Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kuchukua fursa hii kukushukuru sana kwa nafasi uliyonipatia ya kujibu hoja za Waheshimiwa Wabunge. Ninaomba uniruhusu kwanza nimshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kwa miongozo na maelekezo yao ambayo yameendelea kuimarisha sekta ya madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa ninaomba nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Steven Lemomo Kiruswa, Naibu Waziri wa Madini kwa ushirikiano mkubwa anaonipa na msaada mkubwa ambao ananipatia kuendesha sekta hii. Pia, nimshukuru Katibu Mkuu na timu nzima ya wataalam wa Wizara ya Madini ambao wote kwa pamoja wamekuwa msaada mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda ninaomba uniruhusu niende kujibu hoja za Wabunge 20. Hoja moja baada ya nyingine, lakini pia kwa sababu kuna hoja zimesemwa sana nitazipa muda kidogo niweze kueleweka vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaanza kujibu hoja za Waheshimiwa Wabunge, ninaomba nianze na jambo hili, ni bahati mbaya sana watu wengi huwa wanachukulia vitu kwa kawaida na nabii huwa hakubaliki kwao. Leo ninataka niliambie Bunge lako Tukufu, kazi kubwa aliyoifanya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye sekta hii ya madini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ya kwanza, Sera ya Madini ya Mwaka 2009, Ilani ya Uchaguzi ya CCM na Mpango wa Maendeleo uliiwekea sekta ya madini target ya kufikia 10% ya uchangiaji wake kwenye pato la Taifa. Mwaka wa fedha 2023/2024, sekta ya madini ilikuwa inachangia kwenye pato la Taifa kwa asilimia 9.1 na malengo yalikuwa ifikapo mwaka 2025 tuwe tumefikisha 10%. Kwa mujibu wa taarifa za takwimu, Shirika la Takwimu la Taifa (NBS) mwaka 2024, mwaka mmoja kabla ya mwaka wa kimalengo, sekta ya madini hivi sasa inachangia kwenye pato la Taifa kwa 10.1% kwa maana ya double digits. Hii ni kazi nzuri ya maelekezo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa taarifa, Pato letu la Taifa ni dola bilioni 91 sawa na shilingi trilioni 220. Ndugu zangu Wabunge, waende katika nchi zote za Bara la Afrika wanitafutie nchi 10 ambazo zinachangia 10% kwenye pato la Taifa kupitia sekta ya madini. Haitokei popote, siyo jambo la kawaida, ni kazi nzuri ambayo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, Tanzania ni moja kati ya nchi kubwa na wazalishaji wakubwa wa madini ya dhahabu, lakini kwa muda wote nchi yetu haikuwemo kwenye orodha ya nchi zenye akiba ya dhahabu kupitia Benki Kuu. Kwa mujibu wa takwimu, nchi inayoongoza katika Bara la Afrika kwa kuwa na akiba kubwa ya dhahabu kupitia Benki Kuu ni Algeria, ina tani 174 na kwenye 10 bora ya mwisho ni Msumbiji ina tani 3.682 ya akiba ya dhahabu kupitia Benki Kuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo kwa sekta ya madini, tufanye mabadiliko ya sheria, Kifungu cha 59(1) na (2) cha Sheria ya Madini, Sura ya 123 tumekifanyia marekebisho na hivi sasa kinasomeka ifuatavyo; “Mtu yeyote ambaye ana leseni ya uchimbaji na ambaye anasafirisha madini nje ya nchi, lazima atenge asilimia isiyopungua 20 ya madini yote kwa ajili ya kuongezwa thamani, kusafishwa, kuchenjuliwa na biashara ya ndani.”

