke ili tuweke legacy ya Mama Samia ambaye amekwenda kuwasaidia wanawake waingie katika uchimbaji wa madini katika Mkoa wa Geita; niombe kuishauri Serikali na Wizara hii ya Madini. Niombe tuige model kama ile ya sekta ya kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika sekta ya kilimo nilisoma katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu alisema kwamba, Serikali iliweka vituo 79 na ikanunua matrekta 360 na ikasambaza matrekta hayo katika vituo mbalimbali ili kuwawezesha wakulima walioko katika maeneo mbalimbali waweze kupata vifaa kwa gharama ndogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ningeomba model kama hii itumike katika migodi midogo midogo ili kuwasaidia wanawake wachimbaji na wachimbaji wadogo wadogo wakiwemo na vijana. Inunuliwe mitambo na mitambo hiyo iwekwe katika vituo mbalimbali au migodi hii midogo midogo ambayo wanashiriki kuchimba hao wanawake, vijana na wachimbaji wengine wadogo wadogo nao wapewe ikiwezekana kwa gharama ndogo kama ambavyo inafanyika katika kilimo, iwasaidie kushiriki na kupata uchimbaji wenye tija. Ninaamini kwa kufanya hivyo, tunakwenda kupata mabilionea wengi katika Mkoa wa Geita. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Geita ni mkoa wa matajiri. Katika wilaya zote za Geita kote kuna migodi na wanawake pamoja na vijana wamehamasika katika uchimbaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo tunahitaji pia kusaidiwa, au wanawake wanahitaji kusaidiwa, wanawake wachimbaji ni katika utafiti. Ni ngumu sana kwenda kuchimba uchimbaji wa madini katika karne hii ya sayansi na teknolojia uchimbaji wa kubahatisha…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Malizia muda wako umekwisha.
MHE. REGINA H. MIKENZE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninaomba wanawake wasaidiwe gharama za utafiti ili waweze kuchimba uchimbaji wenye tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru na ninaunga mkono hoja. (Makofi)