Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Eng. Ramadhani Hamza Singano

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bumbuli

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. RAMADHANI H. SINGANO: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa kuniona wakati huu ili niweze kuchangia katika sekta hii iliyopo mbele yetu. Kwa dhati ya moyo wangu nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa wasaa wa wakati huu, lakini pia nimshukuru Mama yetu kipenzi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwashukuru Wizara ya Madini kwa hotuba nzuri ya kisomi ya kisayansi, yenye kutupa matumaini kwa Tanzania ijayo. Nimshukuru ndugu yangu Waziri wa Madini Mheshimiwa Anthony Peter Mavunde na Naibu wake, lakini na watendaji wote wa Wizara ya Madini, nimemsikia ndugu yangu Mhandisi Yahya Samamba, Katibu Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda niende moja kwa moja kwenye yale maeneo nyeti ambayo ninataka nishauri. Eneo la kwanza ni eneo la vibali kwenye maeneo ya migodi. Eneo hili lina changamoto kidogo, lakini kwa sababu ni Wizara yenye weledi, ninaamini inaenda kukaa na kuweka vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika maeneo ya mgodi kuna kitu kinaitwa bwawa la tope sumu. Kwa lugha nyepesi hiki ndiyo choo cha mgodi, kwa sababu uchafu wote huhifadhiwa hapa. Sasa Wizara ya Maji inatoa vibali vya ujenzi lakini na Wizara ya Madini inatoa vibali vya ujenzi. Kufika mahali tukawachanganya wale wawekezaji; nani atoe kibali?

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Maji yeye ndiye anapitisha michoro na kuona usahihi wa michoro hiyo na kutoa kibali cha ujenzi. Wizara ya Madini naye anatoa kibali cha ujenzi. Kwa hiyo, hili likaliwe sawa ili kutowachanganya wawekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Madini wanayo Sheria ya 2010 ambayo ni utekelezaji wa Sera ya Madini ya 2009 lakini imekuwa ikipitiwa 2017 na 2024. Wizara ya Maji wanayo Sheria namba 11 ya 2009 ambayo imepata marekebisho pia 2022. Sasa hizi zote ni sheria zinahitaji kukaa ili kuona jibu la pamoja, kusiwe na vibali zaidi ya kimoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ni eneo la bond. Sheria ya Madini ya 2010 ilikuja na kitu kinaitwa kanuni ya rehabilitation bond (Bond ya ukarabati) kwa maana kila kampuni yenye mradi mkubwa inapaswa isukume, ipeleke dhamana yake ya kulinda mazingira ambayo ndiyo hiyo bond, lakini leo NEMC nao wamekuja na kanuni inayoitwa environmental performance bond. Sasa hapa pia tunawachanganya wawekezaji. Ipelekwe wapi; NEMC au Madini? Au NEMC kwa sababu ndiye mwenye mazingira yake? Hapa pia panahitaji kuwekwa sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni wakati wa kufunga mgodi, mabwawa ya tope sumu haya ni hatari sana. Sasa ile layer ya juu inayowekwa kwa kufunika maana yake lazima iangaliwe kwa jicho la kihandisi. Nishauri taasisi zote za maji, mazingira na madini zikae pamoja kuona kuhitimisha hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la mwisho ni kufunga mashimo ya mgodi, inaitwa (pit) namna ya kuzifunga.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa mwongozo sahihi unaojitosheleza haujapatikana. Watu watajiuliza je, tufukie kwa vifusi, je, tuache maji yajae iwe ni maziwa, ni pit lake. Lakini kabla hilo halijafikiriwa kuna mambo ya kitaalam ya kuweza kufanya. Je, kemia ya huo mwamba inafahamika? Kama kuna element za Sulphur huoni kwamba tunaenda kwenye mambo ya acid mines drainage.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kuna mambo mengine ya ki-geology, mwamba unatiririsha maji, yana mwelekeo kuelekea wapi. Kuna wakati pit lake iko juu, level ya maji ya chini ya ardhi iko juu kwa hiyo inalisha, lakini kuna wakati ni kinyume chake, haya yasiposimamiwa vizuri yataleta hatari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni usimamizi wa mazingira katika eneo zima la mgodi. Haya ni maeneo muhimu ambayo nayo yanahitaji wataalam wakae chini watoe miongozo ili tusije tukatengeneza bomu la miaka ya baadaye. Pia ni lazima watu waangalie zile kuta za lile shimo kabla hatujaamua liwe pit lake. Je, ni stable? Na kama siyo stable ikitokea mmomonyoko au landslide tutakuwa wageni wa nani?

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa ahsante sana.

MHE. RAMADHANI H. SINGANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda, ninaunga mkono hoja na ninakushukuru sana kwa nafasi hii. (Makofi)