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kutunga Sheria hiyo Benki Kuu ya Tanzania imeanza kununua dhahabu tarehe Mosi Oktoba, 2024. Leo miezi 18 Benki Kuu ya Tanzania imeweka historia ina tani 23.8 ya dhahabu na hivi sasa Tanzania ndani ya miezi 18 ipo kwenye 10 bora ya nchi zenye akiba ya dhahabu, hii ni kazi kubwa sana imefanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu ambalo lazima tumshukuru sana Mheshimiwa Rais, Mwaka wa Fedha 2015/2016 sekta hii ya madini iliingiza kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali shilingi bilioni 161 kwa mwaka mzima. Baada ya kufanya marekebisho ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2017, tukaanzisha vituo vya ununuzi na masoko ya madini na kudhibiti biashara haramu na utoroshaji. Leo sekta ya madini inachangia kuingiza fedha nyingi zaidi kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha uliopita tuliwekewa malengo ya kuingiza kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali shilingi trilioni moja, mpaka tarehe 30 Juni, 2025, mwaka wa fedha ulipokuwa unaishia tuliingiza kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali shilingi 1,071,000,000,000, sawa na 113%. Mwaka huu tumewekewa lengo la kuingiza shilingi trilioni 1.2 kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Ninavyosimama hapa leo mbele yako mpaka siku hii ya leo, sekta ya madini imeingiza kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali shilingi 1,156,000,000,000, tumebakiza bilioni 44 kuvunja rekodi yetu ya mwaka jana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni kazi nzuri ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Waheshimiwa Wabunge makofi kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hayatoshi, tuongeze makofi kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haya yalikuwa ni maneno ya utangulizi ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, sasa ninaanza kujibu hoja za Wabunge. Ninaanza na hoja ya kwanza, hoja ya kwanza ni ya kuhusu utafiti. Waheshimiwa Wabunge, ninakubaliana nanyi, hatuwezi kuendeleza sekta ya madini pasipo utafiti. Utafiti ni jambo muhimu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu ya Tanzania tumefanya kitu kinaitwa Low Resolution Airborne Geophysical Survey kwa 100% ambayo ilifanyika miaka kati ya 1978 mpaka 1979. Maana yake ni kwamba, tunairusha ndege ambayo inakuwa katika uso wa dunia kwa meta 120 na katika upana wa kilometa moja, lakini tumefanya utafiti wa jiokemia kwa 24% katika Nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa dunia inafanya kitu kinaitwa High Resolution Airborne Geophysical Survey. Huu ndiyo utafiti wa kina ambao una uwezo wa kupiga picha chini ya ardhi mpaka kilometa moja ikakuonesha anomalies za magnetic point kwa maana ya viashiria vya mipasuko ya madini ili tuwaongoze vizuri wachimbaji wetu wadogo wasichimbe kwa kubahatisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili tumelifanya kwa 16% tu kwa nchi yetu ya Tanzania. Nchi yetu ya Tanzania ina ukubwa wa eneo la kilometa za mraba 945,000 ambayo ni sawasawa na ekari 233. Tumeigawa Nchi yetu ya Tanzania katika vitu vinaitwa QDS (Quarter Degree Sheets) zipo 322. Kila QDS moja ina urefu wa kilometa 54 na upana wa kilometa 54 na hivyo inatengeneza eneo la kilometa za mraba 2,916 sawasawa na ekari 726,696, maeneo haya tunayo 322 tunayofanyia utafiti wa kina ni 16% tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka niliambie leo Bunge lako, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anakwenda kuweka record katika Nchi yetu ya Tanzania katika eneo hili la utafiti. Tunao mradi ambao tuko hatua za mwisho kuukamilisha na wenzetu wa Hispania, tukiusaini mradi huu tutarusha ndege katika blocks mbili. Blocks hizi mbili zina eneo la ukubwa kilometa za mraba 176,676 sawasawa na 18% ya Nchi yetu ya Tanzania. Ndugu zangu hivi sasa tuna 16% ukiongeza hizi 18 ambazo