Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sikonge
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza nichukue nafasi hii kukushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia. Awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu ambaye ameendelea kutupa uzima na afya, hatimaye umefika muda na mimi niweze kutoa mchango wangu katika sekta hii ya madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote niungane na Wabunge wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Madini pamoja na Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na watendaji wote ambao kwa kweli tumeona kazi kubwa wanayoifanya na kimsingi hakika wanaitendea haki hii Wizara ya Madini. Niseme tu wazi wazi kabisa kwamba Watanzania wanaona kazi wanayoifanya na macho ya Watanzania ndiyo macho ya Mungu. Kwa hiyo, Mungu anawaona jinsi wanavyofanya, waendelee kufanya kazi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba Mheshimiwa Waziri, kwa kweli hotuba yak ni nzuri, ameeleza mambo mengi sana. Niombe tu Serikali iendelee kuwaunga mkono ili kusudi haya mambo mazuri tuliyoyaona, basi tuweze kuyaona kwa vitendo na hawa wachimbaji wetu wadogo basi wanaendelea kufaidika.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan alisema kwamba ametoa maelekezo kwamba, ifikapo mwaka 2034 angalau 80% ya Watanzania basi wawe wanatumia nishati safi ya kupikia. Kweli Wizara ya Madini hawajabaki nyuma, Wizara ya Madini wamelichukua hilo na leo hii tunaona kuna viwanda vinne vimejengwa vya kutengeneza mkaa unaotokana na makaa ya mawe. Viwanda hivi wamejenga Mbeya, Kisarawe, hapa Dodoma na vilevile kule Tabora. Sisi Wanatabora tumefarijika sana na ujenzi wa kiwanda hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Wanatabora ni wakulima wa zao la tumbaku, tunakausha tumbaku yetu kwa moto. Tulikuwa na mashaka, Wanatabora walianza kuwa na mashaka kwamba je, miaka 10, 15 inayokuja itakuwaje? Tukizingatia kwamba miti iliyopo kule Tabora na hususan Sikonge, basi wana Sikonge ni kama supplier wa mkaa katika nchi hii, miti ilikuwa inakwisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunamshukuru Mheshimiwa Rais kumbe yeye alishaliona tayari na akatoa maelekezo kwa Wizara ya Madini kwamba waende wakajenge kiwanda pale Tabora. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa juhudi hizi ambazo wamezifanya. Hata hivyo, kiwanda kimekamilika na tayari kimeshazinduliwa, lakini mpaka hivi sasa bado hakijaanza kufanya kazi. Tunamwomba sana Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake, hebu kiwanda hiki kianze kufanya kazi basi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika msimu unaokuja tungependa kuona kwamba wakulima wa tumbaku katika Mkoa wa Tabora basi wanaanza kukausha tumbaku yao kwa kutumia haya makaa ya mawe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, ninaona elimu bado haijafika. Hebu wafike kule waende wakatoe elimu. Bado kuna wakulima wana mashaka mashaka kwamba yawezekana makaa ya mawe labda yanaenda kuwaongezea gharama ya uzalishaji. Wafike kule watoe elimu, wawaelimishe wananchi waweze kufahamu, ili kusudi huo mkaa uweze kupokelewa na wakulima wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe tu, ninaamini kwamba wameshafanya research ya kutosha, wameshafanya utafiti wa kutosha na wameshajua gharama za wakulima wa tumbaku wanatumia kiasi gani katika kuni na je, sasa gharama zenu wanazokuja nazo zinakuwaje? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe, suala la kutumia mkaa wa makaa ya mawe, ni suala la kimazingira. Niwaombe sana Wizara watumie lugha yoyote wanayoweza, ili kusudi wadau wa mazingira, wadau wa mazingira waweze kuingia pale na ikiwezekana basi kuwe na ruzuku ili kusudi gharama ya kutumia makaa ya mawe iwe ni chini zaidi ukilinganisha na gharama ya kuni wanazotumia. Hakika si kwamba tutasaidia mazingira, lakini vilevile kwa hawa wakulima wa tumbaku watakuwa wameongeza kipato. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwaombe sana ndugu zangu, hebu watufanyie hayo Wanatabora ili kusudi tuweze kuona kwamba kwa kweli Serikali ya Mama Samia imefanya kazi kubwa na imetusaidia sisi Wanatabora kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwenye upande wa madini, sisi watu wa Sikonge kweli hatuna madini mengi, lakini madini tunayo. Ukienda katika Kata ya Kitunda, tunayo dhahabu, lakini ukija jirani yake hapa panaitwa Kururu, madini ya dhahabu yamegundulika mahali hapo, lakini changamoto aliyoipata msemaji aliyetangulia pale mbele kwamba bado kuna changamoto kati ya TFS…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana. Mheshimiwa Maganga muda wako umekwisha.
MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sana TFS na TAWA wamalize changamoto zao ili kusudi tuweze kufaidika na hayo madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaunga mkono hoja. (Makofi)