Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kupata nafasi ya kuchangia katika hii Wizara muhimu kwa sababu watu wangu wa Jimbo la Tarime Vijijini wanahusika sana katika madini. Ninampongeza Mheshimiwa Waziri amefika Nyamongo yeye na Naibu Waziri wake, lakini ametusaidia sana kutoa leseni kwa wachimbaji wadogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri ile kasi ambayo alianza nayo iendelee vijana, wapate matokeo ili waweze ku-encourage wengine. Inasaidia kupunguza ugomvi kati ya vijana wa Tarime na mwekezaji wa Barrick Plus Mara. Kwa sababu hawawezi kushuhudia dhahabu inatoka tu halafu wao hawapati chochote.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, Mheshimiwa Waziri anafahamu kwamba tuna mgogoro wa CRS. Ninaumia sana mpaka hapo kwamba mvua imenyesha kule Tarime Vijijini tulikuwa na miradi kwenye kata zote 26, sasa maeneo hayapitiki ukienda Bumera hakuna mawasiliano, Susuni hakuna mawasiliano, Itiryo hakuna mawasiliano, Nyarokuba hakuna mawasiliano barabara zimekatika. Hata hivyo, fedha iko pale mgodini tangu Januari zaidi ya shilingi bilioni nne, mgogoro ule ukiisha watu wafanye kazi za maendeleo wapate huduma kama ambavyo Mheshimiwa Rais anatamani tupate huduma wote, watusaidie sana kumaliza mgogoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kwenye CSR. Ukienda kuangalia namna ambavyo CSR inavyofanyika kule Geita na inavyofanyika Kahama na Tarime ni tofauti. Kwa mfano pale Kahama, Barrick wenyewe wamekubali kujenga Barabara ya lami kilomita 96, ninadhani kutoka Kahama mpaka pale Msalala. Vile vile kuna Barabara kutoka Komaswa kwenda mpaka Nyamungo wanatumia mitambo yao, wanapita vumbi, wanaogopa mifugo ya watu hawajengi lami katika lile eneo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda katika hizi kanuni zilizopo ambazo zina mgogoro sasa, miradi ile inatekelezwa na halmashauri, wanatangaza tenda wanalipa wenyewe. Darasa la shilingi milioni 20 mpaka 25, leo mkandarasi wa mgodini analipwa shilingi milioni 37, zahanati ya kujenga kwa shilingi milioni 50 mpaka milioni 100, sasa hivi wanaenda mpaka milioni 160. Fedha nyingi imeenda kwenye miradi ambayo wanatoa utaratibu kwa local fund kupitia TAMISEMI, gharama inakuwa ni ndogo sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sisi tungeomba kanuni hii ibadilike. Mgodi core function yao ni uchimbaji na kutafuta dhahabu, siyo kazi ya kujenga madarasa, kazi ya kuchimba vyoo, kazi ya kutengeneza makalavati, unaongeza kazi ambayo ni ya ziada kwao. Wao wabaki na fedha ile ya mgodini, utaratibu wa manunuzi ufanyike na halmashauri, wakishakamilisha mgodi ulipe kwa viwango vya kawaida. Ule Mgodi wa Barrick ukisimama leo hakuna mtu wa kawaida atafanya tenda pale Tarime, kwa sababu kama analipwa milioni 37, kwa nini afanye mradi wa milioni 20 au 25, hiyo kazi ni ngumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja ambayo wenzangu wamezungumza sana hapa ya technical support. Hili jambo ni very serious tuna shida ya ajira katika hii nchi, vijana wetu wanahangaika mtaani wamesoma hawana kazi, hii sekta ya madini ni sekta ya kuwatoa vijana wengi mtaani wakopeshwe wakachimbe.

Mheshimiwa Naibu Spika, hawa watu wageni ambao wanakuja hapa kwamba wanatoa support, wanatudanganya kama danganyatoto halafu kule wanafanya shughuli nyingine. Mheshimiwa Waziri alete sheria hapa tubadilishe, yeye ametembea, ukienda China, India zipo kazi ambazo mgeni hawezi kupewa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tena mikataba inasema kama una utaalamu ambao hatuna, tunakupatia leseni miaka miwili, mitatu ni lazima uwa-company Watanzania, ukikaa miaka miwili utaalam wako utuachie, rudi kwenu ili vijana wapate ajira hapa. Kwa namna ilivyo... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waitara, ahsante sana, malizia.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ilivyo, mwisho wa siku tutaanza kama mambo ya Afrika Kusini, watu kuanza kupigana. Utaratibu huo uwekwe wazi. Mkataba uoneshe anaomba kufanya kazi gani, ni utaalam gani haupo, simamia leseni watu wafanye kazi. Wabunge wamesema tumezungumza, tumemshauri Waziri, asije kulalamika.

NAIBU SPIKA: Ahsante sana.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na ninaunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Madini. (Makofi)