tutazianza muda siyo mrefu tutafika 34%, ninataka niwaondoe hofu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge wa Geita Mjini ndugu yangu Chacha alikuwa anapata wasiwasi, tutafika 2030 kwa 50%? Kama leo 2026 tunakaribia 34%, tunao mdau mwingine kaonesha interest mkataba uko Wizara ya Fedha atapima block ya kuanzia Dodoma, Singida, Tabora, mpaka Shinyanga, ambayo itakuwa ni 18% na yenyewe pia. Kwa hiyo, tutafika zaidi ya 50% ndani ya muda mfupi huu katika kipindi cha uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge tumpe imani Mheshimiwa Rais, dhamira ni njema tutaifikia kuipima nchi yetu katika kiwango hicho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili, local content, ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, migodi yote nchi nzima inatumia shilingi trilioni 5.1 kwa ajili ya manunuzi ya bidhaa na huduma. Tumetunga sheria hivi sasa, Kanuni ya 13A ya Local Content Regulation, inasema: bidhaa ambazo tutaziainisha ziko 20, hazipaswi kufanywa na mgeni isipokuwa Mtanzania, ili hela hii trilioni tano ibaki Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nichukue fursa hii, kurudia tena ni marufuku kwa mgeni yeyote ambaye ana kampuni hapa Tanzania kufanya kazi zile 20 ambazo zimeainisha kwa mujibu wa regulation yetu hizi ni kwa ajili ya Watanzania, tuujenge uchumi wetu na hii ni kazi kubwa ambayo imefanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la tatu, Waheshimiwa Wabunge wamezungumzia kuhusu leseni. Nitaendelea kufuta leseni, ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais, nitaendelea kufuta leseni. Leseni siyo za upangishaji, leseni ni za kuchimba au kufanya utafiti. Hivi sasa wapo Watanzania na wapo wageni wanamiliki maeneo makubwa ya leseni na hawayafanyi kazi, wachimbaji wetu wadogo wanakosa maeneo ya kufanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimefuta leseni 40 wiki iliyopita, lakini bado nina mtiririko wa leseni nyingi sana na nitaendelea kuzifuta. Wapo wenzetu 38, wanamiliki eneo lenye ukubwa sawasawa na halmashauri za manispaa za Moshi uziunganishe 10. Watu 38 ndiyo wanazimiliki, watu hao hatuwezi kuwaacha na hawafanyi chochote katika leseni hizo, nitafuta leo, kesho na kesho kutwa hatutaacha wachimbaji wetu wanakosa maeneo ya kuchimba kwa sababu ya watu wachache kuzuia leseni hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo ambalo limegusa hisia ya Wabunge wengi sana ni eneo la technical support agreement na hapa nitapunguza sauti yangu. Sheria ya Madini, Sura 123, Kifungu cha 9 kimetamka hivi: “Ni marufuku kwa mgeni yeyote kuingia kwenye leseni ndogo ya uchimbaji, ni marufuku.” Leseni hizi ni maalum kwa ajili ya Watanzania, lakini tukaenda mbali zaidi, sheria ikatambua kwamba kuna wakati Watanzania wanaweza wakachimba, lakini wakafikia sehemu wakakosa baadhi ya vitu vichache na usaidizi wa kuweza kumfikia ili aweze kuchimba kwa tija zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kifungu cha 9 cha Sheria ya Madini kimeweka ruhusa ya kuwepo kwa mikataba ya msaada wa kiufundi. Ninataka nikiri, Waheshimiwa Wabunge mmezungumza kwa hisia na ninakubaliana nao, katika kipindi fulani kifungu hiki kilikuwa abused na kiasi kwamba kikapelekea wageni wengi sana wakaingia kwenye leseni ndogo za uchimbaji pasipo kufuata utaratibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilichukua maamuzi gani? Hapa ninaomba niliseme na nieleweke vizuri. Hatua ya kwanza ambayo tuliichukua katika kuhakikisha kwamba tunaweka masharti magumu ya mgeni kuingia kwenye leseni ndogo ya uchimbaji, cha kwanza tulitunga kanuni. Tulitunga kanuni ya msaada wa kiufundi ambapo hapo awali haikuwepo, lakini pamoja na hiyo tukasema mambo yafuatayo. Nitaomba hapa, wachimbaji wadogo ninajua wapo hapo juu wanielewe vizuri kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nirudie tena leo, ni marufuku mtu yoyote mwenye leseni ya uchimbaji kuingiza wachimbaji wadogo