Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Msalala
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MABULA J. MAGANGILA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Niungane na wenzangu kuwapongeza sana Wizara ya Madini, Mheshimiwa Mavunde na Mheshimiwa Kiruswa. Kwa kweli hotuba hii ya leo ni nzuri sana na kwa kweli inatoa matumaini makubwa sana kwa wachimbaji wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Kahama ambapo kwa madini ni mkoa wa kimadini, katika leseni 1,640 leseni 840 zinapatikana Jimbo la Msalala za wachimbaji wadogo. Katika leseni 70 za utafiti, leseni 32 zinapatikana Jimbo la Msalala, lakini Jimbo la Msalala lina kata 18, kata 12 ni za wachimbaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Msalala ukizungumzia kwenye uzalishaji wa madini katika mkoa wa kimadini wa Kahama, tunazalisha mpaka kuanzia mwezi wa saba mpaka mwezi wa tatu tani 1.7 zimezalishwa katika mkoa wa kimadini wa Kahama, tani 1.3 zimetoka Msalala. Kwa upande wa makusanyo Serikalini, Serikali imekusanya shilingi 135,000,000,000 katika Mkoa wa Kimadini wa Kahama, shilingi 110,000,000,000 zimetoka Msalala. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia adha wanazopitia wachimbaji katika Jimbo la Msalala, endapo zikitatuliwa wanaweza kuzalisha mara mbili ya hiki ambacho tumekusanya. Katika Jimbo la Msalala tunazalisha miezi minne kwa nusu uzalishaji hasa katika msimu wa mvua.
Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake barabara zetu kule hazipitiki, ukiangalia tunazo barabara kama saba ambazo hizi peke yake ndizo zinazochangia haya mapato yote ambayo tumeyaleta hapa. Barabara hizo ni Segese - Jomu, Lunguya namba tisa, Nyambula - Chela na Masavi – Chela. Hizi barabara zikiweza kupitika misimu yote tunakwenda ku-double huu uzalishaji ambao tunaufanya kwenye Jimbo la Msalala. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, zipo changamoto ambazo zimeibuka. Tunaishukuru sana Wizara ya Madini kwa kuendelea kusimamia sekta hii, lakini tuna changamoto za wenye mashamba, wachimbaji wadogo wenye maduara, lakini wenye leseni. Tayari suluhisho limekwishapatikana kwa wachimbaji wenye maduara pamoja na wenye leseni, lakini tunaomba sasa sheria yetu iende ikawatambue wenye mashamba, ili mtu anapoomba leseni kwenye mfumo ikiwezekana apewe kwa 80%, 20% ibaki kwa wenye mashamba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, sisi hapa kwa wachimbaji wakubwa, tuna 16% inabaki kwa ajili ya Taifa letu. Kwa nini kwa wachimbaji wadogo tusiweke angalau 20% au hiyo hiyo 16% ibaki kwa wenye mashamba? Ili mtu anavyokwenda kuwekeza, either lile eneo liwe la kwake amelinunua ama aende akaingie ubia na wenye mashamba.
Mheshimiwa Naibu Spika, ikiwezekana wenye mashamba waunde vikundi ili wamiliki pamoja leseni ili kuondoa migogoro. Sasa hivi tunayo migogoro kwenye maeneo yetu. Tunao mgogoro Mheshimiwa Waziri anaufahamu, mgogoro wa Busulwangili unaendana na hizi hizi changamoto. Mgogoro wa Mwakata unaendana na hizi hizi changamoto, kwamba unakuta anayeomba leseni, anaomba leseni akiwa Dar es Salaam hajui leseni anayokwenda kupatiwa tayari kule walishaanza kuchimba miaka miwili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, akija kupewa leseni huku yeye anakwenda pale, anavyoanza kuwafukuza; mtu alikuwa anapata mgao kama mmiliki mwenye shamba, anapata mgao wa shilingi 200,000,000 au shilingi 300,000,000 kila mgao unapofanyika, wanauza mawe, kila mgao unapofanyika anapata mgao, leo unakwenda kumkadiria heka moja shilingi 800,000 kwa sheria ya ardhi. Lazima mgogoro utaibuka tu kwa namna yoyote ile. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunazungumza Jimbo la Msalala lina kata 18, kata 12 ni za wachimbaji. Hizo kata zote zikiwa na migogoro hilo jimbo litakuwaje? Tutakaa kila siku tunatatua migogoro kwenye hilo eneo. Niombe tuwatambue wenye mashamba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi lingine, Mheshimiwa Waziri ninaomba sasa leseni hizo ambazo tumezifuta, tukawagawie vijana wetu na akina mama ili waweze kuendeleza leseni hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)