Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ambayo anaifanya, hasa kwenye eneo la sekta ya kilimo. Tendo tu la kupeleka pembejeo zenye ruzuku, zimewasaidia sana wakulima waweze kuzalisha kwa kiwango kikubwa sana, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kumshukuru sana Mheshimiwa Chongolo, Waziri wa Kilimo kwa kazi nzuri ya kuisimamia Wizara ambayo anaifanya akishirikiana na msaidizi wake Mheshimiwa Naibu Waziri, wamefanya kazi nzuri. Wameendelea kuisimamia Wizara na ni wasikivu, wanasikiliza watu hasa tendo la kuwashirikisha wadau wote wa sekta ya kilimo, imefanya kila mtu ajenge imani kwenu ninyi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nianze mchango wangu kwenye zao la tumbaku. Zao la tumbaku limepata anguko la bei, ni eneo ambalo tunaiomba Serikali iangalie kwa kina. Zao la tumbaku limeporomoka kutoka bei ya awali iliyokuwepo mwaka 2025, leo hii zao la tumbaku linauzwa wastani wa dola 1.9 kutoka wastani wa dola 2.3 iliyokuwepo mwaka 2025. Ni anguko kubwa ambalo linapelekea wakulima wa zao la tumbaku washindwe kukidhi mahitaji yao na kushindwa kurejesha mikopo ambayo walikopa kupitia vyama vya ushirika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishauri Wizara iangalie katika eneo hili, waangalie mjengeko wa bei ili waufumue, hasa kwenye gharama za uzalishaji ambazo zimekuwa kubwa sana kuliko kile ambacho mkulima anakitarajia kukipata. Wakulima wamekopa pembejeo za gharama ya juu sana mwaka huu, mfuko mmoja upo zaidi ya shilingi 160,000, ambao anakatwa mkulima kwenye eneo la uzalishaji, lakini bei anayoenda kuuza, ni ya chini kiasi kwamba hataweza kurejesha ule mkopo aliokopa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali iangalie, kwenye maeneo ambayo hasa gharama ambazo zinanufaisha kutoka kwenye kilo inayozalishwa ya zao la tumbaku, vyama vya ushirika waangalie na wadau mbalimbali ili waweze kumsaidia huyu mkulima aweze kumudu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua, siyo jambo ambalo limetokea hapa tu kwetu, ni baada ya ongezeko la uzalishaji duniani limesababisha zao hili liweze kupata mtikisiko. Sasa mahala ambapo panapotokea mtikisiko lazima Serikali iweze kutengeneza fidia ya kumsaidia huyu mkulima ili aweze kurudi tena kwenye eneo la uzalishaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni zao la pamba. Mkulima wa zao la pamba bado hajanufaika kwa kiwango kikubwa. Bei anayopewa ni ndogo; anapata kati ya shilingi 1,000 na bei ya juu ni shilingi 1,060. Hata hivyo, bahati mbaya gharama ambazo anachangia huyu mkulima hasa kwenye mfuko wa pembejeo wa pamba ambao unapita bodi ya pamba, nilikuwa ninashauri kwenye eneo hili Mheshimiwa Waziri anajua pembejeo lazima mkulima apate. Hata hivyo, bado tuangalie gharama zile ambazo anazitumia huyu mzalishaji zinamwelemea, anashindwa kupata uzalishaji ambao utamfanya arejee kwenda kwenye kuzalisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba eneo hilo badala ya kutumia zile shilingi 300 kwa ajili ya mfuko wa pembejeo, tunashauri angalau nusu iende kwenye mfuko wa pembejeo na nyingine iende ikamfidie huyu mkulima aweze kupata fedha. Ni muhimu sana. Ukiangalia kwenye maeneo haya ya uzalishaji, yanaweza yakatupeleka kupata uzalishaji ambao ni mzuri na wananchi wakaneemeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la miradi ya umwagiliaji. Miradi mingi ya umwagiliaji imefeli, haijakuwa vizuri na haiendi kwa sababu hakuna fedha ambayo imefika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mradi wa skimu ya umwagiliaji ya Karema ambayo ni ya muda mrefu. Tumetembea na Mawaziri wa kila aina; Waziri aliyeteuliwa kwenye Wizara ya Kilimo, amefika kwenye eneo lile la mradi. Eneo lile ni kero kubwa kwa wananchi na aibu kwa sisi tunaoisimamia Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri, atakapokuwa anahitimisha hotuba yake, tunataka tupate mwafaka wa mradi wa skimu ya umwagiliaji ya Karema ambao bado haujafanyiwa kitu chochote. Awali kabla ya kuweka mradi ule, ulipokuwa umeanzishwa na Serikali, wakulima walikuwa wanufaika, wanapata fedha zao kwa ajili ya uzalishaji, lakini baada ya kuweka miundombinu mibovu ambayo haikuweza kukidhi mahitaji, ule mradi ulisababisha wakulima wengi kuanza kupata hasara kubwa kwa ajili ya mkondo wa maji kubadili uelekeo wake uliokuwepo awali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana kwenye eneo hili la miradi ya umwagiliaji Serikali ifanyie kazi na kwenda kuiona na kuhakikisha wanapeleka wakandarasi ambao wanaweza kufanya kazi vizuri wakawatumikia Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo tu huo mradi wa Skimu ya Karema, kwangu nina mradi mwingine wa skimu ya umwagiliaji ya Kabageni, Skimu ya Iloba, zote hizo bado hazijakamilika. Ninaomba sana, kwenye maeneo haya, yatatusaidia sana kuzalisha, na sisi tunayo mabonde mengi na tunazalisha mpunga kwa kiwango cha juu sana isipokuwa miundombinu ndiyo ambayo haipo sawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba mwendelezo kwenye mabonde ya Mto Katuma, Mto Nyamasi tuweze kupata skimu za umwagiliaji ili ziweze kuwasaidia wananchi kwenye maeneo haya. Miradi ya umwagiliaji ndiyo pekee itakayoweza kuwasaidia wananchi waweze kujikwamua kwenye mfumo wa kilimo chenye uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la masoko, Wizara tunahitaji ishughulike kuwasaidia wananchi kwenye maeneo hasa ya uzalishaji kwenye mazao yote ambayo yapo nchini. Korosho, pamba, chai, kahawa bado masoko siyo mazuri kwa sababu masoko haya hayasimamiwi vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri, atengeneza mifumo ambayo itawasaidia Watanzania ili wananchi wanapokuwa wanazalisha wawe na uhakika wa masoko ya kwao. Mwaka huu tumezalisha mahindi mengi. Kwa kuwa Serikali imetambua uzalishaji ambao ni mkubwa karibu kila sehemu, ninaomba sasa Serikali ijikite kuwasaidia hawa wananchi waweze kupata masoko mazuri ambayo yatawasaidia kuwa na kipato kizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwa kunipa nafasi, ninaunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)