katika leseni yake, ni marufuku. Leseni ni ya uchimbaji siyo ya kuwapangisha watu kuweka maduara. Ukikubali watu waingie kwenye leseni yako mambo yafuatayo lazima yafanyike:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ilikuwa haiwatambui watu wenye maduara na Wizara ya Madini hatujatengeneza haki madini mpya ya watu wenye maduara isipokuwa tumeweka utaratibu. Hivi sasa kwenye leseni yoyote ambapo kuna maduara yamechimbwa, sharti la kwanza ukikubali kuingiza wachimbaji wadogo hakikisha mmesaini mkataba na mkataba umesajiliwa Tume ya Madini, kati ya kwako wewe na mchimbaji mdogo aliyeweka duara lake, ili siku ukipata mwekezaji, kwanza right of first refusal apewe aliyeweka nguvu yake maduara, kwa sababu wewe ndiye umemkaribisha mwenye leseni. Akishindwa yeye ndiyo uende kwa mtu wa pili, hivyo ndivyo Kanuni yetu inavyosema.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kanuni ya 18A ya Mineral Rights inazungumza hivyo, kwamba hilo ni sharti. Ikitokea hivi sasa ni kwamba wamekwenda wageni wengi sana katika maeneo yetu, na kwa kusaini mikataba ambayo muda mwingine imekuwa na mapungufu makubwa sana, nimeelewa kilio cha Wabunge. Waheshimiwa Wabunge, ninaomba waniamini kijana wao, nimesimama hapa mbele ya Bunge hili, nina hofu ya Mungu, siko hapa kuzungumza jambo la uongo, ninataka niwaambie ukweli kabisa. Kanuni yetu tumeitunga ikiwa ina mwaka mmoja, ninaomba waniruhusu nifanye yafuatayo:- (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninayasema hapa Bungeni kuanzia sasa ni marufuku kwa Afisa Madini yeyote kusaini mkataba wa kiufundi (Technical Support Agreement) mpaka mambo yafuatayo awe amejiridhisha nayo: (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, cha kwanza, eneo ambalo mkataba wa kiufundi unaingiwa kama kuna wachimbaji wadogo, hakikisha wale wachimbaji wadogo wamepewa haki ya msingi ya kwanza ya kuwekeza, kama hilo halijatokea, basi na kama hawana nguvu ya kuwekeza hapo lazima wafidiwe gharama ya kile ambacho wamekiweka pale katika yale maduara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, ndiyo kuanzia hapo sasa unaweza kwenda katika hatua ya kumtafuta mwekezaji mwingine ambaye anaweza akaweka nguvu, lakini hatuwezi kuweka nguvu katika maduara ambayo Watanzania wameweka nguvu zao na utaratibu haukufuatwa, hicho ndicho ambacho kanuni inasema. Sasa Waheshimiwa Wabunge ninaomba nitoe maelekezo kwa Maafisa Madini wote wakazi hapa, kuanzia leo ninatoa wiki mbili Maafisa Madini wakazi wote wapitie upya Mikataba yote ya Technical Support Agreement na kuifanyia audit.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninajua wako Watanzania wenzetu ambao wametoa taarifa za uongo, mikataba iliyoletwa tume ni tofauti na ile ambayo wanaitekeleza kule. Kama Mheshimiwa Chacha alivyosema, akibainika mtu wa namna hiyo amevunja sheria kwa mujibu wa Sheria ya Madini na hatua ambayo itafuata ni nitafuta leseni yake. Waheshimiwa Wabunge, katika span hii ninawapa kazi timu yangu kupitia na kufanya audit ya kutosha katika eneo hili, then baada ya hapo, Waheshimiwa Wabunge kwa mapendekezo ambayo wameyaleta, katika haki ya siri kuna nafasi pia, ya kuweza kusikiliza upande mwingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, waniruhusu kwa leo badala ya kutamka hapa kwamba, ninaiondoa moja kwa moja, kwanza nikafanye ukaguzi kupitia timu yangu then tutakuwa tunaendelea ku-monitor situation, ikiendelea kuwa worse tutaifuta hii technical support. Ninaomba kwa leo wanikubalie hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mwanahamisi ameniambia kwamba, leo haungi hoja hii mkono mpaka nifafanue technical support maana yake ni nini. Kwa mujibu wa Kanuni ya 3 ya Kanuni ya Utoaji Msaada wa Kiufundi, inafafanua kwamba, msaada wa kiufundi ni ule msaada ambao una utaalam wa uchimbaji na uongezaji thamani madini, pamoja na uendeshaji wa mitambo ambao haupatikani kirahisi ndani ya nchi; kwa hiyo, tuna underline hapa haupatikani kirahisi ndani ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, timu yangu ikienda kwenye audit ikayabaini haya, kilichosemwa kwenye mkataba na hali halisi ni tofauti, Mheshimiwa Mwanahamisi, ndiyo hapo anakwenda kufuta hizo leseni na hicho kitu kinakuwa kimeishia hapo. Sasa arudishe shilingi yangu Mheshimiwa Mwanahamisi, katika hoja hiyo ninafikiri tumeelewana vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine Waheshimiwa Wabunge wameisema kwa sauti kubwa sana ni ya CSR. Ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, miaka 10 iliyopita uwajibikaji kwa jamii ilikuwa ni hisani, haikuwa kwa jamii, haikuwa kwa mujibu wa sheria. Mwekezaji alikuwa anaamua awajengee choo au darasa ile host community. Waheshimiwa Wabunge tufanye marekebisho ya kanuni, hivisasa kwa mujibu wa Kifungu cha Sheria cha 133, kimeweka sharti la lazima kwa kila license holder ahakikishe anatimiza wajibu wake kwa jamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa Waheshimiwa Wabunge utaratibu ni kwamba, kijiji au eneo husika ndiyo wao wanabuni mradi, wakibuni mradi unapita kwenye Kamati ya Kata, baadaye unaletwa kwenye Kamati ya Fedha, Kamati ya Fedha inapeleka kwenye Baraza la Madiwani. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge hii mipango wanaipitisha wenyewe. Ninawaomba hivi sasa waanze kushiriki, wale ambao katika maeneo yao kuna migodi inapitia huku kwenu katika utaratibu huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikitoka hapo ninakwenda kwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Waziri wa TAMISEMI, kwa ajili ya kupitishwa. Sasa hoja ambayo Waheshimiwa Wabunge hapa wamesema ni kwamba, kuna wasiwasi wa kwamba, gharama inayotumika ya ujenzi wa kupitia CSR ni kubwa kuliko ile ya Serikali. Kabla haijafika mbali kamati ile ipo katika Kamati ya Fedha na Baraza la Madiwani, ni njia ya kwanza ya kumwambia mwekezaji na Kamati ile ya Wataalam kwamba, gharama hii siyo gharama ambayo inakubalika na waipitie upya.
Mheshimiwa Naibu Spika, huu ni wajibu wetu kuanzia ngazi ya chini kabisa. Nawaomba sana Waheshimiwa katika eneo hili tuhakikishe tunasimamia ipasavyo, lakini wameenda mbali zaidi, wamesema kwa nini fedha hizi zisiende halmashauri, wao ndiyo wasimamie suala la utoaji wa hizi fedha. Waheshimiwa Wabunge, ninaomba niwapitishe Kifungu cha 3 cha Sheria ya Manunuzi ya Umma. Kinasema fedha gani ni fedha ya umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, CSR, siyo fedha ya umma. Haiwezi kuingizwa kwenye mchakato wa procurement process ya kikawaida kwa sababu, haiingilii huko. Hata ukisoma Kifungu cha 2 cha Public Finance Act kimeiweka pale bayana, zipi ni fedha za umma; Waheshimiwa, CSR haimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni ngumu sana kui-subject katika utaratibu wa kuipitisha katika halmashauri; hili nimelisema na nimetoa ufafanuzi sana. Ninawaomba Waheshimiwa Wabunge, zipo hoja ambazo Mheshimiwa Chacha amezisema, ninaomba nizipokee kama ushauri. Pia, ninafahamu changamoto ambazo zimetokea kwa Mheshimiwa Mwita Getere, wanipe muda mchache. Baada ya wasilisho hili, nilisema nitawaita, tutakaa kwa pamoja tuweke mkakati, ili CSR hizi ziweze kuwanufaisha wananchi wao kwa kiwango kikubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, imezungumzwa hoja ya double taxation. Hili ninaomba wanikubalie kwamba, ziko changamoto zinazojitekeza ambazo zinasababisha baadhi ya maeneo kutozwa mgawanyo wa mawe zaidi ya mara moja au mara mbili. Tumeongea ndani ya Wizara, nitaitisha wadau, wakiwemo wachimbaji wadogo na wadau wengine wote, pamoja na Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI nitamwomba tushiriki naye kwa pamoja kwa sababu, pia, halmashauri huwa zinaingia katika eneo hili, tujadili kwa pamoja namna bora ya kulifanya jambo hili, liwe suluhisho la kwanza, ili mchimbaji mdogo asichajiwe mawe mara mbili, kwa maana ya tozo.

Mheshimiwa Naibu Spika, suluhisho la kwanza, wachimbaji wadogo wapo pale juu jukwaani, niliwaambia hivi; sheria inataka mtu yoyote aliyepewa leseni ya uchimbaji ukitaka kuchakata, ukichimba, lazima uchakate ndani ya leseni yako. Ukiyatoa monitoring yake ndiyo inaleta changamoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa tukikubaliana kwamba, leo wananiruhusu niweke katazo, hakuna mchimbaji yoyote mdogo Tanzania kutoa mawe nje ya leseni yake hakutakuwepo na tozo ya mara mbili, haitakuwepo. Ninaomba Waheshimiwa Wabunge waniruhusu, tutakaa kwa pamoja kulijadili hili jambo tutengeneze njia nzuri zaidi, ambayo Serikali haitaumia, lakini vilevile tutamsaidia mchimbaji mdogo aweze kukua.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo limesemwa hapa ni la uongezaji thamani katika madini ya dhahabu. Tumepiga hatua, tuna viwanda sita hivi sasa vya kusafisha dhahabu mpaka kufikia 99.99%. Sasa tunawasaidia waweze kufikia ithibati ya LBMA, ambayo inataka uwe na uwezo wa kuchakata tani 10 ya dhahabu kwa mwaka na uwe na fedha kiasi cha euro milioni 15, kwa maana ya kuweza kufanya biashara hiyo. Ndiyo sehemu ambayo tunawasaidia hivi sasa hawa wenzetu kuongeza thamani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama kuna wakati tumeongeza viwanda vingi vya kuongeza thamani ni wakati huu wa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Dodoma peke yake ina viwanda tisa vya kuongeza thamani ya madini, kikiwemo kiwanda kikubwa cha Zingzong kilichoko Zamahelo, ambacho hivi sasa kimeanza kuyeyusha madini ya nickel, lakini ukienda Nala kuna kiwanda cha kubadilisha jiwe lile la shaba, kutoka kwenye kuwa jiwe kwenda kuwa copper cathode.

Mheshimiwa Naibu Spika, haya ni mabadiliko makubwa sana ambayo yamefanyika hapa, lakini tunategemea kuwa na kiwanda kikubwa cha kuyeyusha ferro niobium pale Panda Hill, Mbeya, ambayo itakuwa ni smelter ya nne kwa ukubwa duniani, ukiacha mbili ambazo, moja iko Canada na moja Brazil. Kwenye eneo hili pia, tumefanya kazi ipasavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Madini ya Tanzanite, ni kweli imekuwepo changamoto ya kuporomoka kwa bei, lakini tumekuja na mkakati hivi sasa. Mkakati wa kwanza ni kuhakikisha kwamba, tunarejesha minada ya madini haya ya vito ya Tanzanite, lakini la pili ni kuendelea kufanya maonesho makubwa ya Kimataifa kuitangaza Tanzanite yetu Kimataifa, ili kuweza kuiletea soko.

Mheshimiwa Naibu Spika, madini ya vito ni madini ya luxury, tunashindana na sehemu nyingine zote duniani. Sisi pia, tumeandaa mkakati wa kuhakikisha tunaiweka mbele Tanzanite yetu, inarudisha heshima yake na kuchangia kwenye pato la Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, uwezeshaji wa wananchi kiuchumi na hasa wachimbaji wadogo. Tumeweka utaratibu...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri, hitimisha.

WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, tumeweka utaratibu hivi sasa, kupitia Benki Kuu ya Tanzania ambako imekwenda kutengenezwa taasisi ya kuwapa dhamana wachimbaji wadogo, inaitwa Credit Guarantee Corporation, ambayo itaanza na mtaji wa shilingi bilioni 300 mpaka trilioni sita, kwa ajili ya kuwasaidia wachimbaji wazawa wa Nchi yetu ya Tanzania. Haya yote ninaamini yakifanyika tutakuza sana uchimbaji mdogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ni la ndugu yangu Mheshimiwa Doto Bahemu, ananiangalia sana pale, anataka kusikia kuhusu nickel Kabanga. Mheshimiwa ninataka nimhakikishie kwamba, sisi, kama Wizara ya Madini, mwekezaji siwezi kusema hapa leo anatakiwa lini aanze. Alipaswa kuanza muda mrefu kwa mujibu wa Mkataba wa Msingi wa Mwaka 2021; tumempelekea barua na ameleta commitment, ambayo sasa timu yangu inaifuatilia kuona kile ambacho kimetimizwa, ili kazi hii ianze mara moja kwa mujibu wa mkataba aliousaini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninafahamu mradi huu ni mkubwa. Mimi nitafika, kwa ajili ya kutoa ufafanuzi mzuri kwa wananchi wake, ili niweze kueleweka.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kutoa hoja. (Makofi)